Na Mwandishi Wetu

WADAU wa maendeleo wameombwa kuendelea kusaidia sekta ya kilimo nchini Tanzania, hasa kwa kundi la vijana na wanawake ili kuhakikisha wanaleta mchango katika sekta hiyo.

Wito huo ulitolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban wakati akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano kujadili fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Kilimo na namna ya kutafuta rasilimali fedha za kukabiliana na uhimilivu wa mabadiliko ya Tabianchi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban akizungumza wakati wa Mkutano wa Pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku, Azerbaijan.

Mkutano huo uliofanyika Pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku, Azerbaijan na kuandaliwa na Wizara ya Kilimo na Shirika Care Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu Amina amesema upatikanaji wa ufadhili endelevu na wa muda mrefu bado ni changamoto inayoendelea kwa nchi zinazoendelea hivyo ni wakati muafaka kwa wadau kusaidia katika sekta hiyo muhimu ili kupata rasilimali fedha za kutosha ili kuleta mageuzi.

Wajumbe mbalimbali kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa Pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku, Azerbaijan.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Amina ameshukuru Serikali ya Norway kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta ya kilimo kinachohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi ajenda na vipaumbele vya kuleta mabadiliko katika kilimo kwa lengo la kuongeza ualishaji wa mazao.

Alifafanua kuwa mikakati na sera zinaeleza kuwa ili kukuza ujuzi kwa wakulima inapaswa kutoa motisha kwa ushiriki wa sekta binafsi, kuimarisha minyororo ya thamani na shughuli za uzalishaji, kuhakikisha usalama wa chakula na uwekezaji wa miundombinu.

“Tanzania imejikita katika kuhakikisha usalama wa chakula huku ikijenga mifumo jumuishi zaidi, endelevu, yenye lishe na ustahimilivu. Katika COP 29 hata tunapoangazia ajenda tofauti, bado tunahimiza washirika tofauti kuendeleza mifumo ya chakula na hatua za hali ya hewa katika muktadha wao wa kipekee,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban (wa sita kushoto) akiwa katika picha ya pamja na ujumbe wa Tanzania na Wadau wa maendeleo mara baada ya Mkutano wa Pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaoendelea jijini Baku, Azerbaijan.