Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sera za Kijamii Zanzibar, ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mohammad Yussuf Mshamba amesema ni wakati muafaka wa serikali kurejesha mchakato wa Katiba Mpya.
Ameyasema hayo leo Juni 15, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Mjadala wa wazi iliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) juu ya ‘Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya’.
Amesema ni muda muafaka wa kuanza kwa mchakato huo ambao ulikwama kwa takribani miaka 10.
“Hili suala linahitaji utayari wa serikali, hivyo tunaomba irudishe tena mchakato huu na Rasimu ya Warioba inatosha kuwa pa kuanzia. Na Mchakato huu usihusushe wanasiasa bali ishirikishe wananchi wajitokeze kushiriki.
“Hivyo lazima kuwe na njia ambayo itasaidia kupata maoni ya wananchi ambapo hapo ni suala la utayari tu serikali na Chama kilichopo madarakani, inawezekana chama kinataka twende kwenye Uchaguzi ujao tukiwa bado hatujapata Katiba Mpya,” amesema.
Akichangia mjadala huo, Mwanafunzi wa Chuo cha Sheria, Queen Elizabeth Francis amesema kupatikana kwa Katiba Mpya ndo suluhisho kwa Nchi na itaondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika Katiba iliyopo ya mwaka 1977.
“Naamini Katiba Mpya itakwenda kuleta suluhisho katika nyanja mbalimbali nchini, kwanza ihusisha wananchi kwa ujumla katika makundi tofauti tofauti waweze kutoa maoni yao tofauti na ile ya mwanzo ambayo imepitwa na wakati,” amesema.
Awali Akifungua mjadala huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Mariam Othuman amesema wameshafanya mijadala hiyo katika Mkoa wa Arusha, Mwanza na Mbeya na kiu kubwa ya wananchi ni kupatikana kwa Katiba Mpya.
“Tangu tumeanza kufanya hiyo mijadala hii, maoni ya wananchi ni kwamba wanataka Katiba Mpya kwani wameona hii iliyopo ina mapungufu na inahitaji mabadiliko. Kwahiyo wote ukiangalia mrengo wao nadhani ni wakati muafaka kwa Tanzania kupata Katiba Mpya.
“Na sisi tunasisitiza kwamba kabla ya hayo mabadiliko ya Katiba Mpya lazima wananchi waelewe kwamba hii iliyopo, isije kuwa wanahitaji Katiba Mpya lakini hii iliyopo hawajui ina kitu gani. Kwahiyo sisi tunajielekeza katika kuwaelimisha kwanza, na kisha kuchukua maoni yao,” amesema.