*Butiku asema amepambana na rushwa, afurahi 4R kurejesha mshikamano

*Dk. Chegeni: Licha ya uhaba wa fedha za kutosha, amekamilisha miradi aliyoirithi

* LHRC wadai bado kuna changamoto kubwa katika mifumo ya sera, sheria

*TAMWA yasifia ujasiri, uthubutu alioonyesha tofauti na matarajio ya wengi

Na Waandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kesho Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka minne tangu aingie madarakani. Ni miaka minne ya kivumbi na jasho inayotajwa kulijengea heshima Taifa la Tanzania kimataifa.

Rais Samia aliapishwa kushika madaraka haya makubwa ya kiuongozi nchini kwa mujibu wa Katiba Machi 19, 2021 akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Rais Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam.

Alipoingia maradakani, alikuta nchi inakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo za kuzuiliwa kwa mikutano ya kisiasa, watu kutekwa, kuuawa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Baada ya kuingia madarakani amesema: “Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu, kufarijiana, kuonyesha upendo, kuenzi utu wetu tukiwa pamoja, ni wakati wa kutazama mbele kwa shaka, kwa matumaini na kujiamini.

“Si wakati wa kutazama yaliyopita, ni wakati mzuri wa kutazama yajayo, si wakati wa kunyoosheana kidole, ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele, kufutana machozi na kufarijiana ili kuweka nguvu pamoja na kujenga Tanzania mpya.”

Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, amesema Rais Samia amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na kurejesha amani, umoja na mshikamano wa taifa.

“Amefanya kazi nzuri ya kuleta umoja wa kitaifa kwa kipindi chake, anapambana dhidi ya rushwa licha ya ukweli kwamba bado kuna viashiria vya aina hii. Alikuja na 4R zimekuwa na tija, tumeona zimesaidia kuleta maridhiano mazuri katika nyanja tofauti, kila mmoja wetu anapaswa kumsaidia, maana Tanzania ni nchi yetu na hatuna nchi nyingine.

“Zile 4R zake anazisema kwa nia njema, lakini ningependa zisimamie kusema ukweli katika kutenda haki kwa Watanzania na safari hii tunayo nafasi nzuri mno, tunakwenda kuchagua viongozi, twende tunajua tuna wajibu wa kutenda haki, kusema ukweli, tuna wajibu wa kumsikiliza Rais wetu anasema nini. Katika jambo hili tusije tukarudia makosa, yakitokea tusije tukamsingizia, ni sisi tutakuwa tumesahau tulikotoka,” amesema.

Pia amesema tusiendelee na rushwa, na lazima lisimamiwe kwa kuwa Rais Samia amekuwa akisisitiza.

Amesema kwa sasa nchi inakwenda vizuri na bado nafasi ipo ya kutamka mema na kusifia na yale mabaya bado kuna nafasi ya kuyakemea.

“Bado nafasi ipo ya kuyasema yote niliyosema hapo juu. Bado iko nafasi ya kusahihisha. Ukisikiliza mazungumzo kwenye mitandao au kwenye nyumba tunazokaa wakati tunakunywa bia, Watanzania wanaogopa kusema, wanasema hawasemi lakini wanasema. Huo ni uzuri, tusiwe kama hatuoni, tushukuru. Kuna vyama wanasema hawajaridhika na uhusiano, lakini wanasema, nchi yetu ina amani ya kutosha.

“Tukiendelea kuzungumza na kulinda uhuru wetu, tuzungumze kwa staha, kusahihisha kwa ujasiri na wanaosahihishwa wawe majisiri wa kupokea masahisho. Ukiwa na moyo hivi wa kuogopa husahihishi, lakini tusahihishe kwa adabu, heshima, maana siku zote ujasiri unatokana na ukweli. Hauwezi kuwa jasiri kama unasema uongo,” amesema.

Vilevile amesema Watanzania walikilinda misingi hiyo kwa ujasiri itasaidia mambo mengi ndani ya taifa.

“Wakati mwingine sisi kama binadamu tunakasirika, hasira yetu ionekana ni ya ukweli, haina nia mbaya, tutakuwa tumesaidia mno kusimamia misingi iliyowekwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere,” amesema.

Naye Mbunge wa zamani wa Busega na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Raphael Chegeni, amesema Rais Samia amefanya mengi na makubwa licha ya kuchukua nchi ikiwa katika mazingira magumu.

“Watu wengi mwanzoni hawakuamini wala kutarajia kwa mara ya kwanza Rais mwanamke anaweza kutokea Tanzania na akaweza kumudu majukumu yake kikamilifu, lakini kwa majaliwa ya Mungu, kwa neema na baraka alizojaliwa ameweza kufanya mambo makubwa yasiyotarajiwa na kuamini.

“Mosi, ameweza kusimamia na kukamilisha miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake katika mazingira magumu ya kutokuwa na fedha za kutosha. Alijenga nidhamu ya kusimamia nchi, kuifungua ndani na nje ya mipaka. Cha kwanza alichofanya ndani ya nchi alileta utulivu na amani na kila Mtanzania walau anaweza kujua kesho yake anaweza kuamkaje, iwe kwa wafanyabiashara, si kwa wananchi wa kawaida,” amesema.

Pili, amesema alihakikisha misingi yote ya utawala wa sheria inazingatiwa, huku akiondoa mambo ya vikosi kazi (task force) yaliyoumiza wananchi na kuna watu walijifanya ‘miungu watu’ kwa kuwaumiza wafanyabiashara lakini yote yakapigwa marufuku.

“Kwa vile alikuwa na changamoto ya mapato na rasilimali fedha, alichofanya ni kuifungua nchi na mataifa ya nje na kujenga uhusiano uliochagiza kuirudisha Tanzania katika ramani ya dunia. Yamesaidia kupatikana kwa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi.

“Amekamilisha miradi mikubwa kama Bwawa la Nyerere, SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kusambaza umeme vijijini. Nakumbuka bajeti za TARURA zimeongezwa. Kwa mfano Busega ilikuwa inapata Sh milioni 600 sasa hivi inapokea Sh bilioni 2.7 kwa mwaka, hili ni badiliko kubwa,” amesema.

Kuhusu makusanyo ya kodi, amesema na kuongeza: “Yameendelea kupanda mwaka hadi mwaka na hii  ni dalili njema hata uchumi unazidi kuimarika. Kuna watu walipiga kelele wakati anafanya kazi ya kubinafsisha Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya DP World.

“Hawakujua kumbe mama aliona mbali, leo hii makusanyo yameongezeka maradufu kwa kusaidia kufungua biashara na upakuaji wa mizigo umekuwa mzuri.”

Kuhusu mabadiliko ndani ya CCM, amesema Rais Samia amefanya makubwa mno, yakiwamo ya kusimamia na kurudi katika misingi ya haki, misingi ya usawa, misingi ya kutambua kila mwanachama ana haki, ameondoa ile ‘okotaokota’ iliyokuwapo siku za nyuma ndiyo maana tunampenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Dk. Rose Ruben, amesema Rais Samia ameonyesha ujasiri na uthubutu mkubwa tofauti na matarajio ya watu wengine.

Amesema hali hiyo imetokana na kutimiza malengo yake aliyoahidi wakati anaingia madarakani mwaka 2021.

Pia amesema malengo yake yamenufaisha kila Mtanzania, hasa mwananchi wa kawaida, kuishi kwa amani na kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine bila matatizo.

“Katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi, nchi yetu inaendelea kukuza uchumi. Kwa upande wa uwekezaji umeongezeka kwa kasi, na viwanda vinaendelea kuimarika.

“Hii inaonyesha jinsi wawekezaji wanavyotuamini kutokana na mazingira salama ya biashara na hakuna mtu anayeweza kuwekeza eneo lisilo salama au utulivu,” amesema.

Kuhusu miundombinu, amesema serikali imejizatiti kuboresha sekta mbalimbali kama vile umeme, barabara, afya na maji.

“Ninaamini ujasiri wa Rais wetu umekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo haya, ameweza kuendesha nchi kwa ufanisi. Tumejipatia heshima kubwa kimataifa kutokana na juhudi zake ndiyo sababu Tanzania inajulikana kwa kutoa fursa nyingi za biashara na uwekezaji.

“Hapa Afrika, kuna maeneo yanayoongozwa na wanaume hayana amani, huku watu wakikabiliwa na njaa. Tanzania, tunaendelea kuishi vizuri na tuna chakula cha kutosha. Hali hii inatofautiana na mataifa mengine yanayokabiliwa na machafuko na ukosefu wa amani,” amesema.

Kuhusu ufanyikaji mikutano mikubwa ya kimataiafa, amesema imeonyesha Tanzania imeaminika zaidi kutokana na uongozi bora.

Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Deogratius Bwire, amesema Rais Samia amefanya vizuri baadhi ya maeneo japo bado kuna sehemu hazijafikiwa kama ilivyotarajiwa.

Kwa upande wa wanawake, amesema Rais Samia amehakikisha upatikanaji wa haki zao unakuwa juu na kupunguza ukatili wa kiuchumi.

“Amezingatia haki za kiuchumi kwa wanawake, na kuna wakati asilimia za halmashauri zilisitishwa ili kuboresha maisha yao na katika sekta ya elimu amefanya kazi kubwa kwa kuboresha upatikanaji wa fedha za wanafunzi wa elimu ya juu wanaokidhi vigezo,” amesema.

Pamoja na hali hiyo, amesema changamoto kubwa iko kwenye mifumo ya sera na sheria na kuna vikwazo vigumu kuviondoa kutokana na malengo ya kisiasa.

“Katika masuala ya haki za kisiasa na kiraia, mwanzoni alijitahidi kuleta mabadiliko, kama vile kufungua mikutano ya vyama vya siasa na kuruhusu vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa kufanya kazi zake,” amesema.

Kuhusu mazingira ya kisiasa, amesema yameimarika tofauti na miaka ya nyuma.

“Tunaona vyama vya upinzani kama vile CHADEMA na ACT-Wazalendo vimeimarika, tofauti na awamu zilizopita kulipokuwa na changamoto nyingi,” amesema.