Sekta za umma, binafsi na wadau wa maendeleo kwa jumla, wameshauriwa kuzingatia matumizi bora kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na fursa kwa jinsia zote katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wametakiwa pia kulenga taswira ya nchi kufanikisha takwimu sahihi katika Nyanja mbalimbali kwa manufaa ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zilizopo miongoni mwa wananchi, hivyo kutoa fursa kwa serikali ba wadau kutafakari uboreshaji ya maisha ya jamii.
Hayo yalisemwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.
Alisema maadhimisho hayo ni muhimu kwani yanalenga kutoa taswira ya hali ya nchi na kuonesha changamoto zinazowakabili wananchi na kuwezesha serikali kuboresha maisha ya wananchi.
Pia, Dk. Bilal alisema maadhimisho yanalenga kuihamasisha jamii katika Bara la Afrika juu ya umuhimu wa matumizi ya takwimu katika kupanga maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Alisema ili kuleta msukumo wa matumizi ya takwimu katika nyanja mbalibali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kila mwaka maadhimisho haya hutoa ujumbe maalumu wenye lengo la kuongeza hamasa na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya takwimu, mbapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kumjali kila mwanamke na mwanamme: Kutoa takwimu kijinsia kwa matokeo bora ya maendeleo.”
“Kaulimbiu hii imechaguliwa iwe kichocheo cha kutumia takwimu zilizoainishwa kijinsia katika kubuni, kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya kiuchumi na kijamii barani Afrika, vilevile zitumike katika kufanya uamuzi muhimu wa kisera kuhusu jinsia, ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya Bara la Afrika kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ushiriki wa mwanamke katika masuala ya maendeleo.
“Pamoja na msisitizo huo, ningependa nieleze kuwa takwimu zilizoainishwa kijinsia ni baadhi ya ambazo hutumika katika nchi zetu kila siku, kama ilivyo kwa takwimu za kiuchumi, kilimo, afya, ajira na nyinginezo katika sekta zote za uchumi,” alisema Bilal.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alisema asilimia 70 ya vyakula vinavyotumika katika kaya binafsi hapa nchini vinazalishwa na wanawake, ingawa bado kuna ukweli kuwa pato la Taifa linachangiwa na watu wa jinsia zote (wanaume na wanawake).
“Matokeo ya takwimu hizi kisera yanatuonyesha kuwa kuna umuhimu wa kumpatia mwanamke uwezo zaidi kielimu, ajira na mahitaji muhimu yanayohitajika katika maendeleo ya uchumi wa nchi,” alisema Simba.
Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2010 kuhusu afya ya mama na motto, asilimia 37 ya wanawake walioko katika ndoa wamefanyiwa ukatili na wenzi wao.
Alitaja aina ya ukatili huo kuwa ni wa kimwili, kiakili, kisaikolojia au unaohusu ngono, huku akisisitiza kuwa ukatili ni adui wa maendeleo ya nchi. Alitoa wito kwa wanawake kutokubali kufanyiwa ukatili.