Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Meneja wa Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu kutoka NHIF Bi. Rose Ntundu ametoa ufafanuzi dhidi ya taarifa za upotoshaji zinazosambazwa mtandaoni kuhusu watumishi 148 wa NHIF kuhusika kwenye vitendo vya udanganyifu.
Ntundu amesema kuwa kwenye ripoti ya CAG iliyotolewa Machi 2023 ilieleza kuwa kati ya watumishi 148 walibaonika wamehusika kwenye vitendo vya udanganyifu, watumishi 129 walitoka kwenye vituo binafsi vya kutolea huduma huku watumishi 19 pekee walitoka NHIF na si kama inavyoripotiwa kuwa watumishi wote ni wa NHIF.
Amebainisha kuwa tayari hatua za kisheria na nidhamu zimechukuliwa kwa watu hao kupitia Mamlaka zao za ajira, Bodi au Mabaraza ya kitaaluma huku kwa watumishi wa NHIF waliohusika wote tayari wamechukuliwa hatua.
“Nichukue fursa hii kuwasihi wanachama wetu, watoa huduma na waajiri kujiepusha na vitendo vya udanganyifu, Mfuko utachukua hatua kwa mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu” amesisitiza Bi. Ntundu.