Benki ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL) imeanza msako dhidi ya watu binafsi, vikundi vya wajasiriamali na kampuni zinazodaiwa mikopo na benki hiyo baada ya kushindwa kufanya marejesho ndani ya muda kulingana na masharti ya mikopo.
Msako huo unafanywa na benki hiyo kupitia Kampuni ya Tanfin Consultant E.A Ltd ya jijini Dodoma ambayo imepewa ridhaa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kutoa huduma kwa vyama vya ushirika nchini.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Haidan Bangula, amezungumza na JAMHURI na kukiri kampuni yake kuendesha operesheni hiyo ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wa benki hiyo wakianzia Wilaya ya Siha.
Amesema kwa Wilaya ya Siha ambako wadaiwa wengi ni vikundi vya wajasiriamali pamoja na vikundi vya ushirika, wamepata mafanikio makubwa, ikiwamo kuwabaini wadaiwa na kuwapa hati za madai na wao kukiri kudaiwa.
“Mafanikio yetu ya awali ni kuwabaini wadaiwa na katika kipindi cha mwezi mmoja tulioendesha operesheni yetu katika Wilaya ya Siha tumeweza kukusanya zaidi ya Sh milioni 25. Haya kwetu ni mafanikio makubwa,” amesema.
Hata hivyo amesema changamoto kubwa waliyokutana nayo ni kwa baadhi ya wanavikundi kufariki dunia na wengine kuhama mkoa. Kwa mujibu wa maelezo yake, changamoto nyingine ni dhamana za mikopo zilizowekwa na wadaiwa hao kuharibika na nyingine kuuzwa.
Mkurugenzi huyo ameliambia JAMHURI kuwa wanavikundi wengi waliopewa mikopo na KCBL waliweka dhamana ya mali zinazohamishika yakiwamo makabati, meza na televisheni na kutokana na mikopo hiyo kukaa muda mrefu bila kurejeshwa, baadhi ya dhamana hazipo tena mikononi mwa wadaiwa hao.
Kwa mujibu wa orodha ya wadaiwa hao sugu iliyotolewa na Benki ya Ushirika hivi karibuni, baadhi ya waajiriwa wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa wadaiwa. Mkurugenzi huyo amesema miongoni mwa wadaiwa hao wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha.
“Kwa kweli raia wa kawaida hawana shida. Tumewapigia simu wanakiri kudaiwa na wanaomba wapewe muda wa kulipa, changamoto ipo kwa waajiriwa hasa katika Jeshi la Polisi, hawa kwa kweli wanatusumbua sana, hawataki kulipa,” amesema.
Kutokana na changamoto hiyo, mkurugenzi huyo anakusudia kuonana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah, kuhusu maofisa wake wanaodaiwa mikopo na benki hiyo, vinginevyo ameeleza kuwa atamwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani.
Hata hivyo kampuni hiyo imebaini baadhi ya madudu yaliyokuwa yakifanywa na sehemu ya waliokuwa watumishi wa benki hiyo wasiokuwa waaminifu hasa Idara ya Mikopo ambao walikuwa wakipokea marejesho ya wadaiwa hao na kushindwa kuyaingiza kwenye mfumo wa benki.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa baadhi ya watumishi hao walikuwa wakipokea fedha za marejesho kutoka kwa wadaiwa hao na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi bila kuziingiza kwenye kumbukumbu za benki.
Kutokana na hilo, kampuni hiyo ilijikuta ikikumbana na wakati mgumu kwa baadhi ya wadaiwa ambao walidai walikwishalipa madeni yao huku kukiwa hakuna kumbukumbu za kibenki kuonyesha kuwa walilipa.
“Jambo baya zaidi walikuwa wakiwapigia simu hao maofisa na wao wanawaambia wasilipe chochote maana hawadaiwi lakini ukienda kwenye kumbukumbu za benki madeni hayo bado hayajalipwa,” amesema.
Msako huo wa wadaiwa sugu unakuja siku chache baada ya bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo kuwafukuza kazi maofisa wake watano akiwamo meneja mkuu wa benki hiyo, Joseph Kingazi, wakituhumiwa kuhusika katika ufisadi wa mabilioni ya fedha za benki hiyo.
Maofisa wengine wa benki hiyo waliofukuzwa kazi ni aliyekuwa meneja mikopo, Ombeni Masaidi na Asha Kisega pia kutoka Idara ya Mikopo, Doe Mashinga aliyekuwa mtunza fedha na Ukundi Mmochi aliyekuwa katibu muhtasi wa meneja mkuu.
“Uongozi wa benki unapenda kuutangazia umma kuwa watajwa hapo juu si wafanyakazi tena wa Kilimanjaro Co operative Bank Limited, hivyo benki haitahusika na taarifa au miamala yoyote itakayofanywa na watu hawa,” imesema taarifa hiyo.
Kabla ya kufukuzwa kazi maofisa hao walipewa barua za kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na baada ya uchunguzi kukamilika wakapewa barua za kufukuzwa kazi.
Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo aliyezungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake aliliambia JAMHURI kuwa maofisa hao wamefukuzwa kwa tuhuma hizo za kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika ufisadi wa mabilioni ya fedha ambao umeifanya benki hiyo kuyumba mara kwa mara.
Mjumbe huyo akataja eneo ambalo limeiweka pabaya benki hiyo na kufikia hatua ya kusimamisha utoaji wa huduma ni Idara ya Mikopo, ambapo maofisa hao wanatuhumiwa kujihusisha na utoaji wa mikopo usiozingatia taratibu za benki.
Alitolea mfano wa vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS) vipatavyo 18 pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Same (VUASU) ambavyo vilivuka na deni la zaidi ya Sh bilioni 1.173 katika msimu wa 2016/2017, kwamba hadi sasa vyama hivyo vimeshindwa kurejesha mkopo huo.
“Kwa utaratibu chama kinapewa fedha kulingana na kiwango cha kahawa wanayokusanya, lakini vyama vingi vimepewa pesa nyingi isiyoendana na kiwango cha kahawa wanayoratajiwa kukusanya na matokeo yake wameshindwa kuzirejesha mpaka sasa,” amesema.
JAMHURI linayo orodha ya vyama hivyo na kiasi cha mkopo walichopewa na kiasi cha pesa iliyorejeshwa KCBL na kati ya Sh bilioni 1.9 zilizotolewa kwa vyama hivyo katika msimu huo, Sh milioni 700 tu ndizo zilizorejeshwa hadi kufikia Juni 30, mwaka 2017, huku Sh 1,173,869,049 zikiwa bado ‘mikononi’ mwa vyama hivyo.
Vyama hivyo vya ushirika wa mazao ni miongoni mwa wanahisa 245 wa benki hiyo wakiwamo pia watu binafsi 307 pamoja na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na ilikuwa ikihudumia wilaya sita za Mkoa wa Kilimanjaro.
Benki hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 69 na Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa na lengo la kuwakwamua kiuchumi wakulima wa zao la kahawa mkoani humo kwa kunufaika na mikopo yenye riba nafuu kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika.
Januari mwaka jana benki hiyo ilikuwa miongoni mwa benki tatu zilizopewa muda wa miezi sita na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa Sh bilioni tano, lakini mpaka sasa benki hiyo imeshindwa kutimiza matakwa hayo.
Baada ya tangazo hilo la BoT, KNCU ilitangaza kuuza shamba lake la kahawa la Lerongo lililopo Wilaya ya Hai likiwa na ukubwa wa ekari 581, kwa ajili ya kuinasua benki hiyo katika rungu la BoT, kabla ya waziri mkuu kuzuia uuzwaji wa shamba hilo.