Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Katavi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limemkamata na linamshikilia mzeee mmoja aliyefahamika kwa jina la Simbuka Makande (62), mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Magengase Mkoa wa Tabora kwa tuhuma za kumbaka mwanamke ambaye ni mfanya biashara wa madini baada ya kumrubuni kuwa atamsafishia nyota ya kupata mali
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi All Makame Hamad amethibitisha kutokea kwa tukio hilo amesema kuwa mlalamikaji ni mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Kijiji cha Katuma Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi.
Amesema kuwa mganga huyo wa kienyeji alikuwa ametokea mkoani Tabora na kufikia katika kijiji hicho cha Katuma na kukodi chumba kwenye nyumba ya kulala wageni inayoitwa Bunga .
Kamanda Hamad amesema kuwa mhanga wa tukio hilo naye alikuwa amefikia kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni huku akiwa anaendelea kufanya shughuli za biashara yake ya madini ya dhahabu yanayochimbwa kwenye Kijiji hicho cha Katuma .
Kamanda amesema kuwa ndipo mwanamke huyo alipokutana na mganga huyo ambapo mganga alimweleza mwanamke huyo kuwa anao uwezo wa kuwasafishia watu nyota zao ili waweze kupata mafanikio kwenye shughuli zao na moja ya mashariti yake ni kushiriki naye tendo la ndoa .
Amesema ndipo mganga huyo alimrubuni na kushiriki naye tendo hilo kwa nyakati tofauti tofauti na pia mhanga aliweza kumpatia mganga huyo shilingi 1,060,000 (milioni moja na elfu sitini) .
Kamanada amebainisha kuwa pia mganga huyo anatuhumiwa kufanya kitendo hicho kwa watu wengine watatu mkoani Katavi na kujipatia sh. 4,600,0000 (milioni nne na laki sita) .
Amesema kuwa mtuhumiwa amekuwa wakiwaeleza walalamikaji kuwa tayari amewasaidia wafanyabiashara wengi pamoja na viongozi mbalimbali hapa nchini ambao tayari wamepata mafanikio kupitia yeye.
Kamanda Makame amesema mtuhumiwa amekamatwa na enaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi na mara upelelezi utakapokamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili .