Wiki iliyopita, nilisema Rais John Magufuli amedhamiria kurejesha heshima na wajibu wa Serikali kwa wananchi.
Nikasema hayo hayatawezekana endapo ataogopa lawama na hivyo kuruhusu ufisadi, rushwa, uzembe na udhaifu mwingine kwa sababu tu ya kuwafurahisha walionuna.
Bado naamini Rais ana wajibu wa kuhakikisha wachache wananuna, ili wengi wafurahi. Huo ndiyo uongozi. Kiongozi hawezi kumfurahisha au kukidhi matamanio ya kila mtu.
Mahubiri ya sheikh au padri, yanaweza kufurahiwa na waumini wanaomtii Mungu, lakini wafuasi wa shetani hawawezi kuyafurahia. Katika mazingira na mgawanyiko wa aina hiyo, sheikh au padri atafanya nini ili ayafurahishe makundi yote? Haiwezekani.
Kabla ya kuushambulia uongozi wa sasa, ni vema na haki tukajiuliza Rais Magufuli na wasaidizi wake wamepokea uongozi nchi ikiwa katika hali gani? Nimepata kusema huko nyuma kuwa kabla ya Rais Magufuli, mifumo yote katika nchi yetu ilishakufa, isipokuwa mfumo mmoja tu wa kufanya mambo ovyo! Mfumo wa kutenda mambo ovyo ndiyo uliokuwa umesalia ukifanya kazi zake barabara! Kuubomoa mfumo wa aina hiyo uliokwishaota mizizi si jambo dogo au la kufurahiwa na baadhi ya watu.
Ukiwaacha wamachinga leo wanauza mitumba yao kwenye ukuta wa Ikulu, siku ukitaka kuwaondoa watalalama kwa kelele za kuonewa! Kulalama kwao kunaweza kuwa kwa muda tu.
Rais Magufuli ameanza kuongoza nchi yenye watoro wengi katika ofisi za umma. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Novemba, mwaka jana alisema haya: “Tulikuwa tunagongana huko hewani utadhani huku nyumbani kunaungua moto. Tunapobaki huku ndani tunaokoa hela nyingi na nina hakika (Dk. Magufuli) ataingilia hata kwenye mashirika. Kuna wakuu wao wanasafiri kila siku, nina hakika wataguswa katika hili. Lazima kuziokoa pesa na kufanyia shughuli nyingine, mimi naunga mkono mia moja kwa mia hili…kitendo cha Rais Magufuli kufuta safari za nje hakina maana kwamba uhusiano wa Tanzania na nchi hizo unakufa. Hajakataza wageni, wafanyabiashara wa dunia wala wawekezaji kuja Tanzania, hata wawekezaji hawawezi kukataa kuja Tanzania waache gesi, dhahabu, almasi au tanzanite.”
Wakati Rais Magufuli akizindua Bunge la 11 alisema: “Napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, mashirika ya umma na taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya Sh bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
• Tiketi za ndege zilitumia Sh bilioni 183.160;
• Mafunzo nje ya nchi yalitumia Sh bilioni 68.612;
• Posho za kujikimu zilitumia Sh bilioni 104.552
Fedha hizi zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini kama afya, maji, elimu, umeme na kadhalika. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami. Tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? Nyumba ngapi za walimu? Madawati mangapi? Hivyo, tunapodhibiti safari za nje tunawaomba waheshimiwa wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”
Uamuzi huu ni mzuri. Umelenga kuokoa fedha za umma ili ziwanufaishe Watanzania wengi. Tunaelekea kutimiza mwaka mmoja tangu uamuzi huu uanze kutekelezwa. Badala ya kumlalamikia Rais, tunapaswa kutathmini faida zake.
Tujiulize, utaratibu ule wa rais wetu kwenda Marekani akakaa huko kwa wiki tatu ulikuwa na tija? Kipi alichokipata kwa hizo wiki tatu ambacho sasa nchi inataabika kwa vile rais wa sasa hasafiri nje?
Kipi ambacho wakulima na makabwela wengine wa Tanzania wanakikosa kwa kufutwa safari za viongozi wa umma nje ya nchi? Mwaka mzima unaelekea kutimia Rais wetu akiwa hajaenda Ulaya kutembeza bakuli, tumepungukiwa nini? Haya ndiyo tunayopaswa kujiuliza na kuyapatia majibu.
Kuna watu wameshupaa wakitaka Rais asafiri nje ya nchi, wakisema kutofanya hivyo kunaikosesha Serikali yetu fursa nyingi. Sijui, lakini ulimwengu wa leo Rais wetu kuwa na mawasiliano na viongozi wenzake duniani si lazima asafiri.
Dhana hiyo hiyo dhaifu ndiyo inayowafanya wataalamu wetu wa utalii waamini kuwa kwenda kwao kwenye mabanda ya maonesho Ulaya, Marekani au Asia kuna msaada mkubwa wa kuvutia watalii kuja nchini mwetu kuliko matumizi ya kisasa ya mitandao ya kijamii. Kuna njia rahisi na zenye tija zaidi katika kuendesha mambo kuliko zile zilizozoeleka za kusafiri ughaibuni kila siku.
Ndugu zangu, Rais aliyekuta mambo mengi katika nchi yetu yakiwa yametoka kwenye mstari, hawezi kufurahiwa na wale walionufaishwa na mparaganyiko huo. Wapo wanaosema nchi inapaswa kuongozwa kwa kufuata mifumo. Kweli, nchi inaongozwa kwa mifumo iliyobuniwa na kukubaliwa na wengi, lakini tusisahau kuwa mifumo hiyo huwekwa na watu. Hatuwezi kuanza na mifumo. Tunaanza na watu wa kuweka hiyo mifumo.
Kama mfumo wetu wa uwajibikaji ulikuwa umekufa, sharti tumpate kiongozi au viongozi wa kuufufua mfumo huo. Unapotaka viongozi wasisafiri nje ya nchi holela, huwezi kuweka mfumo huo kwa hisia tu. Ni lazima uujenge mfumo huo kwa kuanza kuwabana hao waliopenda kusafiri.
Unapotaka kujenga mfumo wa uwajibikaji ni lazima kwanza uwe na viongozi wa kuuweka huo mfumo ili baadaye watakaofuatwa wabanwe kwa kuhakikisha wanaufuata.
Ulipaji kodi kisheria upo kwa miaka mingi. Mifumo inayomtaka kila Mtanzania kulinda rasilimali za nchi upo kikatiba. Mifumo ya kupambana na ufisadi ipo. Tujiulize, ni kwanini kwa miaka yote mifumo hii ilisinzia au ilikufa? Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliamini ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Katika haya wapi tulipofeli? Wengi wetu wanakiri kuwa tumefeli hapo kwenye uongozi bora. Je, uongozi bora ni upi? Tunaweza kuwa na tafsiri nyingi. Moja ya tafsiri hizo inaweza kuwa uongozi bora ni ule unaosimamia Katiba, sheria na kanuni mbalimbali zinazoiongoza jamii.
Kuwataka watu watumie muda mrefu kufanya kazi badala ya siasa za maandamano, hakuwezi kutafsiriwa kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya uongozi bora.
Kuwabana wakwepa kodi na wezi wa makontena bandarini hakuwezi kuuaminisha umma kuwa viongozi wanaosimamia jambo hilo ni madikteta wasio na sifa ya kuwa viongozi bora.
Uongozi bora ni ule unaohakikisha wananchi wote wanapata huduma za kijamii kadri inavyowezekana kama matokeo ya uchapaji kazi wao na ulipaji kodi.
Kusema haya hakumaanishi kuwa uongozi wa sasa hauna dosari, la hasha. Viongozi wetu wa sasa, kama waliotangulia katika awamu nyingine, ni binadamu. Yawezekana kabisa wakawa na upungufu wao. Hata hivyo, upungufu huo haupaswi kuyafunika mazuri wanayolifanyia Taifa letu na watu wake.
Yapo mambo mengi ambayo kabla ya uongozi wa Awamu ya Tano hatukuyaona. Leo kuna mabadiliko katika maeneo mengi. Watumishi wa umma wametambua kuwa wao ni watumishi kweli wa umma. Walau sasa mgonjwa anaweza kupokewa hospitalini kwa heshima. Barabarani, hata kama ajali zinatokea, walau madereva wanajua kuna nguvu ya dola inayowataka waheshimu sheria za barabarani.
Tunaona hofu ya watu kukwepa kodi kwa sababu wanatambua ukwepaji kodi ni uvunjifu wa sheria za nchi. Tunaanza kuona wafanyakazi katika ofisi za umma wakiwahi kazini na kuwahudumia wananchi.
Walau kwa miezi hii tunaweza kuona nchi ikianza kupata uhai kwenye usafiri wa anga; huku juhudi nyingine zikielekezwa kwenye madaraja, reli na usafiri wa majini. Wanaobeza ndege zilizonunuliwa wanafanya hivyo kwa kukosa uzalendo. Wanasema ni ndege ndogo, ndiyo ni ndogo! Mgonjwa aliyekosa kula chakula kwa muda mrefu, huanza na chakula laini na kwa kiasi. Mwili ukisharuhusu, yuko radhi kula hata ugali wa mtama.
Alimradi tumetoka wodini, tukubali kuanza na hizi, huku tukijiandaa kupata ndege kubwa zaidi. Huu ni mwanzo mwema. Pale viongozi wetu wanapofanya mambo mema kwa manufaa ya nchi yetu, tuungane kuwapongeza na kuwatia moyo. Nchi hii ilishaharibiwa!
Rais na wasaidizi wako, endeleeni kuwaudhi wachache ili walio wengi wawakumbuke daima kwa mema mtakayokuwa mmewatendea.