Hazina ya sanaa, utalii, utamaduni isiyovuma
*Wapo wanaoongozwa na mawingu kuchonga mashetani
*Wamarekani wapendelea ‘mashetani’, Waingereza ‘wanyama’
*Baadhi watumia ‘calculator’ kuwasiliana na wateja Wazungu
*Walilia soko la uhakika, waishutumu Serikali kuwapa kisogo
Umewahi kuzuru kituo cha wachongaji na wauzaji vinyago cha Mwenge, jijini Dar es Salaam? Kama bado, basi fanya hima ufike ujionee hazina ya sanaa, utalii na utamaduni wa Kitanzania iliyotamalaki, ingawa haivumi.
Kituo hiki kinajulikana zaidi kwa Kiingereza Mwenge Carving Centre (MCC). Kipo kando kando ya Barabara ya Mwenge-Ubungo. Kuna vinyago vya kila aina. Ni kivutio cha utalii cha aina yake.
Vinyago vinavyopatikana kwa wingi zaidi hapa ni vya wanyama, ujamaa na mashetani. Katika sanaa ya uchongaji, ujamaa ni vinyago vyenye mkusanyiko au mrundikano wa watu wengi.
Wiki iliyopita JAMHURI ilitembelea MCC na kubaini mengi, ambayo pengine wengi hawajapata kuyajua. Kumbe mawingu ya angani yana mchango wake katika uchongaji vinyago vya mashetani!
Alberto Sivandeka (64) ni fundi wa kuchonga vinyago katika MCC, anapatikana kwenye kibanda namba 10. Ni miongoni mwa wasanii wanaoongozwa na mawingu kubuni uchongaji vinyago vya mashetani.
“Nachonga sana mawingu, naangalia mawingu nachonga mashetani,” anasema Sivandeka katika mazungumzo na JAMHURI.
Anatumia miti aina za mpingo na mninga kuchonga wanyama, watu na vitu vingine mbalimbali. Yeye na wengine hununua miti hiyo kwa wachuuzi wanaoisafirisha kutoka mikoa ya Pwani na Tanga.
Ukimwona mzee huyu ni buheri wa afya. Anasema alianza kujishughulisha na uchongaji vinyago mwaka 1963 mkoani Mtwara, baada ya kufundishwa na kaka yake aliyeitwa Nchupi (alishafariki).
“Nilihamia Dar es Salaam mwaka 1974, nikaweka kituo kule Mkuranga (kwa sasa iko Mkoa wa Pwani) kwa ajili ya kuchonga na kuuza vinyago,” anasema Sivandeka na kuendelea:
“Niliamua kujikita katika uchongaji unisaidie kimaisha lakini kwa sasa kazi hii naiona ngumu, imevamiwa zaidi na watu wenye uwezo mkubwa [kiuchumi] wasio wataalamu [wachongaji].
“Wenye uwezo wanachukua mafundi wanaowatengenezea vinyago majumbani kwao kwa ajili ya kuviuza kwenye maduka yao hapa nchini na kusafirisha vingine kwenda kuviuza Ulaya. Hao ndiyo wanaotuua, unakuta sisi [wachongaji] hatupati wateja.”
Anasema wateja wakuu wa vinyago wanavyochonga ni Wazungu kutoka mataifa tofauti yaliyopo mabara ya Ulaya, Amerika na Asia.
Kwa mujibu wa mzee huyu, Waafrika wanaojitokeza zaidi kununua vinyago katika kituo hiki, japokuwa si mara kwa mara, ni Waganda. Julai hadi Desemba ndiyo msimu mzuri unaochangamsha biashara hii kwa mauzo.
“Julai mpaka Desemba ndiyo kidogo biashara inakuwa nzuri, lakini Januari hadi mwezi huu (Mei) ndiyo sisi tunakuwa watu wa njaa sana,” anasema huku akiendelea kupiga msasa kinyago cha shetani.
Wateja wengi, kwa mujibu wa wachongaji na wauzaji wa vinyago hapa MCC, wanapendelea kununua vinyago vya wanyama, hasa tembo, faru, nyati, twiga na simba.
Inaelezwa kuwa Waingereza na Wachina ndiyo wanaopendelea vinyago vya wanyama, huku Wamarekani na Wajerumani wao wanapendelea vinyago vya mashetani.
“Wamarekani na Wajerumani wanapenda sana vinyago vya mashetani, Waingereza ndiyo hawataki kabisa mashetani,” anasisitiza mchongaji huyu.
Sivandeka anasema bei ya chini kabisa ya kinyago ni kati ya Sh 1,000 na Sh 2,000 ambayo huhusisha zaidi vinyago vya wanyama kama vile swala, simba na tembo wadogo. Bei ya juu kabisa ya kinyago ni Sh 700,000 ambayo huhusisha zaidi vinyago vya ujamaa.
Ukosefu wa soko la uhakika unatajwa kuwa ndiyo kikwazo kikuu kinachodumaza uchumi wa wachongaji na wauzaji wa vinyago hapa MCC.
“Hatuna soko la uhakika, Serikali imetutenga, sana sana viongozi wanachofanya ni kututembelea tu, hawatusaidii angalau hata kwa kutukopesha mitaji,” anadokeza.
Taswira hiyo inamvunja Sivandeka moyo wa kuendelea na shughuli hii, licha ya kumpatia mafanikio kidogo ya kujigharamia ujenzi wa nyumba ya kuishi eneo la Mbagala, Dar es Salaam, kutokana na kipato cha uchongaji vinyago.
“Akili yangu inanituma niende kijijini nikalime, hii kazi niwaachie vijana, kwa kuwa pia mpaka sasa nimefanikiwa kuwafundisha vijana saba na wanaendelea na kazi hii,” anasema.
Ni takriban miaka 50 sasa Sivandeka anajishughulisha na uchongaji na uuzaji vinyago, lakini hajapata kushiriki katika maonesho ya biashara hapa nchini wala nje ya Tanzania.
“Sijawahi kuhudhuria maonesho yoyote ya biashara ndani na nje ya Tanzania, wanaokwenda ni wenye uwezo, na wengi wao si wachongaji. Sisi mafundi hatuna uwezo huo,” anasisitiza.
Sivandeka na wenzake katika kituo hiki wangependa kuona Serikali inakuwa karibu nao, kwa kuwatafutia masoko ya uhakika na kuwakopesha fedha za mitaji wajikwamue kiuchumi na kuboresha maisha yao na familia zao.
Anatumia nafasi hii pia kuieleza jamii kwamba wachongaji wanaweza kujikwamua kiuchumi, ikiwa watu watajenga mazoea ya kununua bidhaa za uchongaji kutoka kwa wachongaji husika kuliko kwa wachuuzi.
Huku JAMHURI ikiendelea kusuuza moyo kutokana na mandhari nzuri ya eneo hili la MCC, inafika kibanda namba 18. Hapa inakutana na Stela Mdetele na Upendo Maziku, wauzaji wa vinyago na kazi nyingine za mikono ikiwamo michoro ya picha za vitu mbalimbali.
“Karibu kaka, karibu sana.” Ndivyo nilivyopokewa na wanawake hawa, pengine wakidhani wamepata mteja wa kununua kinyago dukani. Wachuuzi hawa wanasema wateja wanaojitokeza zaidi kipindi hiki ni Wachina. Hapa tunaendelea na mazungumzo.
JAMHURI: Lakini Wachina wengi hawajui Kiswahili na hata Kiingereza hawakiwezi sana. Ninyi mnawezaje kuwasiliana nao kibiashara?
Stela: Ni kweli, lakini mara nyingi tunatumia calculator (kikokotoo) kuwasiliana nao kuhusu bei ya bidhaa wanayohitaji. Unamwandikia bei ya kuanzia naye anakuandikia kiasi alichonacho, mwishowe tunakubaliana.
JAMHURI: Huwa hakuna usumbufu unaojitokeza kati yenu na Wazungu, na au tuseme hao Wachina katika kununua na kuuziana bidhaa hizi?
Stela: Mchina lazima umwanzie bei ya juu sana, maana wana mazoea ya kushusha sana bei. Unaweza kumwambia shilingi milioni moja akakwambia akupe laki nne; na unaweza kumwambia laki nne akakwambia ana elfu hamsini.
JAMHURI: Hizi bidhaa huwa mnazitoa wapi kuzileta hapa dukani?
Upendo: Tunazinunua huko mashambani [vijijini] kwa mafundi [wachongaji] zikiwa hazijakamilika, tunakuja kuwakodi mafundi walioko huku kwa ajili ya kuzikamilisha.
JAMHURI: Kuna maelezo kwamba wateja wakuu wa vinyago ni Wazungu, hivi Waafrika wao kweli hawapendi vinyago?
Stela: Ndiyo, Waafrika wao sana sana wanapendelea vitu vidogovidogo kama vile picha za Wamaasai, opener (kifungua) na mishumaa. Pengine hii ni kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi.
JAMHURI: Mkiulizwa kinachowakwaza katika biashara hii mtataja nini?
Upendo: Hata hili la baadhi ya wateja kubeza ubora wa bidhaa zetu ni kikwazo. Yaani wateja mpaka uwabembeleze sana. Lakini pia kiwango cha mauzo kimeshuka sana.
JAMHURI: Mngependa Serikali iwafanyie nini hasa muweze kunufaika na biashara hii?
Stela: Kikubwa zaidi Serikali ingetutangazia biashara zetu ndani na nje ya nchi. Pia ielekeze kuwa bidhaa za uchongaji na uchoraji ziuzwe eneo moja zisizagae kila sehemu.
JAMHURI: Kutenga eneo moja la kuendeshea shughuli hizi za sanaa kutakuwa na manufaa gani kwenu?
Stela: Mafanikio makubwa yatakuwa kuwaleta wateja pamoja, na hiyo itaboresha mauzo ya bidhaa hizi na kutuinua kiuchumi.
Focus Senya ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) tangu mwaka 2003. Anasema chama hicho ndicho mdhamini wa MCC.
“Serikali ilituondoa kandokando ya barabara za Bagamoyo na Oysterbay ikatuhamishia hapa Mwenge kwa umiliki rasmi mwaka 1983. Wakati huo idadi yetu ilikuwa chini ya 100 lakini kwa sasa ujumla wetu ni zaidi ya 400,” anasema Senya.
Anatambua kuwa uchongaji ni sanaa muhimu katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania, na kwamba bila wachongaji utamaduni wa taifa letu utatoweka.
Wamakonde na Wazaramo wanatajwa na wengi kuwa ndio waasisi wa sanaa ya uchongaji, lakini karibu makabila yote zaidi ya 120 hapa nchini siku hizi yana watu wenye vipaji vya kuchonga vinyago.
Mwenyekiti huyu naye anaamini kwamba kuyumba kwa soko la bidhaa za uchongaji kunachangiwa na Serikali kutoipa kipaumbele sanaa hii.
“Viongozi wa Serikali yetu hawajajua kwamba hata kitendo cha kuziweka bidhaa za uchongaji katika ofisi zao tayari ni soko, kwa sababu zitajitangaza kwa wageni na kuonesha tunathamini bidhaa zetu kuliko zinazotoka nje ya nchi yetu.
“Siku hizi ukiona Waafrika, hasa viongozi wanakuja kununua vinyago hapa, unakuta anakwenda kuwazawadia wageni kutoka nje ya nchi. Huu ni urithi wa mawazo potofu.
“Binafsi sioni sababu ya Watanzania kukazania kununua bidhaa za uchongaji kutoka nje ya nchi wakati tumejaaliwa miti mingi na wachongaji wazuri,” anasema Senya katika mazungumzo na JAMHURI ofisini kwake kwenye kibanda namba 30.
Katika jitihada za kukabili tatizo la uelewa mdogo wa Kiingereza miongoni mwa wachongaji na wauza vinyago hapa MCC, CHAWASAWATA imeanzisha darasa la jioni kufundisha lugha hiyo.
“Tumeanza na Kiingereza ili kitusaidie kuwasiliana vizuri na wateja wetu [Wazungu], baadaye tutaongeza somo la Kichina maana hata sasa soko linalotuweka hai ni la Wachina,” anaongeza.
Hata hivyo, anasema dosari ya Wachina ni pale wanaponunua bidhaa za uchongaji katika kituo hiki na kwenda kuziigiza kwa kuzitengeneza kwenye viwanda vyao.
“Hata hapa hapa Dar es Salaam, ukienda eneo la Kariakoo utakuta Wachina wanatengeneza na kuuza shanga na bidhaa nyingine zinazofanana na tunazochonga,” anasema Senya.
Kwa upande mwingine, kiongozi huyu wa CHAWASAWATA anataja changamoto inayoinyima ofisi yake usingizi kuwa ni kuboresha uwezo wa wachongaji.
“Wasanii wengi hapa mpangilio wa shughuli zao si mzuri sana. Wengi wao wanatumia mfumo wa kizamani kuchonga, jambo linalowafanya wasinufaike vizuri na shughuli hizi.
“Kwa sasa ninajaribu kuchukua mafundi 20 wafundishwe kuchonga, kuchora na kufinyanga vizuri kwa kipindi cha miezi mitatu ili nao waweze kuwa walimu wa wengine,” anasema.
Senya anatoa wito kwa viongozi wa Serikali kutambua kuwa ofisi zao nazo ni sehemu ya soko la kutangaza bidhaa za uchongaji, na hivyo, kuwezesha wasanii husika kupiga hatua ya maendeleo.
“Kitu kingine, kama kweli Serikali inataka kuona sanaa ya uchongaji inasonga mbele, iweke mkakati wa kusaidia kumotisha wasanii husika ili nao wasaidie kuweka hai utamaduni wa taifa letu,” anaongeza Mwenyekiti huyu.
Anaikumbusha jamii ya Watanzania na Waafrika kwa jumla kuchangamkia bidhaa za uchongaji badala ya kuendelea kuamini kimakosa kuwa bidhaa hizo ni kwa ajili ya mapambo kwenye ofisi na nyumba za Wazungu pekee.
Kassim Othman ni mkazi wa Kunduchi, Dar es Salaam. Ni miongoni mwa wazawa wachache waliokutwa na JAMHURI wakinunua bidhaa za uchongaji katika kituo hiki.
Huku akiwa amebeba kinyago cha twiga mdogo alichonunua kwa ajili ya mapambo nyumbani kwake, Othman anasema Watanzania wengi hawana elimu kuhusu umuhimu na matumizi ya bidhaa za uchongaji, ndiyo maana hawazichangamkii.
“Watu wengi miongoni mwetu hawajui maana ya vinyago, hawajui umuhimu wa vitu vya aina hii katika mapambo ya nyumbani. Lakini inawezekana hata uchumi duni kwa wengi wetu ni kikwazo cha kununua mapambo haya,” anasema Othman.
Naye raia wa China aliyejitambulisha kwa jina la Bowen Qiang, amekutana na JAMHURI akinunua vinyango vya wanyama wadogo katika eneo hili la MCC.
“Ninaishi hapa Dar es Salaam kikazi, nimekuwa nikifika hapa mara kwa mara kununua bidhaa mbalimbali vikiwamo vinyago vya wanyama. Pia nimekuwa nikiwasindikiza wenzangu kuja kununua mapambo ya nyumbani hapa, na kwa kweli tunavutiwa na bidhaa zinazochongwa na wasanii hawa,” anasema Qiang.
Kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana kwenye tovuti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (HYPERLINK “http://www.tanzania.go.tz”www.tanzania.go.tz), majukumu ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni pamoja na kuandaa mipango ya kukuza na kuboresha fani mbalimbali za utamaduni, hususan sanaa za ufundi wa mikono (ukiwamo uchongaji), kama kielelezo cha utaifa na chanzo cha ajira kwa wananchi.
Hata hivyo, wachongaji wa vinyago katika kituo hiki cha MCC wanaeleza kuwa hawajaguswa na majukumu hayo yanayotajwa na wizara hiyo.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla, anakiri kuwa bado wizara hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwawezesha wasanii wachongaji hapa nchini.
“Ni kweli malalamiko ya wachongaji ni changamoto kubwa kwetu [wizara], lakini niahidi kuwa tutashirikiana na Mkurugenzi wa Utamaduni kuiandalia mkakati wa kuboresha shughuli zao na kuinua kipato chao,” anasema Makalla katika mahojiano na JAMHURI.