DAR ES SALAAM
NA MICHAEL SARUNGI
Katika jambo la upigaji kura kutoka kwa mashabiki wote duniani lililofanywa na mtandao wa
soka wa Sokaa Africa, Wayne Rooney aliibuka mshindi katika nafasi ya kwanza akiwa na kura
60 huku akifuatiwa na Ronaldinho aliyepata kura 38.
1. Wayne Rooney
Mchezaji huyu anaweza asiwe amefanikiwa kuchukua tuzo ya mwanasoka bora duniani, lakini
anahesabika na mashabiki kuwa mmoja wa wachezaji bora wa muda wote aliyevaa jezi namba
kumi mgongoni kwake.
Rooney amechukua makombe yote yanayotakiwa kuchukuliwa katika ngazi ya klabu na
anahitaji heshima kubwa na kutambulika kama mmoja wa wachezaji wakubwa katika historia ya
soka duniani.
Pia mchezaji huyu amebakiza idadi ya mabao 5 tu kuvunja rekodi ya mabao mengi kuwahi
kufungwa katika klabu ambayo inashikiliwa na Sir Bobby Charlton ambaye ni miongoni mwa
magwiji wa soka nchini Uingereza.
2. Ronaldinho
Huyu ni kiungo wa zamani wa FC Barcelona anayechukuliwa kama mmoja wa wachezaji bora
wa muda wote, aliyevaa jezi namba 10 mgongoni, huku akijipatia mafanikio mengi kuanzia
ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.
Pia Ronaldinho wakati wa uchezaji wake amefanikiwa kushinda Kombe la Dunia mwaka 2002
akiwa pamoja na Ronaldo De Lima baada ya kuichapa Ujerumani 2-0, na tangu kipindi hicho
Brazil haijawahi kushinda kombe hilo.
Amefanikiwa pia kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwaka 2004 na 2005, aliweza
kuwateka mashabiki wengi duniani kwa pasi zake za kutoa mipira ya kufa, chenga za maudhi,
ukokotaji maridhawa wa mpira pamoja na tabasamu lake uwanjani.
3. Lionel Messi
Huyu ni mchezaji bora duniani mara 5 ndani ya kipindi cha miaka 10. Ameisaidia klabu ya
Barcelona kuchukua makombe 4 ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya pamoja na Kombe la Laliga
na katika kipindi hicho na kuifanya Barcelona kutawala soka la Ulaya.
Ni katika kipindi hiki ambacho Barcelona imekuwa imara katika namna ambayo haikuwahi
kuonekana miaka mingi, lakini Messi hajashinda taji lolote lile na timu yake ya taifa ya
Argentina.
4. Zinedine Zidane
Kwa ambaye sasa huyu ndiye Meneja wa Klabu yenye mafanikio makubwa duniani ya Real
Madrid, bado anakubalika na mashabiki walio wengi duniani kuwa ni mmoja wa wachezaji
waliobarikiwa kuwa na kipaji cha kipekee duniani.
Gwiji huyu katika soka, amefanikiwa kushinda tuzo ya mwanasoka bora duniani akiwa na klabu
za Real Madrid na Juventus ya Italia, pia ameshinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya.
5. Luis Figo
Luis Figo ni mmoja wa wachezaji wachache waliofanikiwa kuiwakilisha Barcelona pamoja na
Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, kwa mafanikio makubwa enzi za uchezaji wake.
Aliweka rekodi ya kupika nafasi 106 za mabao ambazo ni Lionel Messi pekee ndiye
aliyefanikiwa kuivunja.
Alifahamika kwa ujuzi wake wa kucheza mpira na kuwatesa mabeki kwa kufunga mabao
mazuri. Ameweka rekodi ya kuichezea timu ya Taifa ya Ureno michezo 127.
6. Del Piero
Alikuwa miongoni mwa washambuliaji bora katika historia ya soka nchini Italia, anachukuliwa
kama mmoja wa mastraika waliobarikiwa kiufundi katika kizazi chake. Del Piero pia alikuwa ni
fundi wa mipira iliyokufa.
Pia ameshinda makombe yote aliyotakiwa kushinda katika ngazi ya klabu na pia alifanikiwa
kushinda Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya Taifa ya Italia mwaka 2006. Na haya ndiyo
mafanikio yake.
Mwisho…