NA MICHAEL SARUNGI
Wachezaji wa ndani wanatakiwa kupambana na kuwa tayari kukabiliana na ongezeko la wachezaji wa kigeni wanaotarajiwa kuanzia msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania bara.
Wakizungumza na JAMHURI siku chache baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) kupitia Rais wake, Walles Karia, kutangaza kanuni mpya ya usajili wa wachezaji wa kigeni kwa timu za ligi kuu (VPL) kwa msimu ujao kuongezeka kutoka saba hadi kumi, wadau hao wamesema umakini mkubwa unatakiwa baada ya mfumo huo kuanza.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema pamoja na nia nzuri ya (TFF) ya kukuza soka na kuleta ushindani ndani ya vilabu na kufanya vyema katika michuano ya kimataifa lakini pia wanapaswa kuwaongezea thamani wachezaji wa ndani.
Amesema vilabu vinapaswa kuwa makini kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa kuliko kuwa na wachezaji wenye viwango sawa na wazawa huku wakilipwa mamilioni ya fedha kwa kazi inayoweza kufanya wachezaji wa ndani.
Kuna hatari ya nchi kupotea katika michuano ya kimataifa endapo juhudi za dhati hazitachukuliwa kwa wachezaji wazawa kupata nafasi ndani ya vilabu wanakocheza na kujikuta wakikaa benchi na kuwashuhudia wageni wakicheza.
Mfano uwepo wa wachezaji wa kigeni wengi katika ligi kuu ya Uingereza kwa kiasi fulani kumechangia timu ya Taifa ya nchi hiyo kushindwa kufanya vyema katika michuano ya kimataifa kabla ya kuibuka na kufikia hatua ya nusu fainali katika michuano ya kombe la dunia iliyomalizika nchini Urusi.
Amesema TFF wanapaswa kuwa makini na ongezeko hili kwa manufaa ya soka la hapa nchini vinginevyo inaweza ikajikuta ikilichimbia kaburi soka la Tanzania na kuhitaji miaka mingi kuja kulifukua na kuanza kutafuta mafanikio.
Aliyewahi kuwa kocha wa Mbao FC Mrundi, Etiene Ndayiragije amesema ongezeko hilo linaweza kuwa na faida kwa wachezaji wazawa wa ndani kwa kuwafanya wainue vichwa juu na kuanza kupambana badala ya kubweteka.
Ujio wa wachezaji wengi wa kigeni unaweza pia kuvisaidia vilabu kufanya vyema katika michuano mbalimbali ya kimataifa kwa vilabu vitakavyopata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika michuano mbalimbali ya kimataifa barani afrika na kuongeza ushindani wa ndani.
Kinachotakiwa ni TFF kuweka sheria itakayotoa mwanya kwa wachezaji wa ndani kupewa nafasi lakini hicho kisiwe kigezo cha kubweteka na kuwaacha wageni wakiendelea kulitawala soka la hapa nchini hiyo inaweza kuwa hatari kwao na kwa timu ya taifa.
Bila wachezaji wa ndani kupata changamoto kutoka nje wanaweza kuendelea na kubweteka na kujikuta vipaji vyao vikipotea mapema kabla hata ya wakati hali ambayo inaweza kuviadhiri vilabu na timu ya taifa ya nchi.
Winga wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania Edibily Lunyamila amesema kwa wawaida hakuna jambo lisilokuwa na faida na hasara, kikubwa kinachotakiwa ni wachezaji wenyewe kuwa tayari kupambana na hali yoyote.
Wachezaji wakiwa tayari wa kupambana katika hali yoyote hawawezi kuwa na hofu ya ujio wa mchezaji yoyote ndani ya klabu kikubwa kwao ni kujengewa uwezo wa kujianini na kuwa tayari kwa vita ya namba na wageni hao.