Tangu ilipofuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Nigeria mwaka 1980, ikatolewa mapema ikiwa kundi moja na wenyeji, Misri na Ivory Coast, timu ya soka ya taifa ya Tanzania hadi sasa haijaweza kuifikia tena hatua hiyo na hakuna matumaini yoyote kama itafanya hivyo tena.

Imebaki kuwa inaondolewa mwanzoni tu mwa michuano yote ya kimataifa. Inatolewa kutokana na soka lake kuzidi kudidimia huku mataifa yaliyokuwa dhaifu kama Botswana,  Angola au Libya yakifika mbali kama ilivyokuwa mwaka huu huko Equatorial Guinea na Gabon.

 

Zote hizo zilikuwa miongoni mwa nchi zilizocheza fainali ya Michuano ya Kombe la Afrika (AFCON 2012) wakati Timu ya Taifa ya Zambia ilipotawazwa kuwa mabingwa wapya.

 

Kushindwa kwa Tanzania kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya soka ya kimataifa, kwa namna moja ama nyingine, kunafanana na hali iliyonayo England hata kama imekuwa ikipiga hatua chache mbele.

 

Tangu iliposhinda Kombe la Dunia wakati fainali zake zilipofanyika nchini humo mwaka 1966, England imekuwa ikishindwa kufika hata nusu fainali ya michuano yoyote ya kimataifa inayoshiriki. Siku zote imekuwa ikiishia hatua ya makundi au robo fainali kama ilivyofanya katika fainali za Kombe la Ulaya zilizoandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine mwaka huu.

 

Kutofanya kwake vizuri kisoka kunachangiwa zaidi na Ligi Kuu za nchi hizi kusheheni na kutegemea zaidi wanasoka wa kigeni, mbali na sababu nyingine kama zipo.

 

Katika miaka ya karibuni, Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara imekumbwa na wimbi kubwa la wachezaji kutoka nje ya nchi. Hao ndiyo wanaotegemewa zaidi na timu zote kubwa za Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club, na Dar es Salaam Young Africans (Yanga).   Wachezaji hao wa kigeni ndiyo waliotamba kwa kufunga mabao mengi zaidi msimu uliopita huku wenyeji wakishindana nyuma yao.

 

Kati ya wachezaji 17 waliotikisa nyavu kuanzia mara sita hadi 18, wachezaji wa kigeni walikuwa wanane huku wenyeji wakiwa tisa. Wachezaji hao na mabao yao kwenye mabano ni John Boko (18), Emmanuel Okwi (12), Khamis Kiiza, Nsa Job na Patrick Mafisango (sasa ni marehemu) (11), Kenneth Asamoah (10), Said Bahanuzi (8) na Felix Sunzu aliyefunga mara saba.

 

Wengine ni Mrisho Ngassa, Davies Mwape, Kipre Tcheche, Gaudence Mwaikimba, Hussein Javu, Saidi Dilunga, Enyinna Darlington, Juma Semsue na Mohammed Kijuso waliofunga mabao sita kila mmoja.

 

Wageni katika orodha hiyo ni Emmanuel Okwi, Khamis Kiiza na Enyinna Darlington (Uganda), Kenneth Asamoah (Ghana), Felix Sunzu na Davies Mwape (Zambia), Kipre Tcheche (Jamhuri ya Afrika ya Kati) huku Patrick Mafisango raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia na Kongo.

 

Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Ligi Kuu ya England wakati kati ya wachezaji 21 waliofunga kuanzia mabao 10 hadi 30, wanane peke yake ndiyo Waingereza huku 13 wakitoka nje ya nchi hiyo. Wachezaji hao wa kigeni na mabao yao kwenye mabano ni Robin Van Persie (30), Sergio Aguero (22), Emmanuel Adebayor, Yakubu Aiyegbeni na Demba Ba (16), Grant Holt (15), Mario Balotelli, Papiss Demba Cisse na Edin Dzeko (13), Rafael Van der Vaart na Luis Suarez (11) huku Peter Odemwingie na Javier Hernandez wakiwapeleka makipa marikiti mara 10 kila mmoja.

 

Wachezaji raia wa England waliokuwa katika orodha hiyo ni Wayne Rooney (27), Clint Dempsey (17), Danny Graham, Steven Fletcher, Daniel Sturrige na Frank Lampard (11), Peter Crouch na Jermain Defoe waliofunga msimu wa ligi hiyo na mabao 10.

 

Hivyo ndivyo ambavyo Ligi Kuu Tanzania Bara na England zilivyotawaliwa na wanasoka wa kigeni. Hao ndiyo wanaotegemewa zaidi na timu zao kuzipa mataji kuliko raia wake. Leo kwa mfano Yanga iliyotamba kati ya mwaka 1981 na 1984 ikiwa na wachezaji wa ndani peke yake au ilivyokuwa Pan African wakati huo, kamwe hivi leo hazipo hivyo.

 

Mashabiki waliokuwapo enzi hizo wanaikumbuka Yanga iliyotisha ikiwa na akina Khamis Kinye, Joseph Fungo, Yussuf Ismail ‘Bana’, Fred Felix Minziro, Juma Shaaban, Ahmed Amasha, Athuman Juma ‘Chama’, Allan Shomari, ‘Jenerali’ Juma Mkambi, Shaaban Katwila, Charles Boniface Mkwasa, Makumbi Juma Baruwan, Abeid Mziba ‘Tekero’, Omar Hussein Sultan na Rashid Hanzuruni, Hija Salehe Hija, Juma Kampala na wengineo.

 

Wanakikumbuka pia kikosi mahiri cha Pan African kilichoundwa na kina Juma ‘Hazimo’ Pondamali, Ali Yussuf, Jaafar Abdulrahman, John Faya, Rashid Idd ‘Chama’, Jellah Mtagwa, Salum Mwinyimkuu ‘Carlos’, Doto Rutta Mokili, Gordian Mapango, Hussein Ngulungu, Abdallah Burhan, Mohammed Yahaya ‘Tostao’, Ali Katolila na Peter Tino na kadhalika.

 

Ilikuwapo Simba madhubuti ya kina Idd Pazi ‘Father’, Mussa Kihwelo, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Rahim Lumelezi, Lila Shomari, Abdallah Mwinyimkuu, George Lucas, Mtemi Ramadhan, Innocent Haule, Zamoyoni Mogella, Malota Soma ‘Ball Juggler’ na wachezaji wengine.

 

Tofauti na enzi hizo wakati vikosi vyote vya Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) vikiwa havina mchezaji yeyote wa kigeni huku kandanda likiwa matawi ya juu, hali hivi leo ni tofauti.

Mashabiki wa Simba, kwa mfano, msimu uliopita wasingeweza kukubali timu yao icheze bila Emmanuel Okwi au Patrick Mafisango, kama ambavyo Yanga nao wasingeweza kuambiwa chochote kama akina Yaw Berko, Haruna Niyonzima au Khamis Kiiza hawamo uwanjani huku wakiwa bukheri wa afya wala hawana kadi nyekundu. Huu ndiyo ugonjwa unaolitesa soka la Tanazania.

 

Tumefikia pale zilipo timu za England ambazo hata iweje katika hali ya kawaida, mashabiki wa Arsenal kamwe wasingemwelewa kocha Arsene Wenger kama angemwacha nje Robin Van Persie msimu uliopita.

 

Ndivyo pia ingekuwa kwa Roberto Mancini kama Manchester City dimbani bila Sergio Aguero, Mario Balotelli wala Edin Dzeko au Manchester United isiyokuwa na Javier Hernandez, Liverpool ya bila Luis Suarez, Newcastle United inayocheza bila Papiss Demba Cisse, Demba Ba ama kikosi cha Blackburn Rovers kisichokuwa na Yakubu Aiyegbeni.

 

Tofauti na Serie A ya Italia au La Liga ya Hispania, timu zake haziwategemei kwa kiwango kikubwa wachezaji wa kigeni. Hata Barcelona na Real Madrid zenye wanasoka mahiri zaidi duniani kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, bado zimejaza wachezaji wa ndani.

 

Hao ndiyo hata wenyewe wanawatengenezea uwanjani. Ndiyo maana wanapochezea timu zao za taifa za Argentina ama Ureno hawaonyeshi makali wanayotamba nayo La Liga.

 

Kama anavyosema beki wa zamani wa kimataifa wa Yanga, ambaye sasa ni kocha msaidizi wa timu ya Seeb FC ya Oman, Ahmed Amasha, soka la Tanzania litazidi kuporomoka kama haitawekeza ama kukuza vipaji vya ndani, badala yake ikaendelea kuwategemea wachezaji wa kigeni.

 

“Nasikia kuna Mganda Emmanuel Okwi pale Simba, halafu Yanga nao wana Khamis Kiiza anayetoka pia Uganda. Kwa nini timu zetu zimeacha kulea wachezaji yosso?” Alihoji beki huyo mahiri wa kushoto, alipokuwa akizungumza na moja ya vyombo vya habari nchini.

 

Huo ndiyo ugonjwa unaoliangamiza soka la Tanzania na England, na kuzifanya timu zake za taifa – hata kama ni kwa viwango tofauti – kushindwa kuwa lolote wala chochote kimataifa.