Leo Taifa Stars itakuwa Stade Mustapha Ben Jannet uliopo mjini Monastir, Tunisia, kuivaa Libya katika mchezo wa kufuzu kuwania kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Huu ni mchezo wa pili, katika mchezo wa awali dhidi ya Equatorial Guinea uliopigwa mwishoni mwa wiki, Stars iliondoka na ushindi wa mabao 2-1.
Haukuwa ushindi mwepesi, kwani hadi mapumziko tayari Equatorial Guinea walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa Sassuolo ya Italia, Pedro Mba Obiang, katika dakika ya 16 akimtungua kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja kwa shuti la mbali.
Tuje sasa
Kinachoendelea katika Jiji la New York au Moscow ndani ya dakika hii, kinaweza kujulikana duniani kote ndani ya saa moja. Teknolojia imerahisisha sana maisha na katika sehemu nyingine za ulimwengu huu, watu wengi wanajikuta wakikosa ajira kwa sababu kazi zao zinaweza kufanywa na mitambo ya kisasa.
Makocha Etienne Ndayiragije na Selemani Matola wanaisimamia timu ya taifa kwa sasa. Siku zote ugenini ni tofauti na nyumbani, yako mengi ambayo yatakuwa ni mageni kwa wanasoka wetu.
Lazima watajikuta wakilazimika kutumia simu zao za kisasa kwa ajili ya kuchukua kumbukumbu nyingi kuhusiana na Libya. Hakuna binadamu asiyependa kuona kitu kipya maishani, awe ni kijana wa miaka 20 awe ni mzee wa miaka 85, ulimwengu umejaa maajabu yanayovutia kwa ajili ya kuyapiga picha.
Ningependa kuwakumbusha wachezaji wa Taifa Stars kuwa wanapaswa kuvuja jasho jingi uwanjani kama wanataka kuwa sehemu ya maisha kumbukizi. Wanakwenda kuivaa Libya ndani ya Tunisia, lakini wanapaswa watambue nini Watanzania wanataka.
Waondokane na hali ya wao kuonekana abiria wa kawaida tu anayekatiza katika maeneo ya viwanja vya ndege, wageuke kuwa abiria anayeombwa kupigwa picha na watu wa mataifa mbalimbali. Yaya Toure akikatiza katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Istanbul atakimbiliwa na wanafunzi wa shule za msingi, vijana wa vyuo vikuu na watu baki.
Hali hiyo ni tofauti na ambavyo watu hao wanavyomchukulia mchezaji kama Kelvin Yondani au Simon Msuva. Heshima aliyonayo mchezaji wa kiwango cha Yaya Toure haikupatikana kirahisi, alitoka jasho huku akivumilia mambo mengi ambayo kwao Ivory Coast hayapo.
Mchezaji wa Taifa Stars asiufurahie ushindi dhidi ya Equatorial Guinea, autafute ukaaji wa miaka mingi kwenye nchi ambazo zina mazingira ya soka ambayo ni rafiki kwa mwanasoka.
Mchezaji ambaye baada ya wiki moja ya mazoezi ya Taifa Stars anashindwa kuvifikia viwango vya wanasoka wa nchi aliyokwenda kwa ajili ya kambi hiyo, ni mtalii hata kama hapendi kuisikia kauli hiyo.
Wachezaji wa Libya watakaopambana na hawa wa kwetu, wengine wanacheza soka barani Ulaya, wengine wako huko huko Tunisia. Watakuja kucheza mechi dhidi ya Taifa Stars halafu watapanda ndege kurudi kwenye timu zao.
Hawa wa kwetu wanaweza kujikuta wakienda tena Tunisia kwa ajili ya kambi ya Yanga, Simba au Azam FC, watapiga picha za ukumbusho, ambazo zitakuwa sehemu ya mbwembwe za kuwakoga marafiki zao baada ya kustaafu soka.
TFF inapotumia nguvu nyingi kwa ajili ya Stars lengo ni kutafuta ushindi wa taifa na wakati huo huo lengo jingine ni kumfumbua macho mchezaji ambaye pengine ameridhika na kile akipatacho kupitia ligi yetu. Nikiitazama Taifa Stars nauona mchanganyiko mzuri wa damu changa na wakongwe.
Sitazipenda habari zozote ambazo zinahusiana na wachezaji vijana wa Taifa Stars kuwa na mawazo ya kuzeekea kwenye ligi yetu, pamoja na kucheza mechi nyingi za Kombe la Kagame na zile za Challenge.
Ukikitazama kikosi cha Libya, baada ya kila jina la mchezaji mbele yake kwenye mabano kuna jina la timu anayoichezea ambayo ni ya nje. Sina uhakika iwapo wachezaji wa Taifa Stars wanao wivu wa kufanana na wenzao wanaocheza nao na kupanda ndege kuelekea kwenye ligi kuu bora zaidi.
Hali imekuwa hivyo kwa miaka mingi na itaendelea kuwa hivyo. Mapinduzi yanahitajika kwenye soka letu, hasa yale yanayohusiana na shauku ya kutaka kufika mbali.
Wachezaji wanayo hamu ya kuwa sehemu ya timu kubwa ambazo zinamtunza mchezaji kiasi ambacho akili yake inazama kwenye soka na si katika mambo mengine. Teknolojia inazidi kukua kila kukicha, ninatumaini kamera za simu za wachezaji wa Taifa Stars ni za kiwango cha kisasa, hivyo kumbukumbu za Tunisia zitatunzwa kwa miaka mingi ijayo.
Lakini wachezaji hao hao watambue kuwa wanapaswa wakuze viwango vyao ili yaweze kuwa ndiyo maisha yao ya kila siku ya soka mpaka watakapofikisha umri wa kuamua kustaafu soka.
Makocha wanasemaje?
Etienne Ndayiragije analibainisha hili wazi, pamoja na kusaka ushindi lakini anataka aone wachezaji wakitoka na kucheza nje ya Tanzania.
“Kuna vitu vingi ambavyo mchezaji anarudi navyo akicheza nje. Mtazame Mbwana Samatta au Simon Msuva, wana vitu vya ziada, hivyo wachezaji wapambane na kuacha kufikiria ndani tu.”
Selemani Matola anakiri uoga nao ni tatizo, lakini anaamini kwa dunia ya sasa kuna kitu kipya kinakuja ndani ya nchi.
“Wachezaji kwa sasa wana wivu, wakitazama wenzao ambao wamefanikiwa wanapambana na waendelee hivyo ili kuboresha soka letu.”