Kinachoendelea katika Jiji la New York au Moscow ndani ya dakika hii, kinaweza kujulikana duniani kote ndani ya saa moja. Teknolojia imerahisisha sana maisha na katika sehemu nyingine za ulimwengu huu, watu wengi wanajikuta wakikosa ajira kwa sababu kazi zao zinaweza kufanywa na mitambo ya kisasa.
Tuje sasa! Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, amemuongeza mshambuliaji Ditram Nchimbi anayechezea Polisi Tanzania ya Kilimanjaro kwa mkopo kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.
Ndayiragije amefanya uamuzi huo siku moja tu baada ya Nchimbi kufunga mabao matatu katika sare ya ugenini ya 3-3 dhidi ya wenyeji, Yanga, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Nchimbi anaungana na wachezaji wengine 28 ambao Ndayiragije aliwaita wiki ikiyopita kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji, Rwanda mjini Kigali Oktoba 14 kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) dhidi ya Sudan Oktoba 18.
Mechi ya kwanza Taifa Stars ilifungwa 1-0 nyumbani Dar es Salaam na inatakiwa kwenda kushinda 2-0 ugenini ili kukata tiketi ya kucheza fainali za michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee.
Wanasemaje?
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, yeye anaitazama zaidi Stars kwa kutaka ifanye mambo makubwa zaidi katika kuleta ushindani halisi wa soka.
“Tanzania kuna vipaji, wapo wachezaji wazuri na wenye uwezo, lakini wale wanaoitwa huko watambue wana deni kubwa kuliko wakati wowote ule.
“Kuipigania jezi ya taifa ni heshima kubwa, kwangu Tanzania ikipata mafanikio ni raha, naitakia kila la heri, ila lazima wachezaji watambue kwa nini wapo pale,” amesema Zahera.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems, naye hakuwa mbali na Zahera kwa kuwataka wachezaji wapambane kuhakikisha wanaipa mafanikio nchi.
“Wapambane, wajue nini ambacho taifa linataka kutoka kwao, kufanikiwa kwa Tanzania ni kufanikiwa kwa Simba pia, wapigane kufa na kupona ili kuhakikisha wanasonga mbele.
“Kuna kikosi bora ambacho nina uhakika kitaleta matokeo mazuri yenye kumfurahisha kila mtu,” amesema.
Mbwana Samatta, naye amekitakia heri kikosi hicho, huku akisema ana imani kubwa kitafanya kweli katika mchezo dhidi ya Sudan.
“Nawatakia kila la heri, naamini watafanya kweli katika mchezo huo,” amesema.
Mtazamo
Ila ningependa kuwakumbusha wachezaji wa Taifa Stars, watoke jasho jingi uwanjani kwa ajili ya kuipigania timu yao.
Waondokane na hali ya wao kuonekana abiria wa kawaida tu, anayekatiza katika maeneo ya viwanja vya ndege, wageuke kuwa abiria anayeombwa kupigwa picha na watu wa mataifa mbalimbali.
Yaya Toure akikatiza katika maeneo ya uwanja wa ndege wa Istanbul atakimbiliwa na wanafunzi wa shule za msingi, vijana wa vyuo vikuu na watu baki.
Hali hiyo ni tofauti na ambavyo watu hao wanavyomchukulia mchezaji kama Nchimbi, Juma Kaseja au Shomari Kapombe. Heshima aliyonayo mchezaji wa kiwango cha Yaya Toure haikupatikana kirahisi, alitoka jasho huku akivumilia mambo mengi ambayo kwao Ivory Coast hayapo.
TFF inapotumia nguvu nyingi kwa ajili ya kuweka kambi ya Taifa Stars huku ikitafuta mechi za kirafiki, lengo ni kutafuta ushindi wa taifa na wakati huo huo lengo jingine ni kumfumbua macho mchezaji ambaye pengine ameridhika na kile akipatacho kupitia ligi kuu yetu. Nikiitazama Taifa Stars nauona mchanganyiko mzuri wa damu changa na wakongwe.
Sitafurahi ikiwa ndani ya mipango yao hakuna nia ya kucheza soka kwenye ligi kuu zenye hadhi.
Sitazipenda habari zozote ambazo zinahusiana na wachezaji vijana wa Taifa Stars kuwa na mawazo ya kuzeekea kwenye ligi kuu yetu, pamoja na kucheza mechi nyingi za Kombe la Kagame na zile za Chalenji.
Ukikitazama kikosi cha Nigeria, baada ya kila jina la mchezaji mbele yake kwenye mabano kuna jina la timu anayoichezea ambayo ni ya ligi kuu moja barani Ulaya. Sina uhakika iwapo wachezaji wa Taifa Stars wanao wivu wa kufanana na wenzao, wanaocheza nao na kupanda ndege kuelekea kwenye ligi kuu bora zaidi.
Hali imekuwa hivyo kwa miaka mingi na itaendelea kuwa hivyo. Mapinduzi yanahitajika kwenye soka la bongo, hasa yale yanayohusiana na shauku ya kutaka kufika mbali. Hapa Tanzania ukiiondoa Azam FC, sidhani kama kuna klabu nyingine yenye ubora wa matunzo ya wanasoka.
Wachezaji wanayo hamu ya kuwa sehemu ya timu kubwa ambazo zinamtunza mchezaji kiasi ambacho akili yake inazama kwenye soka na si katika mambo mengine. Teknolojia inazidi kukua kila kukicha, natumaini kamera za simu za wachezaji wa Taifa Stars ni za kiwango cha kisasa, wana kumbukumbu nyingi.
Lakini wachezaji hao hao watambue wana deni, wakuze viwango vyao, soka iwe ndiyo maisha yao mpaka watakapofikisha umri wa kuamua kustaafu.