Na Isri Mohamed
Dakika 90 za mchezo wa kwanza kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Morocco kwenye michuano ya AFCON zimemalizika kwa matokeo ya kikatili kwa Stars kupoteza kwa mabao 3 kwa Nunge.
Mchezo huo umemalizika Stars wakiwa pungufu baada ya beki Novatus Dismas kupewa kadi nyekundu dakika ya 75, wakati wakiwa nyuma kwa bao moja lililofungwa na Romain Saiss dakika ya 30.
Mabao mengine ya mchezo huo yamefungwa na Azzadine Ounah dakika ya 77, na Yassin El Nessir dakika ya 80..
Baada ya mchezo kumalizika Nahodha wa Stars, Mbwana Ally Samatta amekiri Morocco walikuwa bora kutokana na aina ya wachezaji walionao, lakini bado ana Imani na timu yao wanaweza kufanya vizuri kwenye michezo miwili iliyobaki dhidi ya Zambia na Congo.
Aidha Simon Msuva ameongeza kuwa licha ya michuano kuwa migumu lakini bado wana nafasi kwani benchi la ufundi limeshaona wapi walipokosea na watafanya maboresho katika michezo ijayo.
Stars wanatarajia kushuka dimbani tena Jumapili ya Januari 21, 2024 dhidi ya timu ya taifa ya Zambia, majira ya saa 2 usiku.