Wananchi wanaojitolea kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, huenda wakakosa morali ya kuendelea kujitolea baada ya kubainika damu wanayochangia inamwagwa kwa kuharibika kutokana na ubovu wa mashine za kupimia sampo kabla ya kuidhinishwa kwa matumizi, JAMHURI limebaini.
Kituo pekee cha kupima ubora wa damu kabla ya kupelekwa kwa wagonjwa kipo Jijini Mwanza ambacho kinahudumia mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa damu hiyo ya sampo imekuwa ikichukua zaidi ya siku 28 bila kufanyiwa vipimo katika kituo hicho, kutokana na ubovu wa mashine kabla ya kusambazwa kwenye vituo vya afya kwa ajili ya matumizi.
Imeelezwa kuwa tatizo hilo limekuwa la muda mrefu na kama haitapatiwa ufumbuzi inaweza kusababisha wananchi wasiwe na ari ya kuchangia damu.
Mkazi wa Geita ambaye ni mmoja wachangia wazuri wa damu, Erasto Nzumbi, ameonya kuwa iwapo wachangiaji watabaini kuwa damu humwagwa kwa kuchelewa kwa majibu ya sampo, inaweza kuwavunja moyo wa kuendelea kuchangia.

“Sisi tunachangia damu tukiwa na matarajio ya kuwa inaenda kusaidia kuokoa maisha ya watu. Mimi huwa nachangia mara mbili kwa mwaka na nina kadi ya uchangiaji. Hapa Geita kuna hospitali kubwa, ni vizuri vipimo hivyo vingelifanyika hapa. Kumwaga damu kutavunja moyo wachangiaji,” amesema Nzumbi.
Inaeleza kuwa Ofisa Uhamasishaji wa damu salama Kanda ya Ziwa, Bernadicto Medaa, amekaa kimya pasipo kutoa ufafanuzi wa suala la vipimo vya sampo ya damu kucheleweshwa kutokana na ubovu wa mashine.
Medaa alipotafutwa aweze kujibu suala hilo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakutoa ushirikiano.
Kaimu Meneja wa Kituo cha Damu Salama Mwanza, Innocent Byabeza, amekanusha ubovu wa mashine za kupima sampo ya damu katika kituo hicho.
“Hakuna ubovu wa mashine za kupimia sampo ya damu. Hilo jambo ndiyo nalisikia kwako. Majibu ya sampo hayazidi siku tano na tunayatuma kwa njia ya mtandao,” amesema Byabeza.
Byabeza alisema suala la kumwagwa kwa damu kunaweza kutokana na sababu mbalimbali, mfano inapokusanywa damu ya kundi fulani na ikawepo ya kutosha ila wasitokee wagonjwa wa kundi hilo ni lazima itamwagwa baada ya muda wa matumizi kuisha ambao ni siku 35.

“Damu nyingine inamwagwa kutokana na kuonekana haifai baada ya vipimo kufanyika,” amesema Byabeza.
Naye Ofisa Masoko na Mahusiano ya Umma wa Kitengo cha Damu Salama Makao Makuu, Rayah Hamad, amekanusha kucheleweshwa kwa majibu ya sampo ya damu na kuzitupia lawama hospitali ambazo zina tabia ya kuchelewesha sampo hiyo.
“Hospitali zenyewe ndizo zinazochelewesha kupeleka sampo katika kituo cha kanda halafu wanatusingizia sisi.  mashine za reagents zipo za kutosha kwa sasa, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha majibu. Kipindi cha miaka mitatu iliyopita tulipokuwa na ufadhili kutoka Marekani, tulikuwa tukiikusanya sisi.
“Na tulikuwa tunazipima katika maabara zetu ili kuleta ufanisi zaidi. Tunatumia maabara sita ambazo ni Dar es Salaam, Mwanza, Tabora, Mtwara, Mbeya na Kilimanjaro ambapo tuna mchakato wa kuvipunguza viwe vituo viwili tu nchi nzima ili kudhibiti ubora wa damu,” amesema Rayah.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Leonard Subi, amesema kucheleweshwa kwa majibu ya sampo na damu kumwagwa hakujawahi kutokea.
Dkt. Subi anasema Mwanza kuna kituo cha damu salama cha Kanda kinachohudumia mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Kagera na Shinyanga na kwamba zipo  ‘reagents’ za kutosha za kuweza kufanya vipimo kwa miezi minne ijayo.

Anasema majibu ya vipimo huwa yanatumwa kwa njia ya mtandao kwa kutumia ‘barcode’ kwa aliyeleta sampo kazi inayofanyika kwa muda mfupi.
Mkuu wa Benki ya Damu Salama Mkoa wa Geita, Alfredina Fredrick, amekanusha kucheleweshwa kwa sampo hizo na damu kumwagwa.
“Damu haichelewi kwa makusudi. Ikichelewa kama wiki moja huwa ni kwa sababu wapimaji muda mwingine huishiwa ‘reagent’ lakini kama hawajaishiwa huwa hawacheleweshi. Na hilo ni tatizo ambalo lilikuwepo siku za nyuma,” anasema Fredrick.
Anasema hivi sasa vipimo vinafanyika kwa wakati kutokana na bohari ya taifa kuwa na mashine (reagents) za kutosha .
Amesema kuwa mahitaji ya damu kwa Mkoa wa Geita ni chupa 30 ambayo kwa sasa ipo ya kutosha.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Joseph Kisala, amesema hajawahi kusikia taarifa za kumwagwa kwa damu katika mkoa wake na kuhoji taarifa hizo zimetoka wapi.
“Mimi hilo sijawahi kulisikia. Ni wapi umepata taarifa hizo. Mimi ndiyo Mganga Mkuu, hilo jambo ndiyo nalisikia kwako,” amesema Kisala.
Naye Mganga Mkuu Mkoa wa Mara, Dkt. Francis Mwanisi, amekanusha mkoa wake kucheleweshewa majibu ya sampo inayotumwa katika kituo kilichopo jijini Mwanza.
“Sampo tunapeleka kwa wakati na majibu yanarudi kwa wakati. Hakuna damu inayomwagwa kwa kupitiliza muda wa matumizi labda kwa kama haifai kwa matumizi kutokana na vipimo vya kitaalamu,” amesema Mwanisi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Mei mwaka huu, mahitaji ya damu kwa Tanzania ni chupa 450,000.
WHO pia inaonesha kuwa asilimia nane ya vifo vya kinamama husababishwa na kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua na hivyo huhitaji damu kuweza kuokoa maisha yao.