Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia Dar es Salaam

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imeendelea kupokea sifa za utendaji mzuri wenye tija kwa taifa kutoka kwa kamati mbalimbali za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Taifa baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuridhishwa na taarifa ya fedha ya utekelezaji wa mradi wa Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam (DMGP).
Ziara hii ya PAC inakuja muda mfupi baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kutembelea bandari ya Dar es Salaam na kupongeza ufanisi uliopo bandarini hapo.

Akiongea wakati wa majumuisho ya ziara yao katika bandari hiyo ya Dar es Salaam na kupewa ripoti ya mradi wa DMGP, Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Nagy Kaboyoka amesema kuwa Kamati yake kwa kiasi kikubwa imeridhishwa na matumizi ya fedha za umma zilizowekezwa katika miradi hiyo ukiwemo wa DMGP baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Baada ya kupokea taarifa ya CAG tuliamua kuja (kama sehemu ya utendaji wetu kazi) kuona namna mradi huu unavyotekelezwa na namna fedha zinavyotumika.

“ Kupitia ziara hii na ripoti ya CAG tuliyoipitia, imeonyesha wazi namna fedha za uwekezaji zilivyotumika kama vile ilivyopanga na kiukweli tumefurahishwa sana na jambo hili,”amesema Kaboyoka.

Ameipongeza bodi ya Wakurugenzi wa TPA inayoongozwa na Balozi Ernest Mangu na uongozi wa Mamlaka hiyo chini ya Mkurugenzi Mkuu Bw.Plasduce Mbossa kwa utendaji na usimamizi mzuri wa fedha za mradi huo wenye tija kwa taifa.

Kaboyoka ameongeza kuwa moja ya viashiria vya kutumika vizuri kwa fedha hizo baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya bandari hiyo ni pamoja na ujenzi wa magati na upanuzi wa kina unaopelekea meli kubwa kutia nanga bandarini hapo.

Amesema utekelezaji wa mradi wa DMGP ni muhimu kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa inayoingia bandarini humo ili kuendelea kuifanya bandari ya Dar es Salaam na kuendelea kuifanya kuwa lango kuu la uchumi.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yatazidi kuifanya bandari hiyo kuwa shindani na tegemezi kwa nchi za jirani za ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa wajumbe wa Kamati hiyo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Daktari Bw.Baraka Mdima amesema mradi huo ulioanza mwaka 2017 unahusisha maeneo mawili, likiwemo la uboreshaji wa miundombinu na kuimarisha uwezo wa mamlaka hiyo.

Amesema tayari mafanikio mbalimbali yamefikiwa, ambapo hadi kufikia Machi 2025, uboreshaji wa gati namba 1-7 umekamilika kwa asilimia 100 na tayari gati hizo zinapokea meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 305 zenye uwezo wa kubeba makasha 8,000.
Ameongeza kuwa ujenzi wa yadi yenye mita za mraba 73,000 yenye uwezo wa kupokea magari 280,000 kwa mwaka pia umekamilika kwa asilimia 100 na tayari inatumika.

Pia amesema kuwa bandari hiyo ambayo inahudumia asilimia 95 ya shehena yote inayosafirishwa na kutoka nchi za jirani, imefanikiwa kuongeza kina cha lango la kugeuzia meli kutoka mita 12 hadi mita 15.5 na kuongeza upana wa lango hilo kutoka mita 140 hadi 170 na kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 305 tofauti na miaka ya nyuma ilipokuwa na uwezo wa kupokea meli zenye urefu wa mita 240 pekee.

Ameyataja maeneo mengine ya uboreshaji kuwa ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa reli ya ndani ya bandari na mradi wa kusimika umeme ili kuongeza ufanisi.

Amesema faida mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo tayari zimeanza kuonekana ikiwemo mapato kuongezeka.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huu;” amesema Bw.Mdima.

Awali, wakati akielezea mipango ya TPA ya kupanua soko zaidi la biashara baada ya maswali mbalimbali ya wabunge, Bw.Mangu ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu amesema mamlaka hiyo ina mipango mbalimbali, ikiwemo kuboresho bandari zilizopo mipakani na kuiomba Serikali kuzidi kuboresha mitandao ya barabara inayoingia katika nchi hizo .

“Tunalenga kukamata masoko na kuyashikilia vizuri likiwemo soko la Mashariki ya Jamhuri ya Congo (DRC) ambalo ni soko muhimu sana kwetu pia,” amesema.

Wakati wa ziara hiyo, wabunge wa kamati hiyo pia waliitaka TPA kuendelea kuboresha bandari zake mbalimbali inazozisimamia ili kuongeza ufanisi na mapato.

Mmoja wa wabunge hao Bw Japhet Hasunga amesema maboresho katika bandari mbalimbali hapa nchini kama vile ile ya Bagamoyo na ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya reli ya kisasa (SGR) yatasaidia kuongeza ufanisi na kuvutua wafanyabishara wengi kuzitumia bandari hizo badala ya kukimbilia nchi za jirani.

Naye Mbunge Ester Matiku amesema maboresho yanayoendelea katika bandari mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam yataifanya bandari hiyo kuwa shindani na tegemezi katika ukanda wa Afrika.