Katika miaka ya karibuni imezoeleka katika masikio ya Watanzania kuwa majukumu ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni uongozi, kutunga sera na sheria, na kusimamia na kuiwajibisha Serikali. Mara nyingi jukumu la kuwakilisha jimbo au kundi la watu linatajwa tu wakati kuna mazungumzo yanayohusu uchaguzi.

Hii ni tofauti na huko nyuma wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere ambako jukumu la uwakilishi ndilo lililokuwa kuu. Na ndiyo maana wakati huo kwenye kampeni wagombea walitumia alama kama jembe na nyumba kwenye matangazo na karatasi za kura za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kipindi hicho wabunge walikuwa ‘ndugu’, hivyo walikuwa wenzetu. Wabunge wa sasa si wenzetu ni waheshimiwa, ni viongozi! Wahenga walisema ‘Kauli huumba’.  Yeyote aliyeishi katika vipindi hivi viwili vya mitazamo tofauti atakubaliana na mimi kuwa mfumo na mienendo ya kupata wabunge na jina la cheo vinaakisi kinachoamuliwa na wananchi, na matendo ya wabunge ndani na nje ya Bunge.

Kwa kiasi kikubwa dhana ya uwakilishi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hususan Bara, imepotea. Ni wabunge wachache sana wanaofahamika kwa kazi halisi ya uwakilishi.

Kwa lugha nyepesi fasili ya uwakilishi inabeba matendo ya kujua mambo yaliyoko kwenye jimbo husika na hasa yanayohitaji kushughulikiwa na Serikali na kuyafikisha serikalini kwa ajili ya kushughulikiwa; na kuhudhuria mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo ya jimbo na kuwapa wananchi mrejesho.

Aidha, dhana ya uwakilishi ndiyo inayobeba utungaji wa sheria na kusimamia na kuiwajibisha Serikali. Hii ni kwa vile mbunge anatakiwa kushiriki katika shughuli hizi kwa niaba na manufaa ya jimbo lake, au kundi la wananchi analowakilisha.

Kinachoonekana Tanzania Bara katika miaka ya karibuni ni wagombea kufanya kampeni kupitia vyama vyao, na kutumia majina yao na ya vyama kunadi kinachoeleweka kama sera au ilani ya chama kuomba kura kwa wananchi na kuahidi kuwaletea mambo mbalimbali ya maendeleo.

Mbali na sera na ahadi, wagombea walio wengi wanatumia hongo kuwarubuni wapiga kura. Hiki ndicho kinachoeleweka moja kwa moja kama rushwa. Kisichotambulika kama rushwa na ambacho ndiyo rushwa mbaya zaidi, ni anayewania ubunge kuahidi kuwaletea wapiga kura fedha na rasilimali nyinginezo za kujenga miundombinu mbalimbali ya  huduma za kijamii na maendeleo. 

Hii ni rushwa mbaya kuliko ya kuhonga pesa, khanga, sukari na vitu vingine vinavyotolewa kwa watu wakati wa kampeni. Ubaya wa rushwa ya ahadi ni kwamba ni uongo unaowagusa wapiga kura wengi, na ambao umewafanya Watanzania wengi kufikiria kuwa kutoa ahadi za namna hiyo ndiyo kipimo sahihi cha kujua mbunge bora. 

Kosa hilo limekuwa kiasi cha kuonekana kuwa kutoa ahadi za namna hiyo ni halali wakati ni kosa, tena [kimsingi] la jinai! Na kwa vile ahadi hizo mara nyingi hazitimizwi, na zikitimizwa inakuwa danganya toto, watu wengi wamepoteza imani na ahadi hizo na kuona bora anayetoa hongo hapo hapo hata kama kidogo.

Kibaya zaidi ni kwamba mazoea ya hongo na ahadi hewa yamedhohofisha ahadi za kweli na zenye tija. Ni vigumu mgombea kushinda uchaguzi kwa kuahidi kupeleka matatizo serikalini au kuhimiza maendeleo kama hajatoa chochote au kuahidi yeye mwenyewe kuwa mhisani. Hali hii imezidi kudhoofisha dhana ya wabunge wawakilishi na kukuza dhana ya wabunge wafanyabiashara ya siasa wanaowekeza kwa “kununua kura” kwa mtaji wa hongo, au ahadi na kurudisha gharama zao kwa malipo mbalimbali wanayopata ndani na nje ya bunge. 

Huo ndiyo muktadha ambao tumekuwa tukipatia wabunge. Mwaka huu umekuwa tofauti kidogo kutokana na mwamko wa wapiga kura na vuguvugu la kutaka mabadiliko, na matokeo yamedhihirisha hilo kwa kiasi fulani.

Kipindi hiki tumepata wabunge wengi zaidi vijana, wasomi wengi zaidi, wapinzani wengi zaidi na kadhalika. Hata hivyo, pamoja na kuwa na mchanganyiko ulio tofauti na wa uchaguzi uliopita, wabunge wa kipindi hiki wanaweza wakawa wamefanana zaidi na wabunge wa kipindi kilichopita kuliko walivyo tofauti. Hii ni kwa sababu ni vigumu kupata matokeo tofauti kwa mfumo na njia zile zile.

Tayari katika siku mbili za kwanza za Bunge la 11 tumeshuhudia mienendo iliyojitokeza sana katika Bunge lililopita na ambayo iliwakera sana wananchi; kama vile lugha zisizo za staha, kejeli, vijembe pamoja na ubaguzi mkali wa kivyama na itikadi.

Hizi ni tabia na utamaduni ulio hasi kwa mabadiliko tunayoyataka na kaulimbiu ya Rais mpya ambayo tayari imekwishawapa Watanzania matumaini ya kupata mabadiliko wanayoyataka.

Aidha, kubaguana kiitikadi, kuzozana, kuzomeana, kukejeliana na kudharauliana ni mambo yasiyokuwa na tija na yanayoshusha hadhi ya Bunge letu tukufu vibaya sana; na hata heshima za wabunge mmoja mmoja. Wabunge wanatakiwa kukumbuka kuwa kila wanalofanya wanaweka historia vichwani mwa wananchi, vyombo vya habari na ‘Hansard’. 

Hata hivyo, haya yote yanaweza kubadilika kama wabunge watajiona wako bungeni kuwakilisha wananchi kwenye majimbo walikotoka, ikiwa kama sehemu ya Watanzania wote; na kuwa wapo pale kwa gharama ya Watanzania, na siyo vyama!  Vivyo hivyo na kwa wabunge wa Viti Maalum. 

Ni kwa wabunge kuwa wawakilishi wazuri, ndiyo na Bunge kwa ujumla litakuwa na tija na kutoa mchango stahili katika kuleta mabadiliko ya kweli, kudumisha amani, na kuleta maendeleo nchini.

Simu: 0784-463723