Bunge la Tanzania linaunga mkono msimamo wa Morocco katika kupata ufumbuzi wa mgogoro kati ya taifa hilo na taifa la Sahara Magharibi. Mwaka 1975 uliibuka mgogoro wa ndani kati ya Morocco na taifa la Sahara Magharibi linalotaka kujitangazia Uhuru. Mgogoro huu uliofanya Sahara Magharibi kujenga ukuta kama wa Berlin kule Ujerumani, umekuwa na madhara makubwa ndani ya taifa la Morocco.
Msimamo wa Morocco ni kuona mgogoro huo unamalizwa kidiplomasia kwa kuitisha kura ya maoni kwa wakazi wa eneo la Sahara Magharibi, kupiga kura kuamua kama wanataka kuendelea kuwa sehemu ya Morocco au kujitenga na taifa hilo kupata uhuru.
“Sisi kama Bunge la Tanzania tunaunga mkono msimamo wa Morocco wa kuitisha kura ya maoni, ambao ni msimamo wa Umoja wa Mataifa,” Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma hivi karibuni.
Lowassa alisema baada ya kuwa wamekwenda ziarani nchini Morocco, wamebaini kuwa mgogoro ule unaweza kumalizwa kwa njia ya amani badala ya kutumia mabavu. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa kuna shinikizo kubwa la kuendeleza mgogoro huo kutoka Algeria, nchi inayotaka kuona Sahara Magharibi ikipata uhuru na ndiyo inayoipa Sahara Magharibi msaada mkubwa wa kijeshi kwa kisingizio kuwa kuna Waalgeria wengi wakazi wa Sahara Magharibi. UN inataka mgogoro huo umalizwe kwa utaratibu wa mashauriano ya ndani kwa ndani.