Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndungulile, amewashauri wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), kujipanga kwa hoja ili watakapokutana na wabunge watoe ufafanuzi kuhusu mabadiliko ya sheria ya habari wanayoyataka.

Hayo ameyasema wakati alipokutana na wadau hao mkoani Dodoma wakati akizungumzia baadhi ya vipengele vilivyoachwa katika muswada wa habari.

Akizungumza na Mjumbe wa CoRI Deus Kibamba, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF Neville Meena, Ndungulile amesema, ujenzi wa hoja imara utashawishi wabunge.

“Muwe na ufafanuzi halisi na unaoweza kushawishi wabunge, tena kwa mifano. Mfano mnataka kusiwepo na leseni, je nchi nyingine zinafanyaje hasa za Afrika.

Nusrat Henje, Mbunge wa Viti Maalum akizungumza na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma

“Kila hoja mnayoitoa iwe na ufafanuzi mzuri kwa wabunge, mkifanya hivyo, mnaweza kushawishi wabunge na jambo linaweza kuwa rahisi,” amesema.

Naye Mbunge wa Mafinga Cosato Chumi, amesema, sheria zetu zinapaswa kuendana na mabadiliko makubwa ya teknolojia,vinginevyo zinaweza kuwepo lakini hazitekelezeki.

Chumo alitoa kauli hiyo baada ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF alipoeleza madhara ya kuwa na sheria za habari zinazoshusha taswira Tanzania kimataifa.

Balile amesema, kuwa na sheria inayokataza kuingia kwa machapisho ya nje bila kuweka vigezo halisi, kunasababisha taifa kuingia kwenye orodha ya mataifa yanayonyonga uhuru wa habari.

“Kuwa na sheria kama hii tena inayompa mwanya waziri kuamua kuzuia machapisho kwa na ma anavyojisikia, kunaweza kusababisha hata machapisho yenye umuhimu kutoka nje hata kama yana faida na nchi, kuzuiwa.

“Tunaamini kuna machaposho yanapaswa kuzuiwa lakini vigezo viwekwe wazi, kutokuweka wazi kunatoa taswira hasi, lakini katika ulimwengu huu wa teknolojia, unawezaje kuzuia machapisho wakati muda wote yapo kwenye simu?” Balile alihoji.

Mbunge Cosato amesema, kulingana na dunia ilipo sasa, ni vizuri bunge kutunga sheria zinazoendana na mazingira ili ziweze kutekelezeka.
“Ninaelewa mantiki ya hili, sioni kama sheria ya kuzuia machapisho inaweza kufanya kazi kwa wakati huu tulionao kwani muda wote machapisho yapo mkononi (kwenye simu). Sheria za namna hii zifanyiwe kazi,” alisema.

Hata hivyo, amesema hoja ya sheria kutoweka ukomo wa kiwango cha chini cha adhabu ya kifungo ina mashiko; “kweli ukiweka kiwango cha chini cha adhabu, maana yake unamlazimisha hakimu atoe adhabu ya kifungo, si kila kosa linahitaji kifungo.”

Akizungumzia utaratibu wa utoaji wa wa leseni kwa magazeti, Nusrat Henje ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum alisema, sheria inampa mwanya mtoa leseni (Habari Maelezo) kuamua nini cha kufanya kwa chombo cha habari husika.

“Wakati mwingine serikali inaweza kuamka na ‘stress’ na ikaja na maamuzi ambayo sio. Ni vizuri vyombo vya habari mambo yao yakawa yanafanyika kwenye bodi yao,” alisema.

Mbunge huyo alisema, kuna kila sababu kwa tasnia ya habari kuwa na sheria rafiki ili kutoa fursa kwa ujenzi bora wa taifa.

“Ninaona hoja zenu na umuhimu wake, sisi kama wabunge tutashauri kamati namna bora ya kuliendea hili. Tunatamani kuwa na sheria zinazoishi muda mrefu, si hivyo tu bali zinazotekelezeka,” alisema.

Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum amesema, kuna baadhi ya vipengele muhimu vya sheria ya habari vimeachwa na kwamba, kwa ufafanuzi uliotolewa na CoRI unashaiwshi kujumuishwa kwenye sheria ijayo.