NA ANGELA KIWIA
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametangaza hali ya
hatari nchini. Wametangaza ya kuwa maisha ya Watanzania si salama tena,
tunaishi maisha yasiyo na uhakika wa kuiona kesho kutokana na vitendo vya
uhalifu kushamiri nchini.
Wakichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
katika Mkutano uliomalizika, wamebainisha kuwa hali nchi ilipofikia kwa sasa si
nzuri kwa sababu Taifa linapitia katika kipindi kigumu.
Wabunge wamefikia hatua ya kuitaka Serikali kuwapatia ulinzi binafsi kutokana na
hofu waliyonayo katika baadhi ya maeneo wanayoishi na utendaji kazi wao
unakuwa shakani.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Kamati hiyo ya Bunge, Mwenyekiti wa
Kamati, Balozi Adadi Rajabu, alisema ulinzi huo wa wabunge uwe katika makazi
ya wabunge wakiwa wanatekeleza majukumu ya kibunge mjini Dodoma na katika
majimbo yao.
Mapendekezo hayo ya kamati yaliungwa mkono na wabunge wengi, jambo
ambalo si la kupuuza hata kidogo.
Kupitia mkutano huu wa Bunge, wabunge wetu wametuthibitishia pasi na shaka
kuwa maisha yetu yapo hatarini, hatuko salama tena.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge ni moja ya kamati nyeti nchini. Ni kamati
inayopokea na kujadili masuala yanayohusiana na usalama wa nchi, usalama wa
raia na mali zao pamoja na mambo yote yanayohusu usalama kwa ujumla.
Kupitia Kamati hii ya Bunge, wawakilishi wetu wamebainisha ni kwa kiasi gani
ulinzi wa Watanzania ulivyodorora. Walinzi wetu wasivyotimiza wajibu wao kiasi
cha kusababisha raia kuishi kwa hofu na kuweweseka kila mara kwa hofu ya
kupoteza uhai wao.
Wapo wanaoweza kupuuza hili. Lakini kwa wachunguzi wa mambo lazima wahoji,
wajiulize na watafakari kwa kina kuhusiana na taarifa hii ya kamati ambayo
inazalisha maswali mengi.
Kauli hizi za wabunge ni kauli tata zenye kusababisha juu ya masuala mazima ya
shaka juu ya usalama wa raia na mali zao pia usalama wa nchi kwa ujumla.
Wabunge wanataka ulinzi. Wanataka kulindwa na askari wetu ili wasidhurike.
Wabunge wetu wamenusa hatari ya kuishi bila ulinzi kiasi cha maisha yao kuwa
hatarini.
Wawakilishi wetu hawa wahofia usalama wao hapa nchini. Wanaitaka Serikali
kuwapatia ulinzi kila watakapokuwa waweze kulindwa na askari wetu ili
kuwaondoa hofu ya kudhurika.
Hii si dalili njema kwa nchi yetu. Si jambo la kushangilia wala kujivunia kutokana
na nchi kukumbwa na kizunguzungu cha hofu kwa viongozi wetu.
Wabunge hawa wanaolilia ulinzi ndiyo wanaolipwa fedha nyingi kutokana na kodi
zetu. Wawakilishi ambao maisha yao hayafanani kabisa na maisha yetu sisi
tusiokuwa na uhakika wa japo mlo mmoja.
Wakati wao wakitutangazia kudorora kwa usalama nchini na kuomba ulinzi wa
bunduki kila walipo, sisi wapiga kura wao na waajiri wao tunahaha kupata japo
unga wa uji ili kulinda uhai wetu!
Pamoja na kuwalipa mamilioni ya shilingi, bado wanataka tuwatafutie walinzi wa
kuwalinda ambao tutawalipa pia!
Hakika huu ni utani wa ngumi…