Wabunge wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumatatu walilaani kitendo cha kuchomwa kwa nyumba ya rais Joseph Kabila.
Katika taarifa ya pamoja, wabunge hao walikiita kitendo hicho kuwa cha kinyama na kutoa wito kwa raia kuotojihusisha na vitendo ambavyo vingechangia kuzorota kwa amani na maendeleo katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Mapema Jumatatu, washambuliaji walichoma nyumba ya rais katika shamba lake lililo karibu na kijiji cha Musienene, na kumuua afisa mmoja wa polisi. Haikujulikana mara moja jinsi afisa huyo alivyouawa.
Ingawa hakuna aliyedai kuhusika na shambulizi hilo, afisa mmoja wa jeshi aliliambia shirika la habari la ufaransa kwamba wanashuku waasi wa kundi la Mai Mai, na kusema kwamba waliiba kwenye nyumba hiyo kabla ya kuiteketeza moto.
Mashambulizi yanayotekelezwa na Mai Mai dhidi ya wapiganaji wa Kongo na hata wanaotoka nje katika eneo la Kivu Kaskazini yameongezeka katika miezi ya karibuni.