Wabunge wameipogeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha ujenzi na ukarabati wa soko la Kariakoo ambalo limeboreshwa na kuwa na viwango vya kimataifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Justin Nyamoga leo (Aprili 12,2025) Dar es Salaam wakati walipokagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara.

“Sisi kama Bunge tumekagua na kujionea kazi kubwa ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyetoa shilingi Bilioni 28.03 ili kujenga soko jipya na kukarabati lile lililoungua ambapo mradi huu utanufaisha watu wengi” alisema Nyamoga.
Nyamoga aliongeza kusema Wabunge wameridhishwa na viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa katika Soko la Kariakoo unaolifanya kuwa na taswira ya kimataifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Festo Dugange alisema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2022 umefikia asilimia 98 ukigharimu zaidi ya Bilioni 28 ambapo utaongeza nafasi za biashara toka 1,662 hadi 1,907.
Dugange alieleza kuwa lengo la Serikali ni kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara katika soko la Kariakoo ambalo litafanya kazi kwa muda wa saa 24 kuwa maandalizi yamekamilika.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alisema soko litafunguliwa hivi karibuni na kwamba Serikali itahakikisha wafanyabiashara wote wenye sifa wanapatiwa maeneo kulingana na sifa zilizoanishwa.
Akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara sokoni hapo, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim alisema tayari wafanyabiashara 1,002 kati 1,520 wa kundi la kwanza wamepangiwa maeneo ndani na mfumo wa TAUSI.
CPA Abdulkarim aliongeza kusema, wafanyabiashara 518 kati ya 1,520 wana changamoto mbalimbali ikiwemo 194 kuwa na madeni ya nyuma, 134 hawajaza fomu maalum na 190 hawana namba ya kitambulisho cha Taifa (NIDA) na Namba ya Mlipa Kodi (TIN) , hivyo hawajapangiwa maeneo hadi sasa.



