Ijumaa wiki hii Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasilisha bajeti yake bungeni. Kama ilivyo kawaida tayari harakati zimeanza. Wabunge wanapigana vikumbo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco William Mhando amesimamishwa kazi na Wizara ya Nishati na Madini inapambana na upatikanaji wa umeme.
Baadhi ya wabunge wanashutumiwa kuwa wanaitetea Tanesco kwa kuwa wana zabuni za kuuza vifaa mbalimbali katika shirika hilo.
Mwelekeo tunaouona tunaweza kushuhudia yaliyotokea mwaka jana. Wizara hii ilikuwa na mivutano mikubwa mwaka jana hadi bajeti yake ikakataliwa. Rais Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza la Mawaziri na kumwondoa William Ngeleja akamwingiza Profesa Sospeter Muhongo. Pia alimuondoa Katibu Mkuu David Jairo akamwingiza Eliakimu Maswi.
Wawili hawa ndani ya muda mfupi wamefanya kazi ya kupigiwa mfano. Wamebadili sura ya wizara hasa katika eneo la kupata umeme wa uhakika. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam wamehakikisha mgawo wa umeme unatoweka kabisa. Transfoma zimefungwa katika maeneo mbalimbali, mita za Luku zimesambazwa na hata katikati ya Jiji msongo mpya wa umeme umejengwa ulioleta utangamano.
Kwa hali yoyote sisi hatutaki kujiingiza kwenye mtego wa mgogoro wa kutaja iwapo wizara ilifanya jambo jema kuziondoa kampuni za Oryx na Camel Oil kwenye orodha ya kuiuzia mafuta IPTL na kuwapa fursa hiyo BP. Hata hivyo, tutakuwa wa ajabu kweli ikiwa hatuwezi kuiona nia njema ya kulikinga taifa dhidi ya gharama zisizo za lazima.
Kwamba kampuni hizi zilikuwa zinauza mafuta kwa IPTL kwa gharama ya Sh 1,800 na mafuta hayo zinayanunua kutoka kwa BP, lakini leo tunapata ujasiri wa kuzitetea kuwa zilikuwa na haki kisheria kuendelea kuuza mafuta kwa bei ya juu badala ya BP wanaouza mafuta yale yale kwa bei ya Sh 1,460. Hapa wala hatusiti kutaja ukweli kwamba BP ina ubia na serikali wa asilimia 50 kwa 50.
Tunasema katika hili hatupo kumtetea yeyote isipokuwa iwe ni Waziri au Katibu Mkuu aliyeepusha gharama hizi kwa taifa, bila kuwashutumu tunasema wabunge wajiepusha kufanya kazi kama roboti. Sheria ina kanuni zake, na tukibaini kuwa sheria inanyonga uchumi wa nchi, ni lazima tufike mahala sheria itumikie masilahi ya taifa na si ya mtu binafsi.
Tunasema Waziri Muhongo ni mtaalamu na Katibu Mkuu Maswi kwa muda aliofanya kazi ndani ya wizara hii, ameonyesha usimamizi mzuri. Ni vyema wabunge wakawapa fursa ya kulitumikia taifa wawili hawa angalau kwa miaka mitatu, tukashuhudia watalifikisha wapi taifa letu, kwani mwelekeo walio nao ni mzuri. Ijumaa wabunge mjipange kusahihishana si kusulubiana.