Wasia nnautoa, baba alivyonambia.
Nieleze sawa sawa, nanyi mpate sikia.
Wa kwaonya enyi sawa, inafaa kusogea.
Jambo la kwanza kasema, majivuno hayafai
Muovu mtendee wema, japo mtu humnunui
Mjivuno ni hasama, yanaleta uwadui.
Dini ni jambo la pili, baba alivyonambia,
Ulimi wa pilipili, haufai kutumia,
Hutenga watu wawili, hadhari nakwambia.
Ulimi mzuri mali, hupendeza wasikizi,
Huvuta walio mbali, hufuata maongezi,
Sikia yangu kauli, hilo ni jambo azizi.
Nimenukuu wimbo huo ulioimbwa na bendi ya muziki wa taarab ya Black Star ya jijini Tanga, nikiwa na madhumuni ya kuweka msisitizo katika suala ninalokusudia kulizungumza.
Wiki iliyopita, vyombo vyetu vya habari nchini vimetufahamisha mambo mengi yaliyokuwa yakizungumzwa na waheshimiwa wabunge wetu katika Bunge la Bajeti ya Serikali mwaka 2016/17 ambalo hadi leo bado linaendelea mjini Dodoma.
Katika Bunge hilo, wake kwa waume ambao ni wabunge wetu walikuwa katika majadiliano makali na mazuri kutokana na hoja mbalimbali zilizotolewa na Serikali na wabunge wenyewe. Kauli zilizotolewa zilikuwa za kupendeza na za kuvutia wananchi.
Aidha, majadiliano mengine yalibeba na kutawaliwa na kauli chafu zilizowakera baadhi yao, Serikali na sisi wananchi. Hakika kauli hizo hazikuwa na mvuto wala adabu kwa mtu muungwana yeyote, kwa sababu hazikuwa na chembe ya wema, zaidi ya kujenga chuki na mfarakano kati ya wabunge na wabunge, kambi zao za upinzani kisiasa na wananchi katika majimbo yao ya uchaguzi.
Inaelezwa na vyombo vya habari kuwa mnambo Aprili 5, wabunge walikuwa wanajadili bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba. Katika majadiliano hayo, Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki, Mheshimiwa Goodluck Mlinga ( CCM), alitoa kauli kuwa wabunge wanawake wa Chadema wanapata nafasi hizo kwa sifa ya kuitwa ‘baby’.
Kauli hiyo ilizua kasheshe na sokomoko ndani ya Bunge hata kumlazimu Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kuamuru wabunge wanawake wa Chadema na CUF kutolewa nje ya Bunge.
Wabunge hao hawakupendezwa na kauli ya Mlinga kwa sababu wamevunjiwa heshima yao bungeni na utu wao mbele ya wananchi. Mwenyekiti wa Chama Cha Wabunge Wanawake Tanzania ( TWPG ) Mheshimiwa Magret Sitta amelaani na kuonya kauli za kudhalilisha utu wa wanawake bungeni uwepo tena.
Ingawa wabunge hao wa Kambi ya Upinzani Bungeni wamefedheheswa na kudhalilishwa ndani ya Bunge, bado wamedai na kumtaka mbunge mwenzao Mlinga afute kauli yake. Hakufuta.
Juzi tumemsikia Mbunge wa jimbo la Kawe, Dar es Salaam, Mh. Halima Mdee, akiwatangazia wananchi na kuandika barua kwa Mwenyekiti wa TWPG kujitoa rasmi katika chama hicho kwa maelezo kuwa wamedhaliliswa ndani ya Bunge. Kilichofanywa si kitendo cha kiungwana.
Ukweli lazima niseme hayo yaliyotokea na huenda yakatokea tena bungeni, ni mavuno ya mazao yaliyopandwa na wabunge wetu. Kati ya wabunge wa Kambi ya Upinzani na wa kambi ya chama tawala, wote waliopo na wale wa mabunge yaliyopita tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Wamelima, wamepanda, wamepalilia na sasa wanavuna walichopanda. Mavuno haya ni shubiri kwao na ni kakasi kwetu wananchi. La kusikitisha, hata wabunge wapya wameingia katika mavuno haya na wala hawaelewi mbegu kaleta nani kwa madhumuni gani.
Mara kwa mara vyombo vya habari na wananchi wamekuwa wakikemea kauli chafu za vijembe, mipasho, misuto, kebehi, tuhuma na dharau hazifai hapo bungeni. Bunge ni chombo muhimu, kitukufu na maridhawa. Si mahali pa kucheza michezo na kuimba nyimbo kama vile za mdumange, sangula, kigodoro na kadhalika. Ukifanya kama hivyo ni kulivunjia heshima Bunge.
Kauli za bungeni lazima ziwe zenye taadabu, busara, hekima, utu na uungwana. Kauli za mbunge ni nukuu, agizo kwa Serikali na raia. Ndiyo maana kabla ya mbunge kuchangia hoja azingatie kanuni za Bunge na miongozo yake. Awajibike kuhariri maelezo yake kwanza ili kuwavuta wasikiao na wapendezwe nayo.
Mifano iko mingi si Bunge hili tu, hata yaliyopita baadhi ya wabunge wamekuwa wakitoa kauli chafu. Leo wabunge wapya wanapoingia bungeni wanadhani kutusi, kukashifu au kudhalilisha utu wa mtu, chama cha siasa au Serikali ndiyo sifa na uwezo wa ubunge. Nasema ng’o. Wabunge wetu mjisahihishe.
Wananchi wenu wanapenda kusikia hoja na malumbano yenye shibe. Wanataka shule, hospitali, maji safi na salama, miundombinu n.k. Kumbukeni ulimi mzuri mali, hupendeza wasikizi/