Kwa mara nyingine, wiki hii Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanakabiliwa na mtihani wa kuthibitisha kama kweli ni wawakilishi halali wa Watanzania, au la!
Kuanzia kesho watakuwa na fursa ya kujadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inayohusu ufisadi wa fedha katika Akaunti ya Escrow.
Umoja wa wabunge katika kuijadili kashfa hii umeshaonekana, na ni wazi kuwa Watanzania wanasubiri kusikia kile wanachotarajia – nacho si kingine, bali mjadala wenye tija kwao na kwa Taifa lao kwa jumla.
Mara kadhaa mijadala ya aina hii imekuwa ikitawaliwa na jazba. Wananchi hawatarajii kuyaona hayo. Shida yao si kuona au kusikia ufundi katika uzungumzaji, bali ni kuona au kusikia hoja zenye mantiki na vionjo vyenye mwelekeo wa kutetea maslahi ya wananchi na nchi yao.
Wananchi hawatarajii kusikia kunakuwapo ujanja ujanja wa kukwepesha hoja kwa visingizio visivyo na maana kama vile madai ya kwamba kuibuliwa kwa Escrow eti ni matokeo ya harakati za urais mwakani.
Wabunge ni watumishi wa wananchi. Wametumwa na wananchi ili wawawakilishe. Kama nchi hii ingekuwa na uwezo wa kuwa na ukumbi wenye kuhimili watu milioni 45 wa Tanzania, bila shaka kazi hii ingefanywa na wananchi wenyewe. Lakini kwa kuwa hakuna ukumbi wala mantiki ya watu wote hao kukusanyika pamoja, ndio maana wabunge 352 wamechukua dhamana ya kuwawakilisha wananchi wote wa Tanzania.
Mijadala ya Monofu ya Samaki, EPA, na hata Richmond ilithibitisha kuwa nchi ikiwa na wabunge makini, haiwezi kuishiwa hoja za kujadiliwa bungeni. Huu wa Escrow ni kielelezo kingine kinachothibitisha kuwa wabunge wakiamua, kuna madudu mengi sana ambayo yanaweza kuibuliwa na hata kufikia hatua ya kuwawajibisha wahusika.
Matarajio yetu ni kuona baada ya Escrow, wabunge wanahoji ufisadi katika maeneo mengine, kama kule Wizara ya Maliasili na Utalii ambako kumegeuzwa kuwa mgodi wa mafisadi wachache ambao wanaungwa mkono na kulindwa na viongozi wa wizara.
Moto huu wa Escrow ukielekezwa katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), tuna hakika asilimia 90 ya wakurugenzi na watendaji wengine watafikishwa katika vyombo vya sheria na hata kufungwa.
Watanzania wamechoka kuibiwa. Haiingii akilini kuona maskini wakiyakimbia makazi kwa kukwepa kukamatwa kutokana na michango ya maabara, lakini kukawapo kundi la wachache walioamua kufaidi – bila huruma mabilioni ya fedha za umma.
Huu ni wakati wa wabunge kusimama kidete kufanya kazi ya kweli ya uwakilishi wa wananchi. Ni wakati wa kuthibitisha kuwa mhimili wa Bunge ukiamua kufanya kazi, hakuna kinachoshindikana katika nchi hii.
Mwisho, tunawasihi wabunge watende haki. Wawe tayari kuwawajibisha wote waliohusika kwenye sakata hili, lakini wasitumie mwanya huu kuwakomoa ‘wabaya wao kisiasa’ kama tulivyoona katika Ripoti ya Operesheni Tokomeza. Macho na masikio ya Watanzania sasa yanasubiri kuona na kuasikia kazi iliyotukuka kutoka kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa pamoja, tukiamua, Tanzania bila ufisadi inawezekana kabisa.