Bunge la Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 linaanza leo mjini Dodoma, huku Watanzania wakitarajia kuona na kusikia wabunge wao wakipitisha bajeti inayojibu matatizo yanayowakabili.
Kwa hakika hiki ni kipindi mwafaka kwa wabunge wetu kuonesha umahiri wao katika kutetea maslahi ya wananchi waliowatuma kuwawakilisha bungeni.
Matarajio ya wengi ni kwamba wabunge wetu wamejipanga ipasavyo kuhakikisha wanatanguliza maslahi ya umma, bila kujali tofauti za itikadi za vyama vyao vya siasa.
Itapendeza kuona pia katika Bunge hili la bajeti wabunge wanaheshimu na kufuata Kanuni za Bunge ikiwa ni pamoja na kuepuka kulumbana na kutoleana maneno ya kejeli yasiyo na tija kwa wananchi.
Kwa mantiki hiyo, wabunge wanatazamwa kama kioo cha jamii wanayoiwakilisha, hivyo haitarajiwi kuona na kusikia wanatetea na kupitisha bajeti ambayo ni maumivu kwa Watanzania.
Umoja na mshikamano wa wabunge unahitajika kwa kiwango cha juu kufanikisha dhamira ya kupitisha bajeti itakayojibu matatizo ya wananchi.
Lakini, kwa upande mwingine, Spika wa Bunge na Naibu wake wanategemewa kwa kiasi kikubwa kuongoza vikao vya Bunge kwa hekima na busara, lakini pia kwa kuzingatia na kufuata Kanuni za Kudumu za Bunge.
Sisi JAMHURI tunaamini kuwa mshikamano wa dhati kati ya Spika, Naibu wake, mawaziri na wabunge ndio utawezesha kupitisha bajeti itakayowaletea wananchi maendeleo ya kweli katika nyanja mbalimbali.
Hatutarajii kuona wabunge wanageuza mkutano huu wa Bunge uwanja wa malumbano ya hoja kwa lengo la kujipatia umaarufu binafsi na wa kisiasa.
Matarajio yetu ni kwamba mkutano huu wa Bunge la Bajeti utafanyika na kuhitimishwa kwa amani, huku ukiwa umepitisha bajeti inayokidhi mahitaji ya Watanzania.
Mungu libariki Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amina.