Wiki iliyopita nilijizuia kuandika juu ya Bunge na wabunge wetu. Nilijizuia baada ya kusikiliza mjadala uliokuwa unaendelea bungeni, nikawasikiliza wabunge maslahi wanaochangia kwa nguvu hadi wanatokwa na povu midomoni, bila kulieleza Bunge sawa bin sawia kuwa maumivu waliyopata kwa wanahabari yanatokana na maovu yao.
Wakati Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, chini ya Dk. Fenella Mukangara inawasilisha bajeti yake, wabunge hawa wametoa kauli za ajabu. Wanalenga kulichochea Bunge kukandamizi uhuru wa vyombo vya habari. Wanaihamasisha Serikali kutunga sheria ya kusimamia vyombo vya habari, kwa maana ya kuvikandamizi. Imenisikitisha, na nadhani hapa niweke kumbukumbu sawa.
Sitanii, leo nitataja kwa majina. Nianze na huyu kinda Juma Nkamia, Mbunge wa Kondoa Kusini. Nkamia alimwondoa madarakani Paschal Degera kwa fitina. Mwaka jana, huyu Nkamia amepelekwa India na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Alipelekwa kujifunza Sheria ya Haki ya Kupata Habari inavyofanya kazi.
Nimebahatika kusoma ripoti ya kundi la wabunge hawa waliokwenda India. Ni aibu. Aliyoyazungumza Nkamia yamethibitisha ripoti iliyoandikwa. Kundi la wabunge hawa, badala ya kujifunza jinsi Sheria ya Haki ya Kupata Habari inavyofanya kazi, kwa kukutana na viongozi kadhaa nchini humo, waliishia kwenda kufanya shopping na wengine wakatokomea hospitalini kupima afya zao.
Wapo wanaohoji, na nadhani hapa niungane nao kwamba uandishi wa Nkamia umekaaje? Aliwahi kusoma akashinda somo la ‘News Reporting’? Kama alishinda, amewahi kuandika hata makala moja inayoweza kupatikana kwenye maktaba yoyote ya dunia hii kama mwandishi? Majibu ninayopata yanasikitisha. Naye anayajua, siamini kama amepoteza kumbukumbu kiasi hicho.
Wapo wanaohoji pia alipataje fursa ya kwenda Sauti ya Amerika (VOA). Wapo wanaosema wapigakura walivutiwa na sauti ya kutangaza mpira wakamchagua bila kumfahamu vyema. Matamshi yake ya kudharau wanahabari yamethibitisha hilo. Anathubutu kumtukana mamba wakati hajavuka mto. Nkamia angeeleza, kuwa matusi yake kwa wanahabari yanatokana na tishio la mwanahabari Khamis Mkotya, anayetaka kugombea jimboni kwake. Basi.
Sitanii, nije kwa huyu John Komba. Komba angelieleza Bunge tu. Huyu ni Mbunge wa Mbinga Magharibi. Hakuwa na sababu ya kulipotosha Bunge. Alipaswa kuliambia Bunge kuwa anachangia kwa uchungu kiasi hicho, baada ya kuliwa Sh milioni 6 na mtu aliyejipendekeza kwake akiamini ni mwandishi kumbe ni kanjanja.
Tena kibaya zaidi, fedha hizi alizoliwa Komba akiwa pale Peacock Hotel Dar es Salaam, zilikuwa za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Wanahabari wamemshughulikia mtu huyu aliyemtapeli Komba, mbunge mwingine mbumbumbu anamtetea. Anasema ameonewa. Ni masikitiko makubwa. Komba angesema wazi kuwa analilia fedha zake badala ya kutukana taaluma ya habari.
Yupo huyu Hamisi Kigwangwala. Huyu wengi wamekuwa wakitilia shaka kiwango chake cha uelewa. Anapiga kelele na kulichagiza Bunge litunge sheria kali, lakini haelezi kuwa analilia kilichoandikwa magazetini juu yake. Yeye aliomba msamaha wa kodi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) akidai anajenga hospitali Nzega.
Sina tatizo na kupewa msamaha huu, ila msamaha huu ameutumia vibaya. Badala ya vifaa vilivyoingizwa nchini chini ya msamaha wa kodi kupelekwa Nzega, akafungua duka Kigamboni. Vyombo vya habari vimebaini kuwa anauza vifaa vilivyosamehewa kodi. Inamkereketa anakwenda bungeni kushambulia waandishi. Hii inamaanisha nini?
Sitanii, waangalie Ester Bulaya na Stephen Wasira. Wabunge hawa wanafanyiana umafia kupitia vyombo vya habari. Kila mmoja anadaiwa kumchafua mwenzake kupitia magazeti ya udaku, ikiwamo kusingiziana yale mambo ya ‘David Cameron’. Leo wanavichukia vyombo vya habari wakati chanzo cha matatizo ni wao.
Tatizo la Bulaya na Wasira ni ubunge katika Jimbo la Bunda. Hawa wanatumia kila mbinu, safi na chafu kupata jimbo hili mwaka 2015, lakini wanahabari wakizibaini na kuandika mbinu hizi, Bunge linapotoshwa kuwa litunge sheria ya kuminya hata uhuru kidogo uliopo. Nadhani tulipofika sasa tuseme hapana.
Nije kwa rafiki yangu Aden Rage, Mbunge wa Tabora Mjini. Yeye anataka usajili wa magazeti uwe Sh milioni 500. Ukiuliza kinachomsukuma Rage ni yeye kubofua ndani ya klabu ya Simba. Unamuuzaje mchezaji kama Emmanuel Okwi wakati msimu wa ligi unaendelea hata kama wangekuwa wanakupatia shilingi trilioni moja? Waandishi wakichambua hili anakereka anaona bora magazeti yafutwe.
Binafsi nasema, hakuna nchi yoyote duniani iliyopata kuendelea bila kuwa na uhuru wa vyombo vya habari. Tukithubutu kufanya hivyo, tutajenga makundi ya wezi, majangili na wakwepa kodi kupitia bungeni. Vyombo vya habari pekee ndivyo vinavyoweza kusaidia. Wabunge kama hawataki kuandikwa vibaya, wajiepusha kufanya mambo mabaya.
Sitanii, na hapa naomba nitangaze. Tunaisubiri kwa hamu hiyo sheria. Kama Dk. Mukangara alifikiri wanahabari ni laini kama mchicha uliochemshwa, amepotea njia. Akamuulize Mzee John Samuel Malecela. Magazeti, redio na televisheni vina joto kuliko moto wa gesi. Akitikisa kiberiti na kujaribu kufuta hata huo uhuru kidogo uliopo, atashuhudia historia ambayo hajapata kuifikiria maishani.
Tunausubiri muswada alioahidi, tuone hawa wabunge maslahi watafanyaje. Narudia, sisi wanahabari hatuna jeshi, polisi wala magereza, ila wakitaka kufahamu wakamuulize Eliakimu Simpassa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Mamlaka ya Bunge. Tunawasubiri.