Hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha mahakamani wabunge watatu ambao ni wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa mashitaka ya kushawishi na kuomba rushwa ya Sh 30,000,000.

Tunaambiwa wakiwa katika hoteli ya kitalii jijini Dar es Salaam waliomba rushwa hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo kwa lengo la kumsaidia ili taarifa ya halmashauri yake ipitishwe kiulaini.

Mahakama imewaachia kwa dhamana ya Sh milioni 5. Yaani mlungula wa milioni 30 na dhamana milioni 5!

Mbunge mwingine naye amefikishwa mahakamani akituhumiwa kuwa alishawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Naye amepewa dhamana ya Sh milioni 10.  Niongeze kuwa waheshimiwa hawa wote wanne ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wabunge kufikishwa mahakamani kwa shutuma za rushwa ni aibu kubwa. Ni aibu hata kwa askari wa polisi au kamishna wa kodi. Lakini mbunge ana kazi ya kuisimamia Serikali na kutuwakilisha. Amechaguliwa kutokana na kura zetu, hivyo rushwa inapopenya hata bungeni, basi hatuna demokrasia tena,

Kuna watakaosema lakini hawa wametuhumiwa tu, hawajaonekana na hatia. Ni kweli, lakini Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutoa mfano wa Julius Kaisari akisema: “Mke wangu hapaswi hata kutuhumiwa.”

Kaisari alimwacha mkewe kwa tuhuma tu. Alisema tuhuma peke yake, hata kabla ya kuthibitishwa, zilitosha kwa Kaisari kumwacha mkewe ili alinde heshima yake.

Tukiachana na hizo kesi za wabunge zinazoendelea mahakamani,  nani asiyejua kuwa wabunge wengi (si wote) wanaingia ‘Mjengoni’ kwa matarajio ya kujitajirisha na kujinufaisha wao binafsi badala ya kuutumikia umma?

Si ajabu leo wengi wanakimbilia ubunge, tena wako tayari kugawa milungula ili waukwae ubunge. Zamani wakitoa ‘takrima’ ya pilau na khanga, eti ni mila ya Kiafrika. Leo wanamwaga mamilioni. Matokeo yake ndio mbunge kuomba rushwa ili arudishe pesa zake ‘alizowekeza’.

Hili si jambo geni. Kwa mfano, mwaka 2012 aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliwataja baadhi ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuwa waliomba rushwa kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya. Mwaka ule ule wa 2012 Mbunge wa Bahi alipelekwa mahakamani na Takukuru kwa tuhuma za kupokea hongo ya Sh milioni moja kutoka Halmashauri ya Mkuranga.

Lakini tutarajie nini kutoka kwa wabunge ambao wamepitia mchakato mzima wa uchaguzi uliojaa hongo na rushwa? Hawa wameingia bungeni kwa kutumia hongo. Ni dhahiri kuwa wataendelea na tabia hiyo hiyo. Kama walitoa hongo kuchaguliwa sasa watadai hongo ili kujilipa gharama za kuchaguliwa.

Kwa mfano, Julai mwaka jana waandishi walio makini (nawapongeza) walitutaarifu kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge kupitia viti maalumu CCM ulikuwa “kufuru tupu” kwa vile ulitawaliwa na hongo.

Habari kutoka vyanzo vya ndani ya CCM na jumuiya zake zilieleza kuwa kulikuwa na baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge ambao walimwaga kiasi kikubwa cha fedha kuwahonga wajumbe wa vikao mbalimbali kuanzia kata, wilaya hadi mikoa waliowapigia kura.

Mbali na kumwaga kiasi kikubwa cha fedha kwa wajumbe, pia walidaiwa kuwahonga watendaji ambao waliwatumia kuwaandalia mikutano “isiyo rasmi” kwa ajili ya kukutana na wajumbe wapiga kura.

Je, chama kiliwachukulia hatua hawa watoa na wapokea hongo wakati wa kura za maoni? Je, Takukuru iliwanasa wangapi na kuwakifisha mahakamani?

Tuliambiwa kigogo mmoja mwenye ukwasi mkubwa alikuwa anatoa hadi Sh 200,000  kwa kila mjumbe. Mwanachama mmoja wa Umoja wa Wanawake (UWT) alilalamika: “Kuna wajumbe kama 300 hivi, kila mmoja mara ya kwanza alipewa Sh 150,000, lakini baada ya Bunge kuvunjwa walipewa Sh. 200,000.  Yaani ukifika kwenye ofisi za kata kama hujatoa fedha, hakuna anayekusikiliza. Akija aliye toa fedha utashangaa anavyoshangiliwa.  Jamani CCM imefika hapa kweli!”

Mwanachama huyo alisema kuwa kwa mwelekeo wa sasa ndani ya CCM ni miujiza kama mtu hana fedha za hongo, kuchaguliwa.

“Kama mtu ananunua wajumbe unafikiri akipata huo ubunge atawakumbuka waliomuuzia kura? Hii ni biashara ya kura. Inauma kweli,” alilalamika mwanamama huyo aliyetoka Kinondoni, Dar es Salaam.

Licha ya kuwapo madai hayo, viongozi wa CCM walipohojiwa walisema eti hawana taarifa kuhusu vitendo vya hongo miongoni mwa wagombea. Katibu Msaidizi wa UWT  Mkoa wa Dar es Salaam alipoulizwa alisema kwa ufupi kuwa hawana taarifa.

Mfano mwingine ni wa Angelina Mabula, mmoja wa wanawake waliojitahidi kugombea ubunge na leo ni Naibu Waziri. Yeye anasema wakati ule wa kura za maoni alipewa jina la “Kambi ya Masikini” kwa sababu ya kukataa kutoa hongo.

Mabula anazidi kusema: “Baadhi ya wananchi walitaka niwape rushwa hasa katika kipindi cha kura za maoni ili wanichague, lakini nikakataa na wakaanza kuniita ‘Kambi ya Masikini’”.

Mabula hakuwa akizungumza jambo geni katika chama chake. Hata aliyekuwa Rais, Jakaya Kikwete aliwahi kukiri Novemba 2013 kuwa CCM imeshindwa kupambana na rushwa.

Akaongeza: “Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana. Iwapo mwaka huo tutafanikiwa kuishika Serikali, basi mwaka 2020 katu hatutarudi tena madarakani.”

Akiwahutubia watendaji wa CCM wa mikoa na wilaya, Kikwete alisema: “Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za vocha (muda wa mawasiliano). Ndugu zangu hatutafika.”

Huyu alijua alichosema, si kama wale vigogo wenzake wanaosema “hatuna taarifa”. Alikuwa mkuu wa nchi na ripoti zote za siri zilikuwa zinamfikia yeye. Hata hivyo, sina hakika kama baada ya kusema hayo Kikwete alichukua hatua zozote akiwa mwenyekiti wa chama na rais wa nchi. Lakini kuna wanaosema hata wakati yeye alipochaguliwa urais fedha zilimwagwa, tena mabilioni.

Huu ndio utamaduni ulioota mizizi katika CCM. Leo nani anaweza kushangaa kuona wabunge wakidai hongo za mamilioni kutoka mashirika ya umma na halmashauri za wilaya. Wanadai posho mbili, kutoka Ofisi ya Bunge na kutoka mashirika. Nani atashangaa kuona wabunge wakihema kutafuta “lanchi” kutoka mashirika wanayoyasimamia?

Pamoja na haya ni kosa kufikiria kuwa wabunge wanaotoa na kupokea hongo ni kutoka CCM peke yake. Hao wanasikika zaidi kwa sababu hicho ni chama tawala chenye utajiri mkubwa, tena wako wengi bungeni. Wapinzani wako wachache ingawa idadi yao inaongezeka.

Ninachosema hapa ni kuwa hata na wabunge wa upinzani nao wameanza kuathiriwa na ugonjwa huu wa saratani ya rushwa. Nao pia (baadhi yao) sitashangaa iwapo wanaingia bungeni kwa kutoa milungula.

Nitatoa mfano sawa na ule wa CCM wa Julai mwaka jana wakati mchakato wa uchaguzi uliokuwa ukiendelea. 

Kura za maoni, nafasi ya ubunge kwa Chadema zilikuwa zimekamilika mkoani Mbeya. Baadhi ya wanachama walilalamika wakidai kuwa kulikuwapo matumizi ya rushwa katika kura hizo za maoni, kwa baadhi ya wagombea katika juhudi zao za kushawishi wateuliwe kugombea nafasi hiyo ya ubunge kupitia chama hicho.

Mgombea mmoja aliyeshindwa katika kura za maoni, jimbo la Mbeya Mjini alilalamika kuwa dalili zote zinaonesha kulikuwa na matumizi ya rushwa kwenye mchakato wote.

“Tunailalamikia CCM kuhusu rushwa, lakini hata huku ni yale yale, Katibu Mkuu anakiangalia chama kwa ngazi ya juu, huku chini kuna udhaifu sana, hakuna maadili,” alilalamika mgombea huyo wa Chadema.

Lisemwaalo lipo, hata kama viongozi wa upinzani nao watasema “hatuna taarifa.” Ndiyo maana tunaona inapokuja kudai nyongeza za posho, marupurupu, mafao na mishahara ya wabunge, wanasahau itikadi zao na kudai kwa sauti moja- ukiachia wachache.

Inasemekana kila mheshimiwa hulipwa si chini ya Sh milioni 7 kwa mwezi. Halafu kuna mafao ya Sh milioni 238 baada ya Bunge kuvunjwa. Mara ya mwisho walipa kodi wa Tanzania walikamuliwa Sh bilioni 85 ili kuwalipa wabunge mafao yao.

Bado haziwatoshi, na ndiyo maana tunasikia wakidai hongo wanapotembelea mashirika ya Serikali na halmashauri.