Vijana wawili raia wa Ubelgiji wameshtakiwa jijini Nairobi baada ya kukutwa na maelfu ya siafu, katika kile ambacho Kenya inasema ni sehemu ya mbinu ya usafirishaji haramu wa spishi ndogo zaidi na zisizojulikana sana.

Vijana hao, Lornoy David na Seppe Lodewijckx, wenye umri wa miaka 19, walikamatwa Aprili 5 katika kaunti ya Nakuru wakiwa na siafu 5,000 waliowahifadhi kwenye mirija ya maabara, wakidai walikuwa wanazikusanya kwa burudani bila kujua kuwa ni kinyume cha sheria.

Na katika kesi nyingine tofauti, Mkenya Dennis Ng’ang’a na Mvietnam Duh Hung Nguyen, pia walifikishwa mahakamani kwa mashtaka sawa baada ya kukamatwa na siafu 400.

Shirika la huduma za wanyamapori la Kenya, KWS linasema washukiwa walihusika katika biashara ya kusafirisha siafu hao kwenda Ulaya na Asia, hali inayoonyesha mabadiliko ya biashara haramu kutoka kwa wanyama wakubwa hadi viumbe wadogo muhimu kiikolojia.

Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa usafirishaji huo haramu unakiuka haki za nchi juu ya bayoanuai yake na kuhatarisha faida za kiuchumi na kimazingira kwa jamii za wenyeji.