Kituo cha Televisheni cha Palestina kimesema waandishi wa habari watano kutoka kituo hicho wameuawa katika shambulizi la Israeli katika Ukanda wa Gaza katikati.

Walikuwa katika gari la Quds Today lililokuwa limeegeshwa nje ya hospitali ya al-Awda, ambapo mke wa mmoja wa waandishi alikuwa katika pilka pilka za kujifungua, katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.

Kituo hicho kilichapisha video iliyoonyesha gari lililokuwa likichomeka lenye maandishi ‘press’ kwenye milango ya nyuma.

Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF) vimesema vililenga “watekelezaji wa Islamic Jihad waliokuwa wakijifanya waandishi wa habari” na kwamba hatua zilichukuliwa ili kuepuka kuumiza raia.

Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) imesema ilikuwa ‘imevunjika moyo’ na taarifa hizo. “Waandishi wa habari ni raia na lazima walindwe kila wakati,” ilisema CPJ.

Kituo hicho kinakadiriwa kupokea ufadhili kutoka kwa kundi hilo.

Jeshi la Israeli lilitaja majina ya waandishi watano waliouawa kama Ibrahim Jamal Ibrahim Al-Sheikh Ali; Faisal Abdallah Muhammad Abu Qamsan; Mohammed Ayad Khamis al-Ladaa; Ayman Nihad Abd Alrahman Jadi; na Fadi Ihab Muhammad Ramadan Hassouna. Walidai ‘habari kutoka vyanzo vingi vilithibitisha’ kwamba wote walikuwa watekelezaji wa PIJ.

Kufikia Desemba 20, angalau waandishi wa habari 133 wa Palestina walikuwa wameuawa tangu vita vilipoanza, na CPJ inasema kwamba vita hivi vimekuwa janga kubwa zaidi kwa waandishi wa habari.