MWANZA
NA MWANDISHI WETU
Mahakama ya Mkoa wa Mwanza imetupilia mbali kesi dhidi ya waandishi wa habari, Christopher Gamaina (Gazeti la Raia Mwema) na George Ramadhani (kujitegemea) waliotuhumiwa kujifanya maofisa wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Nchi za Ukanda wa Joto (TPRI).
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Bahati Chitepo, amewaachia huru wanahabari hao mwishoni mwa wiki iliyopita, akisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka/Jamhuri ulishindwa kuthibitisha shitaka hilo.
“Kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri kushindwa kubainisha bayana kutendeka kwa kosa, nimeona washitakiwa hawana kesi ya kujibu, hivyo kuanzia sasa wako huru,” alisema Hakimu Chitepo.
Aliongeza kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ni wazi kwamba mamlaka zinazohusika (TPRI na Jeshi la Polisi) zilipaswa kuwapongeza wanahabari hao kwa kusaidia kufichua maovu na siyo kuwafungulia kesi ya jinai.
“Baada ya kupitia maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka nimebaini kuwa waliopaswa kukamatwa na kushitakiwa ni wamiliki wa duka la pembejeo za kilimo na mifugo ambao walibainika kuuza viuatilifu ambavyo havijasajiliwa hapa nchini. Lakini badala yake wakakamatwa waandishi wa habari waliosaidia kufichua hujuma hizo,” amesema hakimu huyo.
Amesema shahidi wa kwanza, Richard Dunstan ambaye ni Mkaguzi wa TPRI Kanda ya Ziwa alikiri katika ushahidi wake kwamba alipigiwa simu na mmiliki wa duka la pembejeo liitwalo Mtasima Agro Vet lililopo Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza akimfahamisha kuhusu watu waliofika dukani hapo kuhoji uwepo wa viuatilifu haramu.
Dunstan aliieleza Mahakama kwamba baada ya kufika dukani hapo aliwakuta watu hao (Gamaina na Ramadhani) ambao walijitambulisha kwake kwamba ni waandishi wa habari, wakamwonesha vitambulisho vyao na kumwambia wana taarifa kuwa duka hilo linauza viuatilifu ambavyo havijasajiliwa TPRI.
Kwa mujibu wa Hakimu Chitepo, ofisa huyo wa TPRI aliieleza Mahakama kwamba baada ya kufanya ukaguzi ndani ya duka hilo, kweli alibaini kuwapo kwa viuatilifu ambavyo havijasajiliwa nchini na kisha kuwashukuru wanahabari hao kwa uzalendo wao wa kusaidia kufichua uovu huo.
“Ninavyofahamu mimi waandishi wa habari wana mbinu nyingi za kutafuta habari, hasa habari za uchunguzi, wanaweza kujiweka bayana au kuficha utambulisho wao.
“Hata hivyo, shahidi wa kwanza ambaye ni ofisa wa TPRI alisema walijitambulisha kwake kama waandishi wa habari na vitambulisho wakamwonyesha, sasa sielewi ni kwanini walikamatwa wanahabari na si yule aliyekutwa na viuatilifu haramu. Lakini nisingependa kuingilia mamlaka nyingine, kila mtu anabeba msalaba wake,” amesema hakimu huyo.
Hakimu Chitepo amesema waandishi wa habari kupitia kalamu zao ni wadau muhimu katika kuisaidia Serikali kufichua maovu miongoni mwa jamii.
Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Sophia ulidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa walitenda kosa la kujifanya maofisa wa TPRI Juni 26, 2018.
Katika kesi hiyo namba 207, waandishi hao wa habari walitetewa na Wakili Edwin Hans kwa hisani ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Akizungumza nje ya Mahakama baada ya uamuzi wa kuwachia huru wanahabari hao, Wakili Hans amesema: “Mahakama imetenda haki, hata mimi ningetoa uamuzi kama huo maana mashahidi wanne walisema Gamaina na Ramadhani walijitambulisha kama waandishi, ila huyo wa mwisho, Inspekta wa Polisi, Paschal Mboya alikwenda kuidanganya Mahakama tu.”
Naye, Gamaina, ameipongeza mahahakama hiyo akisema imetoa uamuzi uliotamalaki haki.
“Mahakama imetenda haki maana kesi hiyo tulibambikwa na polisi ili kutuzima tusifichue uovu wa kuuza viuatilifu haramu. Watendaji wa Serikali wamsaidie Rais Dk. John Magufuli kwa kuwatendea haki wananchi wema, siyo kuwaonea na kuwabambika kesi,” amesema Gamaina.
.tamati…