Wiki iliyopita yametokea matukio mawili makubwa. Wanahabari tumeadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari. Siku hii inaadhimishwa kimataifa na kitaifa imeadhimishwa jijini Mwanza. Kaulimbiu ya siku ya mwaka huu imekuwa ni Fikra Yakinifu, Jukumu la Vyombo vya Habari katika Kudumisha Amani, Usawa na Jamii Jumuishi.
Katika maadhimisho haya zilitawala hoja kuu tatu. Usalama wa wanahabari, weledi kwa waandishi dhidi ya teknolojia inayokua na ugumu wa uchumi kwa vyombo vya habari. Mkurugenzi wa Wakufu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura ameeleza changamoto zilizopo na fursa inayopatikana kupitia mitandao ya kijamii kwa vyombo vya habari.
Suala la wanahabari kujielimisha limejitokeza mara kadhaa na wengi wakakumbushwa matakwa ya kisheria yanayomtaka mwanahabari kuwa amepata angalau elimu ya diploma ifikapo mwaka 2021. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe wakati anawasilisha hotuba yake ya bajeti amesema asilimia 90 ya watangazaji hawana elimu stahiki.
Vyombo vya habari vingi vinajiendesha kwa shida kiuchumi. Kaulimbiu ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ya mwaka huu niliyoitaja hapo juu; “Fikra Yakinifu, Jukumu la Vyombo vya Habari katika Kudumisha Amani, Usawa na Jamii Jumuishi” imesheheni ujumbe mzito ndani yake. Inaeleza kuwa hizi ni nyakati zenye changamoto ya kipekee.
Sitanii, hili la changamoto zinazovikabili vyombo vya habari nitalirejea baadaye, ila nigusie hili nililolikuta hapa Bukoba. Kuna mlipuko wa malaria. Katika kata moja ya Nyanga, kuna watu wasiopungua 92 wamekwenda kutibiwa ugonjwa huu katika zahanati ya Kashenge. Familia nyingi ukipita unakuta watu wanaumwa. Familia moja unakuta ina wagonjwa watatu hadi watano.
Nimetembelea watu mbalimbali nyakati za jioni. Kuna mbu wa kutisha. Kiwango cha mbu kilichopo katika Kata ya Nyanga, kinaashirika hatari ya mlipuko wa malaria unaoweza kuzaa vifo vya kutisha. Nililolishuhudia naomba Serikali iingilie kati tatizo la mbu Bukoba. Ikiwezekana dawa ya ukoko ipuliziwe upya kuokoa maisha ya watu.
Sitanii, baada ya kugusia hili tatizo la mbu nililolikuta hapa Bukoba, sasa naomba kurejea kwenye hoja ya elimu kwa wanahabari. Nimeangalia katika mitandao ya kijamii wengi wanamshambulia Dk. Mwakyembe kwa kauli yake kuwa asilimia 90 ya wanahabari hawana sifa za kufanya kazi ya uandishi wa habari kielimu.
Ni ukweli ulio wazi kuwa radio nyingi na baadhi ya magazeti watumishi wake hawana sifa za kitaaluma. Tumekuwa na ma-DJ walioingia kwenye vyombo vya habari na kuanza kuwa watangazaji. Yapo matangazo mengi ya kimazoea ambayo ukiyasikiliza unapata kichefuchefu. Radio nyingi na televisheni huoni ubunifu wa aina yoyote.
Sungura mara kadhaa ameahamasisha habari za uchunguzi. Habari za uchunguzi zinahusisha kusoma maandiko ya kitaaluma. Yapo maeneo ambayo unahitaji kusoma mikataba iliyoandikwa na wataalam waliobobea. Ni katika misingi hiyo waandishi wanahitaji kuwa na kiwango cha elimu kizuri kwani kipaji pekee hakifanyi kazi kwa sasa.
Alichosema Dk. Mwakyembe tukichukue kwa moyo wa bashasha. Nashukuru wapo waandishi kadhaa mwaka jana nilipoanzisha kampeni ya waandishi kwenda shule, pamoja na wale wachache walionitukana, lakini zaidi ya waandishi 10 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma waliamua kwenda shule. Asanteni sana kwa kukubali ushauri wangu.
Sitanii, dunia ya leo tunahitaji fikra yakinifu. Tunahitaji kuhamasisha wanahabari wetu wengi kwenda shule na kwa kufanya hivyo nchi yetu itajikuta inao wanahabari wenye weledi wa kutosha. Nchi kama Uganda waliishakuwa na sheria hii kitambo. Kiwango cha uandishi wa habari Uganda kiko juu kuliko nchi zote zinazowazunguka katika ukanda wetu.
Ni kwa mantiki hiyo nasema suala la elimu kwa wanahabari sisi waandishi tujitathimini. Changamoto za kiuchumi zinazotukabili kwenye vyombo vya habari, mabadiliko ya kiteknolojia kupitia mitandao ya kijamii na mengine mengi yanawafanya wanahabari kulazimika kuongeza kiwango cha elimu kwa nia njema ya utumishi bora kwa vyombo vya habari Tanzania. Waandishi twende shule. Mungu ibariki Tanzania. Kutokana na makala hii kuandaliwa mapema, naomba kuchukua fursa hii kutumia angalau haya moja kutoa pole kwa Watanzania, wazazi, walezi ndugu na jamaa wa wanafunzi 32, Walimu wawili na Dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha waliofariki kwa ajali ya basi Mei 6, 2017. Nipo huku mkoani, nimeumia mno na Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi. Amina.