Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
BODI ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), imeandaa mkutano wa waandishi na wachapishaji wa vitabu kuhusu Sheria ya amana kwenye maktaba mtandao wa taifa na ununuzi wa vitabu kwa ukuzaji wa soko la ndani utakaofanyika kesho.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya (TLSB), Profesa Rwekaza Mukandara.
Mkurugenzi Mkuu wa (TLSB), Dk. Mboni Ruzegea, alisema jana kuwa mkutano huo utafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TLSB Maktaba Kuu ya Taifa na kwamba lengo ni kujadili kwa pamoja utekelezaji wa sheria ya amana katika mfumo wa maktaba mtandao wa taifa na ununuzi wa vitabu kutoka kwa waandishi na wachapishaji wa ndani.
Alisema TLSB iliyoanzishwa kwa Sheria ya mwaka 1975 inawapa mamlaka ya kuendeleza masuala ya maktaba kwa kuhakikisha nchi inakuwa na vitabu vya kutosha kupitia maktaba.
“Mkutano huu wa kesho unalenga tunachofanya kila siku kwa hiyo tunataka kuzungumza na wachapishaji na wazalishaji kuhusu ubora wa wanachozalisha ili kiweze kuingia kwenye maktaba zetu,” alisema
Alisema mchapishaji au mwandishi binafsi, kampuni au taasisi kisheria lazima awasilishe nakala ya kitabu chake maktaba kuu ya taifa ili kiwekwe kama urithi kwa kizazi kijacho.
Alisema kumekuwa na mapinduzi ya kiteknolojia kwenye maktaba na bodi ina mfumo wa maktaba jumuishi ya kitaifa itakayozinduliwa hivi karibuni ambapo TLSB itakuwa na uwezo mkubwa wa kubadilishana taarifa rasilimali na mtandao wa maktaba zetu.
Tuko mikoa 22 na maktaba zote ziko 43 na bado tuna maktaba jamiii tunamtandao mkubwa na unaendelea kutanuka na maktaba mtandao itarahisisha wananchi wengi kupata huduma zetu,”
“Zamani mtu alikuja na vitabu vinapokelewa vinasajiliwa lakini sasa vinaletwa kwa mtandao, wachapishaji wote wataleta kwa mtandao kwa hiyo itawawezesha wananchi wengi wanapata huduma za maktaba popote walipo,” alisema
“Vitabu vyao vitajulikana na kusomwa kmataifa na hiyo haimaanishi kuwa haki zao za miliki zitakiukwa hapana. Haki zao za umiliki zitazingatiwa haziwezi kupotea kwasababu kuna mfumo wa kulinda haki za wabunifu,” alisema