Wandamanaji nchini Kenya wameapa kuendelea na maandamano yao kupinga nyongeza mpya za ushuru, siku moja tu baada ya polisi kufyatua risasi na kuwaua takriban watu watano.

Watu wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa pia walipovamia majengo ya bunge. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amesikitishwa na ripoti za mauaji na majeruhi katika purukushani hiyo ya kupinga mswada huo tete wa fedha wa mwaka 2024.

Ameitaka serikali kuwa na uvumilivu kwa watu wake na kuwaruhusu kuandamana kwa amani.

Wafuasi wa vuguvugu la maandamano yaliyopewa jina la “siku saba za hasira” wametumia mitandao ya kijamii kuelezea dhamira yao ya kurudi tena barabarani siku ya Alhamisi.

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, wametumia hashtag ya Tukutane Alhamisi.

Rais wa Kenya aapa kuchukua hatua kali dhidi ya maandamano ya vurugu

Jana jioni, Rais William Ruto alilihutubia taifa na kusema matukio ya vurugu yakiwemo waaandamanaji kuvunja ua la bunge na kuingia ndani na kusababisha uharibifu mkubwa, ni kitendo cha uhaini.

Kwa sasa bunge la Kenya limeidhinisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kulisaidia Jeshi la Polisi kutoa ulinzi kufuatia maandamano ya kupinga muswada wa Fedha kote nchini.