Soka la Tanzania linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo tatizo la waamuzi ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau na wanachama wa klabu zinazoshiriki Ligi kuu ya Tanzania Bara.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti mara baada ya kuhitimu mafunzo ya muda mfupi ya waamuzi yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kwa ushirikiano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baadhi ya waamuzi na wakufunzi wameonekana kusikitika kutokana na lawama zinazoelekezwa kwao.

Wanasema waamuzi ni wanadamu ambao wamekuwa wanafanya makosa ya kibinadamu, huku wakirusha lawama kwa mashinikizo kutoka kwa watu wanaotaka timu zao zishinde.

Mmoja wa wahitimu wa kozi hiyo, Jonesia Rukyaa, anasema umefika wakati kwa familia ya wapenda soka kuweka imani kwa waamuzi wa ndani kuliko kuwatupia lawama kila kukicha.

“Waamuzi wa Kitanzania tunapitia wakati mgumu kuliko kipindi chote katika miaka ya hivi karibuni, hali inayotufanya kupoteza kujiamini,” anasema Rukyaa.

Anasema haiwezekani kila mechi waamuzi wakawa wabovu, haiwezekani kila mwamuzi anayeboronga awe amenunuliwa, haiwezekani kila mwamuzi anapokosea atakuwa na mapenzi binafsi dhidi ya timu nyingine.

Anasema waamuzi wanaweza kuwa na matatizo, lakini shabiki hapaswi kumpiga mwamuzi hivyo pamoja na mambo mengine yamekuwa yakichangia kuporomosha kujiamini kwa waamuzi wengi katika ligi za ndani.

Mmoja wa wakufunzi wa kozi hiyo, Israel Mkongo, anasema lengo la kozi hiyo ni kutaka kuhakikisha waamuzi wanaondokana na lawama za kila kukicha zinazoelekezwa kwao.

“Mchezo wa soka ni sayansi inayobadilika kila kukicha, hali inayotusukuma kuwanoa waamuzi wetu kila baaada ya miezi mitatu, hii ndiyo dawa ya kuwafanya waendane na kasi ya mchezo kila siku,” anasema Mkongo.

Naye, Soud Abdul, mmoja wa wakufunzi katika kozi hiyo, anasema viongozi ndani ya klabu pamoja na wapenzi na wanachama ndani ya klabu hizo lazima wajue kuwa soka limebadilika na kuachana na kasumba za Uyanga na Usimba.

“Miaka ya nyuma ilikuwa ni nadra sana kukuta klabu kama Yanga au Simba ikifungwa na klabu ndogo kama Stand United, lakini leo soka limebadilika ushindani unapatikana kila mahala kwa hiyo ni lazima wakubali wanaposhindwa kuliko kuwalaumu waamuzi,” anasema Abdul.

Kozi hiyo ilijumuisha waamuzi 40 kati ya hao waamuzi wenye beji ya FIFA walikuwa 18 na wengine 22 ni waamuzi wa madaraja ya chini.