Ikiwa ni mwezi wa tano sasa vijana 300 walioajiriwa katika Idara ya Uhamiaji wakiwa hawajalipwa mishahara, imebainika kuwa chanzo ni kutopewa barua zao za ajira.
Rais John Magufuli, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Ikulu, Dar es Salaam wiki iliyopita, alisema askari polisi na wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama walioajiriwa hivi karibuni wamekuwa wakilipwa mishahara.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI na kuthibitishwa na maofisa kadhaa wa Idara ya Uhamiaji, umebaini kuwa ama Rais amedanganywa, au kuna uzembe unaofanywa katika ofisi husika katika kuwalipa mishahara watumishi hao wapya walioajiriwa Juni, mwaka huu.
“Watalipwaje mishahara ilhali hadi sasa hawana barua za ajira?” Kimehoji chanzo chetu.
Wiki iliyopita, vijana hao mkoani Dar es Salaam waliahidiwa na wakuu wao wa Idara kuwa wangelipwa mishahara kuanzia wiki hiyo, lakini baadaye zikapatikana taarifa kuwa hata barua za ajira hawajapewa.
Vijana hao walisema wamekuwa wakiishi kwa kuombaomba kwa kipindi chote – kuanzia Juni. Walisema wakati wao wakiendelea kuteseka, wenzao ambao ni polisi – waliofuzu wakati mmoja chuoni Moshi – walianza kulipwa mishahara Septemba, mwaka huu.
“Tunapata shida kweli kweli, hatuna namna ya kuishi, tumekopa hadi tumefikia hatua ya kukwama kabisa.
“Tunatakiwa twende kazini, tunahitaji nauli, fikiria kwa miezi minne, sasa tunaanza mwezi wa tano tukiwa hatuna mishahara. Maisha yamekuwa magumu mno.
“Kama ni suala la uhakiki, mbona wenzetu polisi wameshaanza kulipwa? Tunaamini kuna uzembe katika kulipatia ufumbuzi suala letu,” imesema sehemu ya taarifa ya maandishi ya vijana hao walioileta JAMHURI.
Wameongeza: “Tunamuomba Mheshimiwa Rais aone namna ya kutusaidia kwa sababu wakati mwingine inawezekana hatulipwi kwa sababu wapo wanaotumia kisingizio cha ‘uhakiki’ kutufanya tuendelee kutaabika.”
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Meja Jenerali Jaji Projest Rwegasira, akiri kuwapo kwa madai ya watumishi hao.
Amesema ofisi yake ilishapeleka orodha yao Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Meja Jenerali Rwegasira alikiri kuwapo ucheleweshwaji aliouita ‘mdogo’ kwenye suala hilo la malipo, na kuahidi kuwa litashughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Alisema ameshazungumza na Kaimu Kamishna wa Uhamiaji nchini, Lilian Lembeli, ambaye amemhakikishia kuwa ofisi yake inawasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kumaliza tatizo hilo.
Waziri katika ofisi hiyo, Angela Kairuki, hakuweza kupatikana kupitia simu yake.