Na Lookman Miraji,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kila Julai 18 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ikiwa ni kuenzi ya aliyoyafanya katika jamii ya Waafrika Kusini, Waafrika na Dunia kwa ujumla.

Kupitia kikao cha Jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN) Novemba ya mwaka 2009 , Jumuiya ya Umoja wa Mataifa kupitia katibu mkuu wake kiliitangaza rasmi siku ya Julai 18 kuwa siku kuu ya Kimataifa ya Nelson Mandela ikiwa ni katika kuthamini mchango alioutoa katika jamii ya Waafrika Kusini hususani katika kupambana dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi uliokuwa umekithiri nchini humo.

Nelson Rolihlahla Mandela alikuwa ni Rais wa Kwanza mweusi wa taifa la Afrika Kusini mara baada ya kupata uhuru wake kutoka katika mikono ya wakoloni.

Nelson Mandela aliliongoza taifa la Afrika Kusini katika miaka ya kuanzia 1994 mpaka mwaka 1999.

Shughuli za maadhimisho ya siku hiyo ya Kimataifa ziliadhimishwa Mikocheni Dar es Salaam.

Hafla ya shughuli hizo zilienda sambamba hamasa ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kusaidia watoto wenye changamoto mbalimbali za kibinadamu cha Victoria kinachotarajiwa kujengwa hivi karibuni huko mjini bagamoyo.

Akizungumza hapo wakati wa hafla hiyo Balozi wa Afrika Kusini nchini; Noluthando Malepe amesema kuwa jukumu la kusaidia watu ni la kila mmoja katika jamii endapo ataona kuna watu wanahitaji msaada.

”Kila siku tuifanye kuwa siku ya Mandela, tufanye jambo katika jamii zetu, majirani zetu na hata wafanyakazi wenzetu ambao tutaona wana matatizo hivyo bado kuna nafasi kubwa kwetu kusaidia wengine” amesema Balozi Noluthando.

Aidha Balozi Noluthando ameiomba jamii kuiga mfano wa kituo cha Victorious Centre ambacho hutoa msaada kwa watoto wenye mahitaji maalum na wale waliokumbwa na changamoto ya ugonjwa wa usonji.

”Watu wanatakiwa kufanya kila liwezekanalo kusaidia wasiokuwa na uwezo kwani wengi wa vijana wetu wanaishi katika umasikini, wanahitaji msaada. Hivyo tunatakiwa kufanya jambo kama kituo cha Victorious hapa ambao wanawasaidia watoto wenye usonji pamoja na watoto wasioeleweka na jamii” ameongeza hayo Balozi Noluthando.

Kwa upande mwingine pia shughuli hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka katika mashirika ya kiserikali na binafsi ambapo pia zilihudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu Dkt; Fredrick Sumaye ambae pia alikuwa miongoni mwa waalikwa katika maadhimisho hayo.

Akizungumza mara baada ya shughuli hizo Sumaye ameielezea siku hiyo pamoja na kumuelezea kwa ufupi Hayati Nelson Mandela kama mtu mwenye mchango mkubwa katika mapinduzi ya bara la Afrika.

Sumaye pia amemuelezea Hayati Mandela kama mtu ambaye alikuwa anakumbuka sana watu waliokuwa pamoja na yeye katika ukombozi wa bara la Afrika na katika kupambana na siasa ya Ubaguzi wa rangi nchini Afrika kusini.

”Mandela hakuwa kiongozi wa Afrika tu, alikuwa kiongozi wa dunia nzima. Alikuwa ni mtu wa tofauti sana ukiachilia mbali kupata shida zote wakati wa kufungwa na shida nyingine ambazo amepitia lakini alipofunguliwa tu alisema kuwa tusilipize kisasi na tuwe kitu kimoja.

“Lakini ni mtu ambaye anakumbuka sana watu waliokuwa pamoja nae yeye na watu wa Afrika kusini katika ukombozi wa bara la Afrika na katika mapambano dhidi ya Ubaguzi wa rangi nchini Afrika kusini na ndio maana utaona alipokuwa Rais tu alikuja Tanzania kama nchi yake ya kwanza , kwa hiyo zaidi ya Mandela alivyokuwa lakini pia alikuwa ni mtu anayekumbuka fadhila kwa wale watu walioisaidia Afrika kusini.” amesea Waziri.

Sumaye pia ameongeza kuwa siku hiyo ya Mandela kuwa imeunganishwa na tukio hilo maalum kwa watoto wenye changamoto ya ugonjwa wa Usonji kwa kukumbuka enzi za uhai wake Mandela hakutaka kuacha mtu mwingine nyuma na kuwaasa Watanzania kutowatenga watoto wenye changamoto ya Usonji ila kuwapeleka katika maeneo ambayo watasaidiwa.

”Kwa hiyo leo jambo hili la Usonji limeunganishwa na siku hii ya Mandela kwasababu Mandela hakutaka kuacha mtu mwingine nyuma. Sasa leo hii Siku ya Usonji shughuli iliyofanyika hapa maana yake na sisi kwa hii ya Mandela nasi tunakumbushwa kuwa moyo wa kupenda wale ambao hawakubahatika kama sisi, hawa wagonjwa tusiwaache tu nyumbani tuwapeleke kwenye maeneo ambayo watasaidiwa. Na ndio maana ya kituo hichi cha Victorious lengo lake ni hilo ili hawa watoto wenye hali ngumu waweze kuletwa na kusaidiwa ili wawe sawa na binadamu wengine.” amesema Sumaye.

Please follow and like us:
Pin Share