Na Mwandishi Wetu

Vyuo vikuu vikubwa 15 vya nchini Malaysia vinatarajia kufanya maonyesho hapa nchini kwa lengo la kuwaonyesha Watanazania fursa mbalimbali za kielimu zinazopatikana kwenye vyuo hivyo.

Maonyesho hayo yatafanyika kwenye hoteli ya Verde Zanzibar tarehe 28 mwezi huu na tarehe 31 yatafanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Kwa mujibu wa mratibu wa maonyesho hayo kwa hapa nchini, Abdulmalik Mollel, maonyesho hayo yanataratibiwa na Education Malaysia Global Services (EMGS) ambayo ni wakala wa serikali ya Malasyia.

Mollel amesema vyuo vikuu hivyo ndivyo vikuu bora nchini Malaysia hivyo wanafunzi wanaotarajia kupata matokeo yao ya kidato cha sita, wale waliopata matokeo yao na wale waliokwishapata matokeo yao ya astashahada ndio wakati wao wa kupiga simu na kutafuta fursa hiyo.

Mollel amesema hiyo ni fursa kwa watu wanaotaka kusoma cheti, Stashahada, Shahada za Uzamili na Shahada ya Uzamivu (PhD) nao wanapaswa kuchangamikia fursa hiyo adimu ya kukutana na vyuo hivyo.

Alisema vyuo vikuu vya hapa nchini ambavyo vinahitaji ushirikiano na vyuo viku nchini Malaysia vinapaswa kutumia fursa hiyo kutafutafuta maeneo ya uhusiano kwenye taaluma mbalimbali.

“Vyuo vikuu vinapaswa kuchangamkia fursa kulingana na uhusiano wanaouhitaji, je ni uhusiano kuhusu kozi za uhandisi, kozi za biashara, afya, exchange program za wanafunzi, je ni kuhusu kuendeleza wahadhiri? Hii ndiyo fursa yenyewe ya kuitumia,” amesema Mollel

Aidha, amesema ujio wa maonyesho hayo pia ni fursa kwa taasisi mbalimbali ambazo zingependa wafanyakazi wake kwenda kuongeza kiwango chao cha elimu nchini Malaysia kwenye fani mbalimbali katika kiwango cha Shahada ya kwanza, Shahada ya Uzamili, Shahada ya Uzamivu (PhD).

“Kuna watu wako kazini na wangependa kuongeza ujuzi na pengine wangependa kuongeza ujuzi wao nchini Malaysia sasa vyuo vikuu hivyo vitakuwa hapa kwa hiyo taasisi hizo ama ni za serikali au binafsi hii ndiyo fursa ya kuitumia,” amesema Mollel

“Inawezekana kukawa kuna taasisi binafsi na umma zenye fursa mbalimbali kama chuo cha aviation, ambao wanataka kukutana na wenye vyuo hivyo moja kwa wao waseme muda huu ili siku vitakapokuja waweze kutumia muda wao vizuri,” amesema

Amesema taasisi za fedha ambazo zimekuwa zikikopesha wanafunzi wa elimu ya juu Zanzibar na Tanzania Bara, NGos mbalimbali zinazosaidia wanafunzi wanatakiwa kujua kwamba huu ndio muda wao wa kuwasiliana na vyuo hivyo ili iwerahisi kukutana nao watakapowasili hapa nchini.

Mollel alisema kuna mawakala mbalimbali wa elimu ya juu nje ya nchi walioko hapa nchini na wale nchi za Zambia, Rwanda, Malawi, Burundi na Kenya wanapaswa kuja nchini kuzungumza na wawakilishi wa vyuo hivyo kwa tarehe watakazokuwa nchini.

“Kwa mfano maonyesho haya hayataanzia hapa Tanzania, yataanzia Kenya kwa hiyo mawakala wa Kenya wanaweza wakaenda moja kwa moja wakafanya booking ya kukutana nao na mawakala wa Tanzania wanaotaka kupeleka wanafunzi Malasyia tena kwenye vyuo ambavyo mwanafunzi anaweza kuanzisha Malaysia akamalizia Canada, au akaanzisha Malaysia akamalizia Marekani au Uingereza,” amesema

“Au vyuo vikuu hapa nchini ambavyo vinataka kuanzisha program za ushirikiano kwamba mwanafunzi anaweza kusomea Tanzania miaka flani na akasomea Malasyia miaka flani hizi ni miongoni mwa fursa ambazo vyuo vya Tanzania hazipaswi kuzikosa,” amesema

Amesema wakuu wa shule za sekondari wanapaswa kufanya mawasiliano ya namna wanavyoweza kukutana na wawakilishi wa vyuo hivyo kwani kutokana na wingi wa wanafunzi kuna uwezekano wengine wakakosa fursa ya kuonana na vyuo hivyo.