Kama kuna nchi yoyote yenye vyombo vingi vya umma, basi nchi hiyo ni Tanzania. Shabaha ya vyombo vyote hivyo ni kumtumikia binadamu au kutumikia umma wa Tanzania.

Lakini vyombo hivi vya umma vinasaidia umma? Na kama vinasaidia umma ni kwa kiasi gani? Kuna vyombo vya umma vilianzishwa na mkoloni.  Tukarithi tulipopata uhuru.

Tuna Serikali iliyoanzishwa na Wajerumani mwaka 1891. Tuna Jeshi la Polisi lililoanzishwa na Mwingereza mwaka 1916, makao makuu yake ya awali yalikuwa Lushoto.

Tuna Mahakama yaliyoanzishwa na Mwingereza mwaka 1921. Tuna vyama vya wafanyakazi. Chama cha kwanza cha wafanyakazi Tanganyika (Tanzania Bara) kilianzishwa Tanga mwaka 1922. Tuna vyama vya ushirika (vya wakulima), chama cha kwanza cha ushirika Tanganyika kilianzishwa Bukoba mwaka 1924.

Tuna Bunge ambalo chimbuko lake ni Baraza la Kutunga Sheria lililoanzishwa mwaka 1926. Tuna serikali za mitaa zilizoanzishwa mwaka 1927 kwa jina la ‘Tawala za Wenyeji’ mpaka zilipoitwa  Serikali za Mitaa mwaka 1950.

Tuna Jeshi la Magereza lililoanzishwa mwaka 1931, makao makuu yake ya awali yalikuwa Morogoro. Tuna redio ya umma iliyoanzishwa mwaka 1951 kwa jina la ‘Sauti ya Dar es Salaam.’ 

Utasema ni kitu kipi hatuna? Kila chombo tunacho, vyote vingetenda haki Tanzania isingekuwa na amani tu, ingekuwa peponi.

Kana kwamba vyombo hivyo havikutosha kuhudumia umma wa Tanzania, baada ya kupatikana uhuru tulianzisha vyombo vingine. Tuna Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililoanzishwa mwaka 1963. Jeshi la mgambo tuliloanzisha mwaka 1971.

Tuna Tume ya Haki za Binadamu tuliyoanzisha mwaka 2001 kutokana na Tume ya Kudumu ya Uchaguzi tuliyoanzisha mwaka 1966 ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na tume kama hiyo.

Mbali na vyombo hivyo vya umma, wananchi wameunda vyombo vingine vilivyoongeza idadi ya vyombo vya kuhudumia umma. Tuna Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichoanzishwa mwaka 1995. Tuna Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kilichoanzishwa mwaka 1994.

Tuna taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tuliyounda mwaka 1975. Tuna Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kilichoanzishwa mwaka 1987. Tuna Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA) kilichoanzishwa mwaka 1989.

Mbali na vyombo hivyo, kuna ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyoanzishwa mwaka 1992. Tuna Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoundwa upya mwaka 1993 baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi Tanzania, Mwenyekiti wake wa kwanza akiwa Jaji Lewis Makame, na kadhalika.

Ukweli ni kwamba karibu vyombo vyote hivyo vya umma na vya watu binafsi vinapigania haki. Lakini kila mtu analalamika kwamba nchi haina haki. Tunakosea wapi?

Nionavyo mimi, vyombo vingi havitendi haki kwa sababu si huru na vinatumikia umma wa Tanzania. Na hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi wa vyombo hivyo kulinda zaidi maslahi yao binafsi badala ya kulinda maslahi ya umma wa Tanzania.

Inakuwaje mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ipigwe marufuku nchi nzima na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikakaa kimya?

Inakuwaje Tume ya Uchaguzi inalalamikiwa kila uchaguzi kwamba inapora kura za upinzani ofisi ya Msajili wa Vyama isipiganie tume huru ya uchaguzi?

Inakuwaje Jeshi la Polisi liendelee kumwagia maji ya upupu na kuwapiga wananchi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ikakaa kimya?  

Kwa hiyo, tumeunda vyombo vingi vya kusimamia haki kwa lengo la kuudanganya ulimwengu.