Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedi, Dar

TASNIA ya habari inapaswa kuwa na sheria na kanuni rafiki ili kuruhusu kukua na kwamba, kuweka sheria kali na ngumu, kunaua vyombo vya habari lakini kunaacha athari hasi kwa taifa.

Hayo yamesemwa leo na Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Mwendapole,wakati akizungumza na Mhariri wa Raia Mwema, Joseph Kulangwa na Erasto Masalu, msimamizi wa kitengo cha Mwanahalisi Online wakati alipotembelea katika ofisi hizo na kukabidhi flash zenye mapendekezo ya mabadiliko ya sheria kwa wanahabari.

Joseph Mwendapole, Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri (TEF), aliyesimama akiwa katika chumba cha habari cha Mwanahalisi Digital alipokwenda kutembelea na kueleza mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari ulipofika

Amesema kuwa sheria za habari zinapaswa kuwa rafiki kwa mazingira ya ndani na nje ya nchi kuliko kuwa na sheria mbazo ni kali na utekelezaji wake unakuwa ni mgumu.

“Hatupaswi kujifungia, tunapaswa kuwa na sheria zinazokubalika ndani na nje ya nchi.Tunawezaje kutengeneza sheria za vyombo vya habari ambazo baadaye mwenyewe uliyeshiriki kutengeneza unaanza kuomba toba.

“Tofauti na nyuma kidogo, kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.

Mwendapole ameongeza kuwa mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana wadau wa habari wanasema uhuru wa habari ni lazima ulindwe kisheria.

Ameeleza kuwa, mchakato wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini, unalenga kujenga mazingira rafiki na bora kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Vyombo vya habari vinahitaji sheria rafiki zinazolenga kuimarisha mazingira ya utendaji, kutunga sheria ngumu na kandamizi,huchangia kuua ustawi wa vyombo vya habari,” amesema.

Amesema, baadhi ya sheria zinazotumika kuongoza tasnia ya habari zilizotungwa mwaka 2016, zinaumiza waandishi pamoja na vyombo wanavyofanyia kazi.

“Kabla ya Nape (Waziri Nape Nnauye) kufungulia magazeti ya kampuni hii, kwa mfano gazeti la MwanaHalisi lilishinda kesi mahakamani lakini pia lilimaliza muda wa kifungo chake, pamoja na yote hayo walipoomba leseni, hawakupewa.

“Hapa yametumika mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari Maelezo aliyopewa kisheria kugoma kutoa leseni kutokana na namna anavyojisikia, haya ndio miongoni mwa mambo tunayopigania yaondolewe,” amesema Mwendapole.

Hata hivyo Mwendapole ameushukuru uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu na kuagiza wadau wa habari kukutana ili kupitia sheria zilizopo kwa lengo la kuimarisha tasnia ya habari nchini.