Vyombo vya habari (mass media) ni njia ya mawasiliano kati ya mtu na mtu, katika kuhabarishana, kuelimishana na kuburudishana. Iwe wakati wa kazi, mapumziko au starehe. Ni njia ya kufikia kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika taifa lolote duniani.
Kila chombo (medium) kinafanya kazi kwa maadili ya kazi, kanuni na weledi. Kushirikiana na kingine katika kupokea na kutoa taarifa mbalimbali katika mustakabali wa maendeleo ya mtu au jamii.
Redio, magazeti, runinga, filamu, video, vitabu, majarida, simu, teleksi na mitandao ya kijamii ni vyombo vya habari. Vyombo vyote hivi vinafanya kazi chini ya miundo, sera na taratibu za utekelezaji wa masuala ya habari katika kutimiza madhumuni na malengo ya mamlaka zinazoendesha vyombo hivi.
Ukiangalia utendaji kazi wa vyombo hivi, utaona ni njia ya kupitisha au kusafirisha mawazo, fikra au ujumbe kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili. Ni lazima vipitishe ujumbe unaokusudiwa. Ni matarajio ya mtumaji na mpokeaji habari, elimu na burudani kujenga uhusiano mwema.
Hapa ndipo penye uangalifu, ni aina gani ya ujumbe unatumwa na unapokelewa kati ya mtu na mtu. Ama sivyo vyombo hivi vitatumika kwa madhumuni na malengo mabaya badala ya mazuri.
Kitendo cha usafirishaji au upashanaji habari, fikra, rai kwa njia mbalimbali zikiwamo za vyombo vya habari ndiyo mawasiliano yenyewe. Mawasiliano yapo ya mtu na mtu, jamii na jamii na taifa na taifa.
Vyombo hivi ili viwe na sifa ya kupasha habari havina budi kuwafikia watu wengi sana kwa wakati mmoja. Watu wengi sana katika istilahi ya habari ndiyo umma (hadhira). Ndipo vinapokuwa vyombo vya mawasiliano na umma. Katika mazingira haya vyombo hivi vitumike kwa umakini.
Katika lugha rahisi na fupi kutamka tunasema vyombo vya habari, kwa lugha ya Kiingereza ni ‘Mass Media’, vyombo hivi vina uwezo na sifa za msingi kuwafikia watu wengi sana, katika sehemu mbalimbali na katika mazingira tofauti. Vilevile haraka sana na kwa wakati mmoja.
Kwa sifa hizi, baadhi ya watumiaji (wasikilizaji na wasomaji wa habari) wanatumia vibaya vyombo vya habari: kwa maana ya kinyume cha malengo na madhumuni ya kuwapo kwa vyombo hivi. Wanavitumia katika kujenga chuki, fitina, kejeli, dharau na kadhalika.
Wakati mwingine bila hadhari, tafakuri na uelewa wa taarifa, nao baadhi ya waandishi, watangazaji na wasimamizi wa matangazo wanajikuta wametumbukia katika malumbano ya kisiasa na kijamii kupinga au kukubali ujumbe unaopita katika vyombo vyao.
Kushiriki kwao katika malumbano hujenga taswira kwa umma kuona na kuamini matangazo ya malumbano ya kejeli au dharau ni moja ya sifa na adilifu ya vyombo vya habari. Jambo ambalo si kweli na si sahihi. Ni vema tukajitoa katika hili na kuweka umma katika mazingira salama.
Hekima na busara iliyoje kwa viongozi, umma na wanahabari wote nchini kuacha kutumia tabia ya kutafuta malumbano ya uhasama badala ya malumbano ya amani na usalama. Tukumbuke kila mchuma janga hula na wa kwao. Wa kwao wenyewe ndio Watanzania, tutaangamia.
Vyombo vya habari si ukumbi wa mipasho, si jukwaa la visanga na si kambi ya mafunzo ya vita. Vyombo vya habari ni mlango wa maarifa, ni chuo cha mafanikio na ni bahari ya amani na usalama. Mungu ibariki Tanzania, tubariki watoto wa Tanzania.