*Upuuzi, uhuni vyafanywa katika mitaa
*Kisingizio cha gesi chatumika kufanya uasi
*Nyumba ya Waziri, CCM, umma zateketezwa
Vifo vya watu kadhaa vimeripotiwa kutokea mkoani Mtwara vikisababishwa na vurugu za wananchi walioamua kuchoma mali za watu binafsi, umma na taasisi mbalimbali.
Askari wanne wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki dunia katika ajali iliyotokea eneo la Kilimahewa, Nachingwea. Walikuwa wakielekea Mtwara kuongeza nguvu ili kudhibiti vurugu zilizoibuka.
Wanajeshi wengine zaidi ya 21 waliokuwamo kwenye gari lililopata ajali, walijeruhiwa. Pia mwananchi mmoja amefariki dunia mjini Mtwara.
Miongoni mwa mali zilizochomwa moto na kundi linalotajwa kuwa ni la wahuni wapenda vurugu ni nyumba ya Waziri, magari ya Serikali pamoja na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mtwara.
Chanzo cha vurugu hizo kimeelezwa kwamba ni msimamo wa wananchi wanaopinga ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam. Vurugu za jana zilianza baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuhitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 bila “kukata kiu” ya wananchi hao ya kusitishwa kwa mradi huo.
Hadi JAMHURI inakwenda mitamboni, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara ilithibitisha kupokewa kwa maiti ya mtu mmoja.
Miongoni mwa majengo yaliyochomwa moto ni nyumba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)), Hawa Ghasia, ofisi ya CCM Saba Saba na nyumba ya mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Jengo jingine lililotajwa kuchomwa moto ni la hoteli ya Shengena inayoaminika kwamba ndimo walimofikia askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).
“Nyumba kadhaa za watumishi wa Serikali zimechomwa maeneo ya Shangani,” alisema mmoja wa wananchi walioshuhudia.
Kulikuwa na habari kwamba wananchi kadhaa waliojiandaa kufanya vurugu walitumia baruti kulipua majengo na kuwashambulia polisi.
Vurugu hizo zilisababisha kufungwa kwa shughuli zote za kijamii mjini Mtwara. Magari pekee yaliyoonekana barabarani ni ya polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Barabara nyingi zilifungwa na wananchi kwa kutumia magogo na mawe.
“Hali si nzuri huku Mtwara, kwa ufupi hali ni tete na hakuna amani, mabomu ya machozi yanarushwa, huduma zote za kijamii zimefunngwa, hakuna usafiri, masoko, maduka na baa zote zimefungwa, daladala, teksi na bodaboda hazifanyi kazi. Kwa ujumla kinachoendelea ni mapambano makali kati ya Jeshi la Polisi na wananchi,” amesema mwananchi mmoja.
Pia kulikuwa na habari kwamba daraja la Mikindani lilivunjwa na hivyo kukata mawasiliano kati ya Mtwara na maeneo mengine.
Wananchi ambao idadi yao haikupatikana walikamatwa na polisi na kupelekwa rumande.
Msimamo wa Wizara ya Nishati
katika hotuba yake jana, Profesa Muhongo alisema, “Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa Desemba, 2012 kulifanyika maandamano ya wananchi wa Mtwara wakitaka kujua faida ya kugunduliwa gesi asilia katika mikoa ya Kusini.
“Utashi wa wananchi ndiyo wa Serikali. Kama nilivyoelezea kwenye hotuba yangu, manufaa yatokanayo na uvunaji wa gesi asilia ni mengi. Hivyo, Serikali makini na sikivu imesikia, imeelewa na sasa inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuhusu manufaa hayo.
“Hata hivyo, ni muhimu ikaeleweka kuwa maandamano ya aina hiyo yanarudisha nyuma utekelezaji wa mipango ya Serikali inayolenga kuleta maendeleo ya wananchi na Taifa letu kwa ujumla.
“Hivyo, yakiendelea yanaweza kuwafukuza wawekezaji kwa kuhofia maisha yao, mali zao na mitaji yao. Umeme wa uhakika ni uchumi wa uhakika. Ndugu zetu wa Mtwara wasizuie ndugu zao wa Tanzania kupata umeme wa uhakika kwa uchumi wa uhakika,” alisema.
Spika aahirisha Bunge
Kikao cha Bunge ambacho kilipangwa kiendelee jana jioni kwa wabunge kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini, kiliahirishwa na Spika Anne Makinda.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Spika Makinda alisema uamuzi huo ulilenga kuipa nafasi Serikali kushughulikia mgogoro wa Mtwara.
Pia alisema uamuzi huo ulilenga “kutomwaga mafuta ya petroli kwenye moto”.
“Kama wabunge wangeendelea kuchangia, ingekuwa sawa na kumwaga mafuta kwenye moto unaowaka. Kamati ya uongozi tunakutaka kujadili jambo hili, na wakati huo huo Serikali nayo iandae taarifa kwa ajili ya kuiwasilisha bungeni kesho,” alisema.