Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) kimeiomba Serikali kuweka wakalimani wa lugha ya alama katika matukio muhimu ya kitaifa ili kulijumuisha kundi hilo katika michakato muhimu ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani inayoadhimishwa Desemba 3, kila mwaka, Mwenyekiti wa Chavita, Selina Mlemba, amesema mawasiliano mengi yanayofanyika kwenye vyombo vya habari yamekuwa yakiiacha mbali jamii ya viziwi.
“Hotuba za viongozi wa kitaifa hutolewa bila kuwapo wakalimani, mara chache tumekuwa tukipata viporo tena katika nyakati ambazo si sahihi.
“Hata mijadala muhimu ya kitaifa imekuwa ikipita bila kutufikia kama mjadala wa hivi karibuni wa gesi asilia ambao hatukujua kinachoendelea,” amesema Mlemba.
Chama hicho pia kimeiomba Serikali kuanzisha bodi itakayosimamia lugha ya alama huku kikivitaka vyombo vya habari kuzingatia mahitaji ya haki za watu wenye ulemavu kwa kuajiri wakalimani.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata), Jonas Lubago, amesisitiza urasimishwaji wa lugha ya alama uharakishwe pamoja na kamusi ya lugha ya alama kuwekwa mtandaoni.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Kanisa la Viziwi Tanzania, Mchungaji Joseph Hiza, amesema wanajisikia vibaya wanapokosa hotuba za Rais pale anapohutubia Taifa au kuzindua miradi mbalimbali.
“Rais anahutubia Taifa hatujuwi anachosema mpaka mtu baadaye aje kukuelezea tunakuwa wa mwisho kupata habari, tunajisikia vibaya,” amesema Hiza.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema suluhisho la mabadiliko kwa maendeleo jumuishi, nafasi ya ubunifu katika kuchagiza dunia fikivu na yenye usawa.