Soka la Tanzania litaendelea kushuka endapo juhudi za makusudi hazitafanyika na mamlaka husika kurudisha viwanja vyote vya michezo vinavyotumika kinyume na taratibu.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wadau wa soka, wanasema japokuwa soka la Tanzania linakabiliwa na changamoto nyingi, bado kuna tatizo la ukosefu wa viwanja vya michezo.
Katibu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ilala (IDRFA), Kanuti Daudi anasema soka la Tanzania lilichimbiwa kaburi kuanzia mwaka 1990 pale mamlaka husika ziliporuhusu uporaji wa maeneo ya wazi hapa nchini.
“Ndugu mwandishi miaka hiyo niliyoitaja mfano pale Jangwani kulikuwa na viwanja vipatavyo 21, na viwanja hivyo vyote vilikuwa na timu kuanzia za watoto na wakubwa,” anasema Daudi
Anasema wachezaji zaidi ya 600 walikuwa wakifanya mazoezi asubuhi na jioni, hali iliyoongeza uzalishaji wa vipaji.
“Nakumbuka baadhi ya timu zilizokuwa na viwanja pale Jangwani ni Simba, Yanga, Nyota Nyekundu, Ashanti, Polisi Dar, Nyota Afrika, Cosmo Politan, Young Technical, Saigoni na nyingine nyingi” anasema Daudi.
Anasema timu hizo zilikuwa katikati ya jiji hasa Kariakoo na vitongoji vyake, lakini pia maeneo mengine ya jiji kama Ilala, Sinza, Ubungo, Temeke mpira wa miguu ulikuwa ukichezwa.
Anasema hata mikoani mpira ulikuwa ukichezwa karibu kila mahali ndio maana katika miaka hiyo kila mkoa ulikuwa na timu ya ligi kuu iliyokuwa ikitoa upinzani wa kweli.
“Hebu ziangalie timu kama Mecco ya Mbeya, Pamba ya Mwanza, Majimaji Songea, African Sport, Cost Union za Tanga, Milambo ya Tabora, Reli ya Morogoro na nyinginezo. Zilikuwa ni timu zenye ushindani wa kweli tofauti na leo” anasema Daudi.
Anasema kutokana na uwepo wa viwanja vya michezo, mpira ulikuwa ukichezwa kuanzia ngazi ya chini hadi juu huko ndiko walikoibukia watu kama akina Peter Tino, Abdallah Kibaden, Leodgar Tenga, marehemu Omary Mahadhi na wengine.
Anasema tatizo lingine ni kufa kwa mashirika ya umma ambayo yalikuwa yakimiliki timu za mpira hali iliyochangia kukua kwa mpira nchini.
Anasema Timu kama Pamba ya Mwanza, Bandari ya Mtwara, Reli ya Morogoro, RTC Kagera na nyingine nyingi zilikuwa zikimilikiwa na mashirika ya umma lakini baada ya mashirika hayo kujiondoa katika michezo timu hizo zimepotea.
Anasema kama kweli nchi inahitaji kupata mafanikio katika michezo wa soka na mingine kuna haja ya kurejesha viwanja vyote vilivyoporwa.