Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Msomera
Jumla ya viwanja 10,000 vinatarajiwa kupangwa na kupimwa katika sehemu ya eneo lililokuwa Pori Tengefu la Handeni awamu ya pili kwa ajili ya wakazi wanaohamia kutoka hifadhi ya Ngorongoro.
Hayo yamebainishwa tarehe 7 Machi 2024 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda katika eneo linalotekelezwa mradi wa kupima viwanja na mashamba wakati wa ziara ya pamoja ya Mawaziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na ile ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye eneo la kijiji cha Msomera Handeni mkoa wa Tanga.
Mhe, Pinda amesema, kati ya viwanja hivyo viwanja 5000 ni kwa ajili ya makazi na 5000 ni mashamba. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi viwanja 2500 vya makazi vitapimwa kwenye kijiji cha Msomera, viwanja 1500 kijiji cha Kitwai B (Simanjiro) na viwanja 1000 kijiji cha Sauyi (Kilindi).
Aidha, amesema hadi kufikia februari 28 mwaka huu jumla ya viwanja 5,882 vimepimwa sawa na asilimia 118 ya lengo la kupima viwanja 5000 katika maeneo ya upangaji yaliyopo vijiji vya Saunyi (Kilindi) na Msomera (Handeni).
Amebainisha kuwa, kati ya viwanja hivyo, viwanja 5,272 ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi pekee na hivyo kuwa na ziada ya viwanja 610 ikilinganishwa na malengo ya upatikanaji viwanja 5000.
Mhe, Pinda ameweka wazi kuwa, zoezi la upimaji mashamba linaendelea katika kijiji cha Msomera ambapo hadi kufikia februari 28, 2024 jumla ya idadi ya mashamba 3,507 yamepimwa sawa na asilimia 70 ya lengo la kupima mashamba 5000 katika maeneo ya upangaji ya msomera, Saunyi na Kitwai.
“Ili kufikisha lengo la kupima mashamba yaliyobaki 1493 tunategemea kukamilika kazi ya uwandani ndani ya wiki mbili, kazi ya uandaaji wa mipangokina kwa ajili ya upimaji mashamba inaendelea”. Alisema Mhe, Pinda
Mhe, Pinda alimshukuru Rais Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuiwezesha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi vifaa alivyovieleza kuwa vimesaidia na vinaendelea kusaidia katika utekelezaji wa mradi katika eneo la kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe, Abdallah Ulega aliipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kazi kubwa na nzuri ya kufanikisha mipangpkina na hatimaye kupima mashamba na viwanja katika eneo la Msomera.
‘’Kazi imeonekana na tumeona kazi nzuri ambayo imekwisha kuanza na inaendelea ya upimaji viwanja na mashamba katika maeneo ya kilimo na mifugo katika eneo hili la Msomera ’’. alisema Ulega.
Hata hivyo, Mhe, Ulega amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kutoa elimu kwa watumiaji ardhi na kusisitiza kuwa, jambo hilo lazima liwe endelevu ili kuepuka matumizi holela ya ardhi na kusisitiza kuwa lazima ardhi isimamiwe ipasavyo.
Utekelezaji wa mradi wa kupanga na kupima katika eneo la Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga umefanikisha kuwaweka pamoja wageni wanaohamia kwa hiari kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wenyeji waliokutwa kwenye eneo la pori tengefu kuisha pamoja na pasipo migogoro yoyote.