Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), limezundua Maonesho ya Kimataifa ya Wazalishaji yajulikanayo kama TIMEXPO 2025

Maonyesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 22 Novemba mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam na yanatarajiwa kuhudhuriwa na waonyeshaji 4,000 na watembeleaji zaidi ya 35,000.

Picha mbalimbali za viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Mwenyekiti Hussein Sufian na Mkurugenzi Mkuu, Leodegar Tenga wakizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano wa uzinduzi wa maonyesho ya kimataifa ya wenye viwanda maarufu kama EXPO 2025 yanayotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo uliofanyika jana alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Suleiman Serera.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Dk Serera alisema Tanzania inazidi kupanda chini ya uongozi shupavu na wenye maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Serikali kuendelea kutekeleza mageuzi ya kina ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani, shirikishi na unaoendeshwa na teknolojia.

“Tunawekeza kwenye miundombinu. Tunafanya nishati ya kisasa, kuwezesha biashara, na kuweka dijitali. Tunapunguza gharama za kufanya biashara na kufanya kazi bila kuchoka ili kuiweka Tanzania kama kitovu cha viwanda kwa Afrika Mashariki na Kusini,” alisema.

Alisema marekebisho yaliyofanyika siyo ya mapambo kwani yanalenga kufungua fursa, kuvutia uwekezaji, na kutoa kazi zenye staha kwa watanzania.

Alisema sekta ya viwanda nchini Tanzania inakua na uwekezaji mkubwa umeendelea katika usindikaji wa mazao ya kilimo, vifungashio, dawa, nguo, vifaa vya ujenzi, na hata vifaa vya elektroniki.

“Kupitia Mkakati Jumuishi wa Maendeleo ya Viwanda (IIDS), FYDP III, na marekebisho ya udhibiti, tunaendelea kuweka kipaumbele katika ukuaji wa viwanda kama njia ya ukuaji jumuishi na ushindani wa kimataifa,” alisema.

Afrika sio tena bara la malighafi bali ni bara la masoko na watengenezaji wa bidhaa na kwamba kwa kuwa soko huru la Afrika AfCFTA linatumika sasa, watengenezaji wa bidhaa Tanzania wanaweza kufikia watumiaji bilioni 1.4 katika bara zima.

“Lakini ufikiaji pekee hautoshi lazima tuzalishe kwa kiwango kikubwa, chapa iliyo bor na kuuza nje kwa mkakati ndiyo maana TIMEXPO ni muhimu kwaajili ya kuuambia ulimwengu kwamba kuna bidhaa zinatengenezwa Tanzania. Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyowahi kusema: “Tanzania si maskini namimi leo nasema sisi ni matajiri,” alisema

Mkurugenzi Mtendaji wa (CTI) Leodegar Tenga alisema malengo ya maonyesho hayo ni kuonyesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini Tanzania kwenye masoko ya kimataifa.

Alisema EXPO 2025 itasaidia kuonyesha fursa za maendeleo ya viwanda yaliyopo ili kuendelea kuvutiwa uwekezaji wa nje na kukuza viwanda vya ndani ikiwemo kupata wabia wa nje ya nchi.

“Rais amefanyakazi kubwa sana kwenye miaka yake minne amevutia uwekezajiwa pande zote duniani, tumeona mitaji inakuja kutoka nje, teknolojia mpya kwa hiyo nawahamasisha wenye viwanda waje kwenye maonyesho waonyeshe bidhaa zao,” alisema Tenga