Kwa miaka 10 mfulululizo Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete hakutoa kipaumbele katika bajeti ya maendeleo hali iliyoathiri uchumi wa nchi na hivyo kudumaza uchumi wa mtu mmoja mmoja, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Mapitio ya kibajeti yanaonyesha kuwa Rais Kikwete alitilia mkazo matumizi ya kawaida badala ya maendeleo, ambapo baadhi ya wizara, mikoa na taasisi baadhi ya miaka zilikuwa zinapata fedha chini ya asilimia 10 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Vitengo muhimu vya kusimamia uchumi, Rais Kikwete alivitelekeza kwa baadhi ya nafasi za usimamizi kukaa hadi miaka mitatu kuwa na ama watu wanaokaimu au kutokuwa na watu kabisa, hali iliyoufanya uchumi kujiendesha kama gari bovu.
Hata hivyo, uchunguzi wa kina wa JAMHURI, umebaini kuwa vitendo nyeti au taasisi zilizomhusu, aliviwezesha kupata zaidi ya asilimia 90 ya bajeti vilizotengewa, ikiwamo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo mara zote ilipata bajeti asilimia 100 na wakati mwingine ilitumia zaidi ya ilichotengewa.
Maofisa waandamizi Serikalini, wanasema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ikulu na vitengo vyake vilipata bajeti karibu yote iliyotengewa kwa kuwa zilihusika moja kwa moja na matumizi binafsi ya Rais au safari za nje ya nchi zilizoligharimu taifa mamilioni ya fedha.
Kwa zaidi ya miaka miwili, mashirika nyeti kama Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limekuwa halina Bodi ya Wakurugenzi, ambapo ametumia mwanya wa kisheria kupitia kwa rafiki yake, Lazaro Nyalandu, kutumia kifungu kinachompa mamlaka Waziri na Katibu Mkuu kushauriana kufanya matumizi ya fedha za shirika na kwa muda wote wamefanya hivyo.
“Kama Rais [John] Magufuli anataka kufumbua jipu nene, basi aingie Wizara ya Maliasili na Utalii ashuhudie Nyalandu alivyotumbua fedha za walipakodi kwa kushirikiana na swahiba wake Rais Kikwete. Nakuhakikishia hata kama ana roho ngumu kiasi gani, atatokwa machozi. Yale si matumizi, ni balaa. Nyalandu anakwenda London mara mbili au tatu kwa mwezi kwa kutumia kodi zetu? Dah, hii haikubaliki,” kinasema chanzo cha JAMHURI.
Eneo jingine ambako Rais Magufuli anaweza kutokwa chozi ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Pale aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, Mzee Pius Msekwa alikwishaandaliwa hadi mashitaka kwa matumizi mabaya ya fedha za umma kwani katika vikao ilikuwa wanalipana hadi posho mara tatu, lakini habari za kina zinasema Kikwete alizuia asifikishwe mahakamani.
Habari kutoka Hazina, zinaonyesha kuwa Bajeti iliyokuwa inapitishwa bungeni ilikuwa kiini macho tu, kwani Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala na wakuu wa baadhi ya taasisi za serikali zinazotegemea bajeti ikiwamo Mahakama, walikuwa wanaumizwa kwa kupewa bajeti ndogo kuliko kiasi.
Wakati mwelekeo wa hesabu unaonyesha mwenendo ule ule kwa miaka karibu yote 10, kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, Ofisi ya Makamu wa Rais (mstaafu), Gharib Bilal iliyokuwa na jukumu la kusimamia Mazingira na Muungano ndiye alikuwa mhanga wa kwanza kwa kunyimwa fedha za maendeleo. Wakati Bunge lilimpitishia bajeti ya Sh 12,853,886,760, aliishia kupewa Sh 1,335,046,752 kama fedha za Maendeleo. Kiasi alichopewa ni sawa na asilimia 10.3, huku akikosa cha Sh 11,518,840,008 sawa na asilimia 89.7.
Waziri Mkuu (mstaafu) Mizengo Pinda, naye alipata maumivu sawa na Makamu wa Rais. Wakati Bunge liliipitishia Ofisi ya Waziri Mkuu 43,871,152,000, aliishia kupata Sh 21,621,854,268 sawa na asilimia 49.2 kiasi cha Sh 22,249,297,732 kilichosalia hakukiona.
Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Bunge liliitengea Sh 7,898,840,000 ikaishia kupata Sh 2,312,024,742 sawa na asilimia 29.2. Kiasi cha Sh 5,586,815,258 hakukiona. Hali iko hivyo kwa wizara karibu zote kiasi kilichopitishwa na Bunge na kiasi walichokikosa kama kilichowekwa kwenye mabano vinasikitisha.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilitengewa Sh 92,458,684,240, ikapata 68,446,159,512 (24,012,524,728), Viwanda na Biashara walitengewa 78,836,643,000, wakapata 44,532,182,577 (34,304,460,423), Elimu na Mafunzo ya Ufundi walitengewa 119,498,051,000, wakapata 48,403,308,014 sawa na asilimia 40.5 ya bajeti (71,094,742,986), Ardhi na Makazi walitengewa 70,072,349,000, wakapata 17,924,216,355 (52,148,132,645) na Maji na Umwagiliaji walipitishiwa 553,243,220,000, wakapata 235,212,755,970 (318,030,464,030).
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitengewa 471,282,941,000, ikapata 379,223,308,413 (92,059,632,587), Maendeleo ya Jamii, Jinsia & Watoto ilitengewa 11,910,672,000, ikapata 2,923,620,590 (8,987,051,410), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitengewa Sh 84,620,732,000, ikapata 40,152,600,020 (44,468,131,980) na Ulinzi na JKT ilitengewa Sh 229,582,027,000, ikapata 107,216,816,585 sawa na asilimia 46 (122,365,210,415).
Wizara ya Nishati na Madini ilitengewa Sh 1,176,412,745,000, ikapata 831,891,052,037 (344,521,692,963), Usafiri ilikuwa 409,220,820,000, wakapata 211,757,710,855 (197,463,109,145), Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilitengewa 33,847,235,000, ikapata 6,805,515,028 sawa na asilimia 20.1 (27,041,719,972) na Maliasili Na Utalii ilitengewa 11,648,166,000, ikapata 2,822,419,974 (8,825,746,026).
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ilitengewa 12,700,000,000, ikapata 8,327,500,000 (4,372,500,000), Wizara ya Ujenzi 853,725,979,000, ikapata 592,902,522,947 sawa na asilimia 69.4 (260,823,456,053) na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilitengewa 29,099,603,000, ikapata 16,083,661,145 (13,015,941,855).
Hata hivyo, wizara mbili zilineemeka. Hizi ni Wizara ya Fedha Bunge liliitengea 233,669,169,000, ikapata 225,068,875,750 sawa na asilimia 96.3 (8,600,293,250), huku Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilitengewa Sh 28,000,000,000, ikapata 25,465,800,000 sawa na asilimia 90.9 (2,534,200,000). Ingawa hizi fedha zinatajwa kama matumizi ya maendeleo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni za safari za nje kwa asilimia kubwa.
Kwa mikoa nako hali ilikuwa tete. Mkoa wa Katavi fedha za maendeleo ulipangiwa Sh 2,226,303,932, ukaishia kupata 1,386,576,901 (839,727,031), Simiyu ilipangiwa 3,106,896,553, ikapata 749,480,364 (2,357,416,189), Njombe 2,609,867,174, ikapata 1,564,379,709 (1,045,487,465), Geita 2,801,571,553, ikapata 1,450,724,849 (1,350,846,704) na Arusha 1,545,672,000, ikapata 834,589,943 (711,082,057).
Mikoa mingine kiasi ilichopangiwa, ilichopata na ilichokikosa kwenye mabano ni Pwani 1,196,292,000, ikapata 590,966,763 (605,325,237), Dodoma 5,045,596,000, ikapata 2,289,803,492 (2,755,792,508), Iringa 1,069,215,000, ikapata 639,865,937 (429,349,063), Kigoma 2,557,688,000, ikapata 1,334,057,603 (1,223,630,397) na Kilimanjaro 2,933,116,000, ikapata 1,861,999,010 (1,071,116,990).
Lindi 810,912,000, ikapata 412,712,807 (398,199,193), Mara 4,484,629,000, ikapata 2,066,081,000 (2,418,548,000), Mbeya 3,921,131,000, ikapata 1,042,595,542 (2,878,535,458), Morogoro 1,558,576,000, ikapata 831,905,294 (726,670,706), Mtwara 983,343,500, ikapata 587,186,661 (396,156,839) na Mwanza 983,929,000, ikapata 510,946,083 (472,982,917).
Ruvuma 1,927,732,578, ikapata 3,615,805 (1,924,116,773), Shinyanga 1,741,278,000, ikapata 792,901,766 (948,376,234), Singida 5,598,026,869, ikapata 2,692,257,170 (2,905,769,699), Tabora 3,035, ikapata 477,000 825,674,928 (2,209,802,072), Tanga 868,347,000, ikapata 481,632,203 (386,714,797), Kagera 1,649,832,000, ikapata 739,177,667 (910,654,333), Dar es Salaam 1,591,622,000, ikapata 656,904,615 (934,717,385), Rukwa 1,329,362,000, ikapata 728,245,310 (601,116,690) na Manyara 1,861,777,000, ikapata 777,425,098 (1,084,351,902).
Wakati wizara na mikoa ikipata bajeti ndogo, na hali ikiwa hivyo hivyo kwenye halmashauri kuhusiana na fedha za maendeleo, vitengo vilivyokuwa Karibu na Rais Kikwete, uchunguzi unaonyesha kuwa vilipata fedha za kutosha.
Taasisi ya Rais Inayosimamia Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ilitengewa Sh 25,000,000,000, ikapata 19,325,631,267 sawa na asilimia 77.3 (5,674,368,733), Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu kilitengewa 399,685,000, kikapata 394,066,380 sawa na asilimia 98.5 (5,618,620), Haki za Binadamu na Utawala Bora walitengewa 1,034,169,000, wakapata 790,894,135 (243,274,865)
Ofisi ya Rais Mipango ilitengewa 2,037,229,000, ikapata 800,100,000 (1,237,129,000) Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya 2,798,000,000, ikapata 1,499,129,152 (1,298,870,848) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) 15,344,335,000, ikapata 11,388,906,064 (3,955,428,936).
Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitengewa Sh 826,000,000 na haikupata hata senti tano (826,000,000), Hazina 37,989,725,000, ikapata 27,056,038,683 (10,933,686,317), Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali 7,161,747,000, ikapata 6,143,270,615 (1,018,476,385), Mambo ya Ndani 8,980,451,000, ikapata 3,837,350,200 (5,143,100,800), Magereza 2,666,566,000, ikapata 877,048,750 (1,789,517,250) na Ofisi ya Rais na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri ilitengewa 66,427,194,388, ikapata 62,417,194,388 sawa na asilimia 93.9 (4,010,000,000).
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma ilitengewa 19,320,000,000, ikapata 14,763,830,332 (4,556,169,668), Sekretarieti ya Maadili 3,083,544,000, ikapata 1,963,738,884 (1,119,805,116), Idara ya Mashtaka 2,167,759,000, ikapata 1,854,553,680 (313,205,320), Ulinzi 10,000,000,000, ikapewa 7,967,259,750 (2,032,740,250), Jeshi la Kujenga Taifa 6,000,000,000, likapewa 525,000,000 (5,475,000,000), Idara ya Mahakama 42,716,668,000, ikapewa 7,353,817,680 sawa na asilimia 17.2 (35,362,850,320). Hili ndilo limekuwa chimbuko la kesi kucheleweshwa nchini.
Idara ya Bunge nayo ilionja joto ya jiwe, kwani ilitengewa 8,899,600,000, ikaishia kupewa 1,793,750,000 (7,105,850,000) na Idara ya Uhamiaji ilitengewa 151,200,000,000, ikapewa 60,000,000,000 (91,200,000,000).
Uchunguzi unaonyesha kuwa katika misingi ya kupalilia matumizi yasiyohojiwa, kwa muda mrefu Ikulu chini ya Rais Kikwete imejiendesha bila maofisa au mifumo ya udhibiti wa matumizi hali iliyochangia fedha nyingi kutumika kiholela.
Taarifa rasmi ya Serikali inaonyesha kuwa Taasisi ya Rais ya kusimamia matokeo makubwa sasa (President’s Delivery Bureau (PDB), haikuwa na Meneja wa Kitengo cha Ununuzi wa Umma hadi kufikia Juni, 2014. Nafasi hii ilikuwa wazi kwa miezi 16. Pia hakuwapo Meneja Utafiti na Nyaraka kwa zaidi ya miezi 16, hakuwapo Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu – Ufuatiliaji na Tathmini na hakukuwapo Mkurugenziwa Miundombinu na maofisia wengine nyeti, hivyo mambo yalikuwa yanafanywa na watu wasio na sifa. Mbaya zaidi hata Meneja wa Huduma za sheria hakuwapo.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wizara ambazo zilikuwa na vipenzi wa Kikwete, zilikuwa zikitumbua kuliko maelezo. Mfano hai unatolewa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa mkutano wa Smart Partnership.
Serikali ilitoa malipo ya Sh 187,478,000 kwa M/S Simply Computers Tanzania Ltd kwa ajili ya manunuzi ya vifaa vya ofisi vya kuendeshea mkutano wa Smart Partnership. Hata hivyo, vifaa hivyo vilipokelewa Septemba 9, 2013 ikiwa ni miezi mitatu baada ya kukamilika kwa mkutano huo. Mkutano wa kimataifa wa Smart Partnership Dialogue wa mwaka 2013 ulifanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 31, 2013.
“Kutozingatiwa kwa bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya manunuzi ya tiketi za usafiri wa ndege. Bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya tiketi za usafiri wa ndege ilikuwa Sh 21,000,000, lakini kiasi halisi kilichotumika kwa tiketi hizo ni Sh.186,998,268; hivyo kupelekea matumizi zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa kwa Sh.165,998,268,” inasema sehemu ya taarifa rasmi ya Serikali.
Akizungumza kwa masikitiko na wafanyabiashara hivi karibuni, Rais Magufuli alirejea jinsi Serikali iliyopita ilivyokuwa imetekelezea maendeleo ya nchi hii kwa kusema: “Sijui kama mnafahamu, lakini ukweli ni kwamba tangu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2015/2016 ipitishwe Juni 30, mwaka huu, hakuna fedha yoyote iliyokwisha kutolewa kwenye wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
“Kama kutolewa, basi tutakuwa tumeanza kuzitoa kwenye wizara kuanzia mwezi huu (Novemba 2015), Katibu Mkuu Kiongozi yuko hapa, aseme. Miezi sita tangu bajeti hiyo ipitishwe, hakuna hata senti kwa ajili ya maendeleo iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya wizara yoyote, bali zilizokuwa zikitolewa ni zile za mishahara tu na kwenye shughuli nyingine.
“Kwa hiyo, ninapojaribu kusema haya na kusisitiza umuhimu wa ninyi kulipa kodi, hatufanyi haya kwa sababu ya jeuri, bali kwa nia njema ili malengo ya Watanzania yaweze kutimia.”
Uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa maendeleo ya nchi hii yamesimama kwa muda mrefu kutokana na fedha za maendeleo chini ya Serikali ya Rais Kikwete kutopelekwa wizarani na mikoani, hali iliyoifanya Tanzania kutopia hatua kwa kasi.