Kipenga cha uchaguzi kimepulizwa tangu Agosti 21, 2015 na refa ni Tume ya taifa Uchaguzi (NEC).
Kuanzia tarehe ile wachezaji wote ambao ni vyama vya siasa wamepaswa kucheza mchezo huu yaani kuandaa sera zao kwa wananchi kulingana na sheria ya uchaguzi na kanuni zake zilizoandaliwa kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu uwe huru na wa haki.
Nimesikia maneno mawili tofauti juu ya uchaguzi wa mwaka huu. Moja ni “Mtiti” sijalielewa. Neno hili mtiti linatumika katika kituo cha televisheni cha ITV katika kipindi cha kila Jumatano saa 3:30 usiku, kinaongozwana Sam Mahela kinaitwa “Mtiti wa Uchaguzi Mkuu”.
Ni kipindi kwa mtazamo wangu kinawapa fursa wagombea uongozi wa urais kumwaga sera zao na pia kujibu baadhi ya hoja zinazotolewa na wasikilizaji kwa manufaa ya Watanzania, wanapomuuliza mgombea anayezungumza katika kipindi cha siku husika kuelezea sera za chama chake.
Nina neno naona linafaa kututahadharisha wapiga kura juu ya wagombea urais kutoka vyama mbalimbali. Ni tahadhari zaidi kuliko onyo kwa maana ndiyo kwanza kampeni za uchaguzi zimeanza hivi majuzi tu Agosti 23, 2015.
Hizi ni nafasi nzuri sana kwa wagombea urais kunadi sera za vyama vyao kwa wananchi kupitia runinga. Wapiga kura waliojiandikisha kupiga hiyo kura. Nimeita vitimbi au vitimbwi kwa namna ninayoona yanayotokea wakati wa kujinadi wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini. Siyo vitendo vya kawaida hata kidogo. Wala siyo maigizo ya wasanii bali ni vituko halisi.
Kama nilivyosema awali mtiti wa uchaguzi neno lenyewe hilo sijalifahamu vizuri linamaanisha nini. Lakini neno vitimbwi naweza kulitolea maelezo kutokana na kamusi ya sarufi ya Kiswahili. Vitimbi au vitimbwi ningesema ni vioja au vituko au tabia inayotendwa na mtu, isiyoeleweka au isiyokuwa ya kawaida kwa mtu yeyote wa kawaida. Si kichekesho wala si maudhi bali ni cha kustaajabisha na pengine kinashangaza watu.
Vyama vyote vya siasa vimesaini maelewano (memorandum of understanding) kufuata mwongozo uliokubalika na vyama vyote namna ya kuendesha hizo kampeni zake. Kuna lugha mwafaka ya kutumia na kuna namna ya kusimamia upigaji kura na uhesabuji wa hizo kura hatimaye kupata matokeo ya kukubalika na vyama vyote vya siasa.
Kumbe wananchi wanatarajia kuona kampeni za kistaarabu kuanzia siku ya uzinduzi wa kampeni mpaka hiyo Oktoba 24, 2015 ya kufunga kampeni kusubiri upigaji kura tu hiyo Oktoba 25, mwaka huu. Kwa maana hiyo basi kuna siku zipatazo 60 za viongozi wetu kunadi majukwaani sera za vyama vyao. Je, ni hivyo kweli katika nchi yetu?
Wacheza mpira wote katika mechi muhimu wanapoanza wanakuwa na mori (sisi tunasema wanakuwa na presha ya juu kabisa) na wanakuwa na wasiwasi na ari ya kutaka kupata bao la kwanza na hapo kuwavunja moyo (demoralize) wapinzani wao.
Hapo tunaona vituko, ubabe wa kusukuma kukamiana na hata kucheza rafu na pengine kupiga mipira ovyo bila mwelekeo (no pattern). Basi utasikia makocha wanasema, wameacha kufuata mafunzo waliyopewa kwenye mazoezi, hawajatulia hata kidogo kuweza kutuonesha mchezo murua.
Kituko au kitimbwi cha kwanza nilikiona katika ule uzinduzi wa kampeni za CCM pale Jangwani. Waliwekwa wasemaji wengi na wakatumia muda mrefu kutoa maelezo ya kumnadi mgombea wa chama chao. Hali ile haikumpa muda mgombea wao wa CCM kunadi sera za chama chake kwa mujibu wa Ilani ile ya Chama.
Hili nalisema kwa vile utaratibu wa Tume kwa muda wa kujinadi mgombea unamalizika saa 12:00 jioni. Kupitiliza muda huo ni uvunjaji wa kanuni za uchaguzi, ni kosa. Hiyo ni rafu ya wazi wazi na refa anapaswa kutoa kadi ya njano kwa chama husika – kuonya.
Imeandikwa katika magazeti kuwa uzinduzi ule ulianza adhuhuri majira ya saa 7 hivi, na ukamalizika au kufungwa mnamo saa 12:30 jioni. Kumbe kati ya muda ule wa saa 8-10 ungetosha kabisa viongozi kumtambulisha huyo mgombea wao wa CCM na kuanzia saa 10:30 mpaka saa 11:45 hivi ungetosha kwa mgombea kunadi sera za chama chake.
Rekodi za waandishi wa habari zimeonesha mgombea wa CCM alianza kuongea saa 11:40. Kwa maana hiyo alipewa dakika 20 tu kunadi sera za chama. Ni dhahiri muda huo haungemtosha mgombea yeyote kutoa au kumwaga sera za chama. Ilani ya uchaguzi ni kubwa hata uwe hodari namna gani kuifupisha (to condense it) kama presii (precis) mtu hangalifanikiwa kwa muda ule wa dakika 20 tu.
Basi hapo chama kinajiingiza katika mazingira ya kushawishika kuongeza muda wa mkutano. Hicho ni kinyume cha sharia, ni uvunjaji wa kanuni zilizokubalika, basi ni utovu wa nidhamu. Imedhihirika bayana kabisa kikao kile cha uzinduzi kilihitimishwa saa 12:33 jioni.
Kwa muda huo mgombea wa CCM alipata kutumia dakika 53 hivi kunadi sera za chama chake! Hapo nani alaumiwe? Uongozi! Maana walikuwa na muda kuanzia saa 8-12 takribani saa 4 kamili za chama kujinadi na kumpa mgombea wake muda wa kutosha kuzungumza na pengine hata kujibu baadhi ya maswali kutoka wapiga kura wenye shauku ya kutaka ufafanuzi wa jambo hili au lile kati ya yale yaliyosemwa pale. (Tazama Mwananchi Toleo No. 5508 la Jumatatu Agosti 24 mbele kabisa uk. 1 ‘Magufuli ataja vipaumbele 25’ kati ya saa 11:40-12.33 ni muda wa dakika 53 tu). Hivyo mimi nakiona ni kituko kimojawapo cha uchaguzi wa mwaka huu.
Kituko cha pili nilichokiona ni kile cha mgombea urais kutoka Ukawa akisafiri kwa mabasi ya daladala Ukonga/Gongo la Mboto/Mbagala ili kuonja adha wapatazo wananchi wa Dar es Salaam katika usafiri. Mimi nakiita kituko maana haijapata kutokea kiongozi yeyote hapa nchini eti apande daladala! (Tazama Raia Tanzania toleo Na. 0448 la Agosti 25, 2015). Kuona adha za walalahoi. Huko ni kujisingizia kuona huruma (sympathize with) wananchi.
Ni aina yake ya maandalizi ya uzinduzi wa kampeni zake, cha kustaajabisha hapa ni lile wazo la kwenda kuonja maisha ya wanyonge. Haijapata kutokea hata enzi za mababu zetu Wayahudi wakati wa Bwana wetu Yesu Kristo, kiongozi kwenda kwa wanyonge kuonja wanavyoishi, ili aje awatatulie dhiki zao.
Tunajua fika, wakoma enzi za Bwana Yesu walikuwa wakitengwa kabisa na jamii, lakini haijapata kusikika eti kuhani au kiongozi wa Mayahudi kwenda kuishi nao. Tunachokijua ni kuwa wakoma wenyewe walimwendea Yesu wakilia na kumuomba awaonee huruma na awaponye. Tunasoma haya katika Marko sura ile ya I mstari ule wa 40 hivi, “akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigiai magoti na kumwambia “ukitaka waweza kunitakasa”. Tena tunasoma katika kitabu cha Luka sura ile ya 17 mstari ule wa 12 “Na alipoingia katika kijiji kimoja alikutana na watu kumi wenye ukoma wakasimama mbali wakapaza sauti wakisema, ee Yesu Bwana mkubwa uturehemu” (Luk. 17: 12 – 13) ndio utaratibu hapa duniani.
Kwa kutafakari hizo nukuu kutoka maandiko matakatifu (Biblia), mimi naona ni kituko kwa kiongozi mkubwa wa nchi, Waziri Mkuu mstaafu wakati huu wa uchaguzi kwenda kupanda daladala eti analenga kujifunza shida za walalahoi! (Taz. Raia Tanz. Toleo No. 0448 la Jumanne Agosti 25, 2015 uk. mbele). Kwani alipokuwa Waziri Mkuu wa nchi hii hakuwahi kusikia matatizo ya wanyonge? Kulikuwa na matatizo ya umeme katika nchi, hayo hakuyasikia? Kwa nini wakubwa hawa hawakupanda dalada wakati ule waje wapande leo?
Ninajiuliza vituko namna hii wakati wa maandalizi ya kuomba kura yanaashiria nini? Miaka yote hii shida za wanyonge hazikujulikana? Kwanini zifikiriwe sasa? Maadam utaratibu wa kuendesha kampeni uliokubalika na vyama vyote vya siasa hapa nchini unajulikana, hakuna sababu za kuanza kucheza rafu sasa. Mahali pa kampeni patajwe, muda uelezwe, wagombea waende kujieleza kule. Lakini siyo aina hii ya kuandaa mvuto wa wananchi kuungwa mkono.
Kule nchi za Magharibi wanakubaliana njia moja nzuri sana, hata mimi ninaiafiki. Wagombea wote wanakuwa na midahalo pamoja na msimamizi kutoka taasisi ya habari kama vile BBC au VOA. Wanapangiwa siku na muda wa kuja kujieleza katika ukumbi ulioandaliwa na hupewa jambo la kulielezea. Mathalani uchumi wa nchi au ajira katika nchi au maendeleo ya Taifa na kadhalika. Tuliona katika runinga midahalo namna hiyo.
Katika uchaguzi kule Uingereza viongozi wa vyama sita hivi walionekana katika mdahalo namna hiyo wakielezea sera zao na kujibu maswali ya wananchi. Kule Marekani wagombea wapatao tisa wa Chama cha Republican wamekuwa na mdahalo namna hiyo kwa kumtafuta mgombea mmoja tu wa chama hicho kupambana na Democrats katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2016.
Hapa Tanzania, je, Tume ya Uchaguzi au vyombo vya habari haviwezi kuwapambanisha wagombea wetu katika mdahalo namna hiyo? Wangeweza tu kuelezea sera za vyama vyao ili wapiga kura tuweze kuwapiga masuali. Kuna ugumu gani?
Aidha, kuna kituko kingine nimekisikia. Ni sakata la Uwanja wa Jangwani kwa watu wa Upinzani. Kila walipouomba kumetokea mizengwe! Hee, jamani pale ni viwanja vya wazi, kila chama kinaweza kuutumia kwa shughuli zake mradi wanalipia gharama zote kwa mamlaka husika. Kwa visingizo leo hiki kesho kile ili mradi wengine wasivitumie viwanja vile ni sawa hiyo?
Kama chama fulani kiliruhusiwa kutumia kwa masharti yale yale na vyama vingine viutumie uwanja huo ni haki ile ile kwa wenye hitaji namna ile ile. Ninafurahi kusikia Ukawa wamefanikiwa kuzindua kampeni zao hapo hapo penye viwanja vya Jangwani. Wenye macho wameona na wenye masikio wamesikia. Kilichobakia ni uamuzi wa dhamiri yako wewe binafsi kura yako utampa nani.
Kituko kingine ni kile nilichokisoma katika gazeti moja. Hiki kimeandikwa hivi, “Lakini kituko walichofanya CHADEMA kwa kile alichosema Mwenyekiti wao Freeman Mbowe kuwa wamebadilisha gia angani na kumfanya Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea urais kupitia UKAWA ni cha hatari kwenye siasa” (soma Raia Tanzania Toleo No. 0448 Jumanne Agosti 25, 2015 uk. 21 safu ya kwanza ibara ya pili).
Mwandishi wa makala hii amechambua mengi kuhusu hilo. Ameweza hata kujiuliza maswali namna hii sasa tujiulize Chadema kumpa Lowassa nafasi nzito kama hiyo ya kupeperusha bendera, tena si ya chama kimoja bali vinne, ni lini mmemfanyia vetting? Chadema pia na wao wamemfanyia mgombea huyo kwa kumnyofoa kwenye nafasi hiyo bila kufuata sheria.
Lakini kituko hiki kilichofanywa na Chadema kinakwenda mbali zaidi kihistoria. Mwandishi anaturudisha nyuma kabla ya Uhuru wa Tanganyika. Hapo anatukumbusha azma ya watu wa ukanda wa kaskazini anasema haya, ninamnukuu “Ila tangu mfumo wa vyama vingi umeanza nilikuwa najiuliza mbona vyama vingi vinaanzishwa kama siyo kushamiri upande mmoja wa kaskazini mwa nchi? Halafu wakati mwingine unakuta mwenyekiti wa chama Taifa anakuwa na mbunge mmoja, na wakati mwingine huyo huyo ndiyo anakuwa mbunge pekee wa chama hicho. Wengine hata ofisi hawana lakini unaambiwa huyo ndiyo mwenyekiti wa chama kitaifa!
>>ITAENDELEA