Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Geita
Maneno matupu hayavunji mfupa. Msemo huu hulenga kuihamasisha jamii kuchukua hatua sahihi za kiutendaji ili kufikia malengo kusudiwa badala ya kuzungumza sana pasipo utekelezaji wowote.
Kwa muda mrefu jamii imekuwa na mtazamo wa shaka katika utekelezaji wa mambo kadha wa kadha kutokana na baadhi ya viongozi kuwa na maneno mengi yasiyo na utekelezaji ndani yake.
Ndiyo maana si ajabu watu kuahidiwa jambo kisha ukasikia wakisema: “Hiyo ni siasa tu!” Wakimaanisha hakuna ukweli katika jambo linalosemwa isipokuwa ni maneno matamu yenye kutafuta namna ya kuwalainisha ili mhusika atimize azima yake kwa wakati huo.
Sasa wakati umefika wa kuachana na mitazamo hiyo iwapo tuna nia njema ya kulijenga taifa katika ukweli, haki na uzalendo kwa manufaa mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.
Watanzania wanataka kuona taifa likistawi katika nyanja tofauti kama elimu bora, afya bora, kilimo bora, uvuvi bora, ufugaji bora na uongozi bora. Kwa ujumla ni kwamba watu wanataka kuyapata maisha bora.
Tunaamini msingi mkuu wa maisha hayo mazuri unapatikana iwapo kutakuwa na uongozi bora wenye dhamira ya kweli pamoja na siasa safi.
Aidha, kwa kiasi kikubwa nchi yetu tunaipongeza kwa baadhi ya hatua za kimaendeleo ambazo zinaendelea kuonekana ili kuyasogelea maisha bora kwa kila Mtanzania.
Lakini tutambue kuwa ili tuweze kufika salama tuendako, makundi yote yaliyopo kwenye jamii ni muhimu yakatendewa haki badala ya wengine kudhani hayana mchango wowote katika safari hiyo.
Na kwamba kuyafikia mafanikio ya kweli hakuna njia ya mkato, lazima tukubali kuumia ili baadaye tufurahie matunda ya kuumia kwetu, na katika maumivu hayo muhimu tukubali kuwatibu walioumia safarini badala ya kuwatelekeza msituni.
Makala hii inajikita kuwaangazia wenzetu walioumia safarini na kupata madhara makubwa na wengine kukumbwa na changamoto mbalimbali kabla ya kufika mwisho wa safari yetu.
Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani, huadhimisha siku ya afya ya akili ikiwa ni kuendelea kuihamasisha jamii kutambua, kulinda na kulithamini kundi hilo katika jamii kuliko kuwabagua na kuwatelekeza.
Waswahili wanasema; kila aliye mzima leo huenda kesho ndiye mgonjwa wa akili, ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya watu wenye changamoto hiyo walikuwa wazima kabisa kabla ya kukumbwa na kadhia hiyo.
Licha ya jamii kuwa na mitazamo tofauti kwa kundi hili, wataalamu wa afya wanasema kwa kiwango kikubwa tatizo la afya ya akili linatibika na kupona iwapo mgonjwa atahudumiwa kikamilifu na kupata msaada wa kisaikolojia.
Abebeshwa mimba Biharamulo
Mwandishi wa makala hii amezungumza na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gwabya, Biharamulo, mkoani Kagera, Paulo Kaboja, anayemwelezea kuhusu mlemavu wa afya ya akili ambaye alibebeshwa mimba na watu wasiojulikana kisha kumtelekeza mtoto wake kabla ya wasamaria wema kumuokota.
Mlemavu huyo ambaye hakufahamika jina lake inaelezwa alifika kwenye kitongoji hicho mwaka 2021 na kuanza kuishi mitaani huku akila vyakula vichafu na kulala kwenye maboma mabovu ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Mbali ya kula na kulala pasipofaa, inaelezwa alikuwa akivaa nguo zilizoraruka na wakati mwingine kubaki uchi wa mnyama pasipo kupata msaada wa huduma za kiafya.
Kaboja anasema baada ya mwaka mmoja wa maisha ya mlemavu huyo wa akili, alishangazwa kuona mabadiliko ya kimaumbile ambayo yalidhihirisha wazi kuwa ni mjamzito na baada ya muda mfupi alijifungua mtoto ambaye baba yake hajafahamika.
Hata hivyo, alimtelekeza mtoto wake mwenye umri wa mwezi mmoja na kutokomea kusikojulikana pasipo kujua hatima ya maisha ya kichanga hicho.
Diwani wa Viti Maalumu, Ziyun Hussein, anasema alilazimika kumchukua mtoto huyo kwa ajili ya matunzo ya awali ili kunusuru maisha yake ambayo yalikuwa hatarini kutokana na kukosa huduma muhimu za mama, ikiwamo maziwa, mavazi na matibabu.
“Baada ya kichanga hicho kutelekezwa na mlemavu wa akili, nililazimika kukichukua ili nisaidie matunzo ya awali kabla serikali haijapata ufumbuzi wa kubeba jukumu la malezi na makuzi ya mtoto huyo,” anasema.
Emmanuel Michael, mkazi wa Kijiji cha Kitela Kata ya Chato, anasema unyanyapaa na ukatili kwa watu wenye changamoto ya akili ni mkubwa sana na hakuna jitihada zozote za kukabiliana na kadhia hiyo.
“Watu wenye ugonjwa wa akili hawathaminiwi kabisa kwenye jamii. Utakuta mtu anatembea utupu, wala hakuna jitihada za kumuwahisha kwenye vituo vya afya ili atibiwe.
“Wengine pia hawajui kama changamoto ya akili inaweza kutibiwa hivyo huamua kumtelekeza mgonjwa na kumuacha akirandaranda ovyo mitaani,” anasema Michael.
Msadizi wa kisheria kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la CHALAO, Hamis Mwitazi ‘Burebure’, anaitaka serikali kuja na mwarobaini wa kupunguza ongezeko la magonjwa ya akili katika jamii, sambamba na umma kuelimishwa kwa kina umuhimu wa kuwasaidia watu wenye kadhia hiyo.
“Kwa bahati mbaya baadhi ya watu huamini ugonjwa na changamoto ya akili hutokana na kulogwa, laana na wengine wakidai ni ugonjwa usio na tiba,” anasema.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba jamii kubwa haina uelewa mpana kuhusiana na changamoto ya afya na ugonjwa wa akili, hali inayosababisha jamii kuwatenga, kuwanyanyapaa, kuwatendea ukatili na kutowapa mahitaji muhimu kwa afya ya binadamu.
“Lazima tukubali kuwa hatujawatendea haki watu hao, kwani nao ni binadamu kama sisi na isitoshe wengine wamekumbwa na changamoto hiyo wakiwa kwenye utumishi wa umma, sekta binafsi na wengine wamezaliwa na tatizo hilo,” anasema Mwitazi.
Daktari Bingwa afya ya akili
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Said Kuganda, akizungumza na mtandao wa kijamii wa Matukio na Maisha, anasema magonjwa ya akili yanatibika na kwamba jamii inapaswa kuwapeleka hospitalini watu wote wenye changamoto hiyo badala ya kuwafungia ndani na wengine kutelekezwa mitaani.
“Magonjwa haya yapo mengi na mengine husababisha kuchanganyikiwa. Lakini ni muhimu watu watambue kuwa yapo magonjwa ya akili ambayo ni ya kurithi na mengine hutokana na changamoto za maisha.
“Tatizo kubwa bado lipo kwenye uelewa mdogo wa jamii. Unakuta mgonjwa au mwenye changamoto ya afya ya akili anapelekwa hospitalini baada ya miaka miwili na zaidi, tena baadhi yao huanzia kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli wakiamini ndugu yao amelogwa, jambo ambalo si kweli,” anasema.
Dk. Kuganda anasisitiza kuwa upo uwezekano mkubwa kwa wagonjwa wa akili kutibiwa na kupona iwapo watafikishwa hospitalini mapema na kwamba jamii inapaswa kubadilika na kuwathamini watu wenye changamoto hiyo badala ya kuwatelekeza ovyo.
Dalili za ugonjwa
Dk. Kuganda anasema zipo dalili zinazoweza kujitokeza kwa mtu anayeelekea kuchanganyikiwa, ikiwa ni pamoja na kusikia sauti nyingi zinazomsemesha wakati wengine hamzisikii.
Anaweza kuhisi anaona vitu ambavyo ni hatari au vinavyomfurahisha pasipo wengine kuviona na hujikuta akichukia au akicheka peke yake na/au kuongeaongea.
“Wengine hulazimika kuvaa nguo zaidi ya moja na hupoteza hamu ya kuoga na kufua nguo, kubeba mizigo, kujitenga na hata kula vyakula visivyofaa kuliwa na watu wengine,” anasema Dk. Kuganda.
Kadhalika anaishauri jamii inapoona ndugu au jamaa ana dalili miongoni mwa hizo, kuwa ni muhimu kuwawahishwa kwenye vituo vya kutolea tiba ili uchunguzi wa kitaalamu na kisaikolojia ufanyike haraka ili kutatua tatizo mapema.
Kauli ya Waziri wa Afya
Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari katika kuadhimisha ‘Wiki ya Afya ya Akili’ Mkoa wa Dar es Salaam mwaka jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anasema takwimu za kidunia kwa mwaka 2021 zinaonyesha kuwa tatizo hilo ni kubwa ambapo takriban watu milioni 970 wameathiriwa na magonjwa hayo.
“Magonjwa ya akili yanaongezeka kwa kasi na kati ya watu wanane mmoja ana tatizo la akili huku Tanzania ikikadiriwa kuwa na watu milioni saba wenye tatizo hilo, kati yao takriban milioni 1.7 wakisumbuliwa na sonona,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, akataka huduma za afya ya akili na wataalamu wa saikolojia tiba zipatikane kuanzia ngazi ya zahanati na hospitali za wilaya, mikoa na za kitaifa.
Ummy akataja baadhi ya magonjwa ya akili yanayosumbua zaidi nchini kuwa ni sonona, kihoro, kizofrenia, matumizi ya bangi, milungi na unywaji pombe kupita kiasi.
Pia anaeleza sababu za watu kukumbwa na ugonjwa huo kuwa ni kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha, kuzaliwa na vinasaba, vilevi, magonjwa ya mwili kama ukimwi, malaria kali, msongo wa mawazo wa kiwango cha juu, shinikizo la makundi rika na matukio yenye tishio la maisha kama majanga, ukatili, unyanyasaji na migogoro.
“Tumeona takwimu za watoto kujiua na tumeambiwa na WHO kifo kimoja kati ya 100 hutokana na kujiua. Kwa hiyo asilimia 50 ya kesi hizo zinatokea kabla ya umri wa miaka 50, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa uchumi wa taifa,” anasema Ummy.
Nini kifanyike?
Kwa kuwa mamlaka imelitambua tatizo la afya ya akili lilivyo kubwa katika jamii, tunaamini ni wakati muafaka wa kupeleka huduma za matibabu kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Serikali iwe na matashi ya dhati kupambana na tatizo la afya ya akili kwa jamii badala ya mipango mingi isiyokuwa na utekelezaji.
Serikali itenge fedha za kutosha kuzisaidia tasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) kutoa elimu kwa jamii kubwa ili itambue kuwa magonjwa na changamoto za afya ya akili vinatibika.
Wagonjwa wa akili wanaozurura mitaani wachukuliwe na kupelekwa kwenye huduma za kutolea matibabu kwa ajili ya uchunguzi na ushauri. Wapate tiba pasipo ndugu na jamaa zao kudaiwa gharama za matibabu.
Jamii ijiepushe na visababishi vya ugonjwa wa afya ya akili, ikiwamo uvutaji wa bangi, milungi, unywaji pombe kupita kiasi, pamoja na kujenga tabia ya kueleza wazi kuhusu changamoto zinazomfanya mtu kukosa furaha na kuwaza sana.
Madaktari na wanasaikolojia tiba wapelekwe kwenye vituo vya kutolea tiba, sambamba na ujenzi wa miundombinu ya afya, pia kuzingatia uwepo wa wodi maalumu kwa watu wenye afya ya akili.
Jeshi la Polisi lishirikiane na jamii kuwabaini watu wanaowatendea ukatili walemavu wa akili kwa kuwabebesha mimba na kuwatelekeza pasipo matunzo ili wafikishwe mahakamani kwa hatua za kisheria.